Sunday, February 5, 2017

SISITIZO LA KUPANULIWA USHIRIKIANO WA KUNDI LA 20 NA NCHI ZA AFRIKA

Nchi za kundi la 20 zimetaka kupanuliwa ushirikiano na nchi za Kiafrika.
Kikao cha siku tatu cha Mawaziri wa Utalii wa kundi la 20 na wawakilishi wa mataifa ya Kiafrika kilihitimisha shughuli zake Ijumaa iliyopita mjini Johennesburg Afrika Kusini. Katika kikao hicho, Ujerumani kama mwenyekiti wa kundi hilo ilitaka kuimarishwa ushirikiano wa muda mrefu baina ya nchi za kundi la 20 na mataifa ya Afrika. Mwakilishi wa Ujerumani sanjari na kusisitizia mpango wa ustawishaji  bara la Afrika unaoitwa ‘Agenda ya 2063 alisema kuwa, Afrika na nchi za kundi la 20 zinatakiwa kufanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuinua kiwango cha ushirikiano wa pande mbili. Kikao cha mjini Johennesburg sanjari na kuashiria nafasi chanya ya Afrika duniani, kimesisitiza pia juu ya ubunifu wa mipango zaidi ya kisasa kwa ajili ya nchi za bara hilo.
Baadhi ya viongozi wa nchi za Kiafrika
Kundi la 20 huandaa mijadala huru baina ya nchi za viwanda na zinazoinukia kiuchumi, kuhusiana na uthabiti wa uchumi wa dunia. Kundi hilo huunga mkono ukuaji wa uchumi na ustawi katika nchi mbalimbali za dunia lengo kuu likiwa ni kuzishirikisha nchi wanachama katika kuimarisha muundo wa masoko ya kifedha ya kimataifa na kadhalika kuandaa mazingira ya mazungumzo kuhusu sera za fedha na ushirikiano wa kimataifa.
Nchi wanachama za kundi hilo zinamiliki asilimia 90 ya pato jumla, asilimia 80 ya biashara ya dunia na theluthi mbili ya idadi ya watu wote duniani. Sisitizo la kupanuliwa ushirikiano na nchi za Kiafrika lina maana kwamba, kutumia nguvukazi ya vijana na vyanzo vyake asilia kutasaidia nchi hizo kuinukia kiuchumi katika medani ya kimataifa. Hii ni kusema kuwa hivi sasa nguvukazi barani Afrika inaongezeka kwa kasi. Hivyo ikiwa nchi za Kiafrika zitaweza kuwadhaminia vijana wao mahitaji ya elimu na ujuzi, basi nguvukazi hiyo kubwa itasaidia katika kuinua uchumi wa mataifa hayo. Hivi sasa uwekezaji wa kigeni umeongezeka zaidi barani Afrika kuliko eneo lolote lile duniani.
Nguvukazi ya vijana wa Afrika
Chunguzi zinaonyesha kwamba, matarajio ya ukuaji uchumi wa muda mrefu kutokana na mahitaji ya kigeni na mabadiliko ya ndani barani Afrika, ni mambo yanayopewa umuhimu mkubwa. Mbali na hayo bara la Afrika linategemewa sana kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji ya dunia katika sekta ya mafuta, gesi asilia, madini, chakula, mazao ya kilimo na vyanzo vingine asilia. Hii ni kusema kuwa bara hilo linamiliki asilimia 10 ya akiba ya mafuta duniani, asilimia 40 ya akiba ya dhahabu na asilimia 80 hadi 90 ya madini mbalimbali. Ni kwa msingi huo ndio maana ikaaminiwa kuwa ukuaji uchumi barani Afrika unaweza kuandaa fursa za kutosha za ajira kwa nchi za bara hilo. Kama ambavyo kilimo pia kinaweza kuandaa nguvu kubwa kwa ajili ya mashirika makubwa katika sektka hiyo.

No comments:

Post a Comment