Tuesday, February 7, 2017

UCHAGUZI WA RAIS SOMALIA KUFANYIKA LEO, WAGOMBEA 22 WANACHUANA

Uchaguzi wa rais nchini Somalia unafanyika leo ukiwashirikisha wagombea 22 baada ya kuakhirishwa mara kadhaa.
Uchaguzi huo wa Rais wa Somalia uliakhirishwa kwa sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na kuongezeka vitisho vya kundi la kigaidi la al Shabab na wasiwasi wa usalama katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Ripori zinasema, kwa kuzingatia hali hiyo pia wabunge 275 na maseneta 54 wa Somalia wanatazaniwa kupiga kura katika eneo maalumu lenye ulinzi mkali katika uwanja wa ndege wa Mogadishu. 
Ripoti zinasema, kuna uwezekano mkubwa kwamba, uchaguzi huo utaingia duru ya pili kutokana na ukweli kwamba, ni vigumu kwa mgombea yeyote kupata thuluthi mbili ya kura zinazohitajika katika duru yake ya kwanza.
Mji wa Mogadishu siku moja kabla ya uchaguzi wa rais
Mchuano mkubwa zaidi unatazamiwa kushuhudiwa kati ya Rais wa sasa wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, Waziri wake Mkuu, Omar Abdirashid Ali Sharmarke na rais wa zamani wa Somalia Sharif Sheikh Ahmed.
Maafisa wa eneo linalojitawala la Somaliland wametangza kuwa, eneo hilo halitashiriki katika uchaguzi wa leo wa rais. Eneo hilo limekuwa likifanya jitihada za kujitenga na Somalia lakini hadi sasa suala hilo halijakubaliwa na jamii ya kimataifa.
Mogadishu
Usalama umeimarishwa sana mjini Mogadishu na maeneo mengine ya nchi hiyo kwa ajili ya kudhamini usalama wa wapiga kura.

No comments:

Post a Comment