Saturday, February 11, 2017

KIONGOZI MUADHAMU : MATATIZO YOTE YA M/KATI YANASABABISHWA NA MAREKANI

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema, matatizo yote ya eneo la Mashariki ya Kati ni uingiliaji wa baadhi ya madola makubwa ikiwemo Marekani katika masuala ya ndani ya eneo hili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo leo jioni wakati alipoonana na Stefan Löfven, Waziri Mkuu wa Sweden hapa mjini Tehran na kusisitiza kuwa, Marekani na madola mengine mengi ya Ulaya yamehusika moja kwa moja katika matukio machungu ya nchini syria na Iraq na kwamba wananchi wa eneo hili wamekasirishwa mno na uingiliaji wa madola hayo ya kibeberu.
Amesema, utatuzi wa matatizo ya eneo hili inabidi ufanywe na wananchi wenyewe wa Mashariki ya Kati na huku akiashiria namna hali inavyorejea kuwa ya kawaida nchini Iraq amesema, mgogoro wa Syria nao unaweza kutatuliwa kwa njia hiyo hiyo na hilo litawezekana iwapo tu wanaowaunga mkono magaidi wataacha kufanya hivyo.
Mazungumzo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Waziri Mkuu wa Sweden

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kitendo cha baadhi ya mabalozi wa nchi za Magharibi cha kushirikiana na wapinzani wa serikali ya Syria na kuwapa silaha waziwazi mwanzoni mwa mgogoro wa nchi hiyo ni mfano wa wazi wa uingiliaji wa madola ya kibeberu katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Amesema, kuna wajibu wa kujua kwanza chanzo cha mgogoro huo ndipo zichukuliwe hatua za kuutatua.
Ayatullah Khamenei amegusia pia safari za mara kwa mara za viongozi na maafisa wa serikali za Ulaya hapa mjini Tehran katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita lakini pamoja na hayo, sehemu kubwa ya maafikiano yanayofikiwa hayajatekelezwa kivitendo na kumwambia Waziri Mkuu wa Sweden kwamba: Kutokana na welewa nilio nao juu yako, ni kwamba wewe ni mtu wa kuchukua hatua na kufanya mambo kivitendo, hivyo tunachokitarajia ni kuona utekelezaji wa kivitendo wa maafikiano yanayofikiwa na isiwe ni makubaliano yanayoishia kwenye makaratasi tu.
Mazungumzo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Waziri Mkuu wa Sweden

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia kura ya ndio iliyopigwa na Iran kwa ajili ya kuchaguliwa Sweden kuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, Baraza la Usalama ni chombo muhimu sana ambacho kwa bahati mbaya kimekuwa mateka wa baadhi ya madola makubwa ya kibeberu. Hata hivyo upo uwezekano wa kukizuia chombo hicho kuchukua maamuzi ya kugongana na ya kindumilakuwili.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameitaja hamasa ya kupigiwa mfano iliyooneshwa na wananchi wa Iran katika maadhimisho ya Bahman 22 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu jana Ijumaa na kusisitiza kuwa: Maadhimisho ya mapinduzi mbalimbali duniani hufanyika kimaonyesho na kwa gwaride la jeshi kwenye eneo moja maalumu lililohudhuriwa na baadhi ya watu tu, lakini maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ambayo ni ya wananchi wenyewe; kwa hakika ni sherehe za kweli za kitaifa zinazofanyika kona zote za Iran ambazo zinawashirikisha watu wa matabaka yote.

No comments:

Post a Comment