Sunday, March 26, 2017

HRW YATAKA RAIS WA SUDSN SZUIWE KUINGIS JORDDN AU AKAMATWE

Shirika la kimataifa la Haki za Binadamu HRW limetaka Rais Omar al Bashir wa Sudan azuiwe kuingia nchini Jordan.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, Human Rights Watch imetoa tamko la kuitaka serikali ya Jordan imma imzuie Rais Omar al Bashir kutembele nchi hiyo au imtie mbaroni mara atakapowasili nchini humo.
Taasisi hiyo ya kimataifa isiyo ya kiserikali imegusia tuhuma zinazomkabili Rais wa Sudan za kuhusika katika jinai za kivita za jimbo la Darfur la magharibi mwa nchi hiyo na kuitaka serikali ya Jordan iheshimu makubaliano ya kimataifa.
Katika tamko lake hilo Human Rights Watch imesema, kwa vile Jordan ni mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, ina wajibu wa kutekeleza makubaliano yaliyounda mahakama hiyo. Shirika hilo la haki za binadamu limedai pia kuwa, kama Jordan itamruhusu Rais al Bashir kutembelea nchi hiyo au kama haitomtia mbaroni, itakuwa imekwenda kinyume na ahadi zake kwa mujibu wa makubaliano ya ICC. 
Mahakama ya ICC inadai kuwa Rais Omar al Bashir wa Sudan amehusika katika jinai za kivita katika jimbo la Darfur na imetoa waranti wa kutiwa mbaroni.
Kikao cha wakuu wa Jumuia ya Nchi za Kiarabu kimepangwa kufanyika Jumatano ya tarehe 29 mwezi huu wa Machi nchini Jordan. Rais Omar al Bashir amealikwa kushiriki kwenye kikao hicho.
Jimbo la Darfur la magharibi mwa Sudan lilikumbwa na machafuko tangu mwaka 2003 kulalamikia kudharauliwa na kutelekezwa na serikali.

IRAN YATAKA MAREKANI ISHTAKIWE KWA JINAI ZA KIVITA BAADA YA MAUAJI YA MOSUL

Afisa wa ngazi za juu nchini Iran amesema kuwa, hujuma za ndege za kivita za Marekani katika mji wa Mosul, Iraq ambazo zimeua idadi kubwa ya raia, ni jinai za kivita.
Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema, jinai iliyofanywa na Marekani huko Mosul ni sawa na jinai za kivita zinazofanywa na magaidi wa Daesh (ISIS) pamoja na makundi mengine ya magaidi wakufurishaji ambao wanawalenga raia na watu wasio na hatia. Amesema jinai hizo za Marekani zinapaswa kushughulikiwa haraka iwezekanavyo katika mahakama ya kimataifa.
Siku ya Jumamosi Marekani ilikiri ilifanya mashambulizi ya angani huko magharibi mwa Mosul mnamo Machi 17 mwaka huu na kuua raia 200. Wakuu wa Iraq wanasema Mareknai ilifanya hujuma kadhaa siku hiyo.
Maeneo ya raia yaliyohujumiwa na Marekani huko Mosul, Iraq
Shamkhani amesema, hata kama Marekani inadai eti hujuma hiyo haikuwa ya makusudi, lakini hilo haliwaondoi hatiani Wamarekani waliotenda jinai hiyo. Shamkhani amesema, jeshi la Marekani limekuwa likiua raia wasio na hatia katika eneo hili kwa kisingizo cha kupambana na ugaidi.
Umoja wa Mataifa pia umetangaza kushtushwa na kupoteza maisha raia katika shambulio hilo la Marekani mjini Mosul, kaskazini mwa Iraq.

IGAD; WAKIMBIZI WAHIFADHIWE KWA MUJIBU WA SHERIA ZA KIMATAIFA

mediaWaziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam DesalegnPhoto: Reuters/Tiksa Negeri
Mkutano wa IGAD umefunguliwa rasmi jumamosi jijini Narobi ambapo wito umetolewa na viongozi wa nchi wanachama wa shirika hilo kufanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa wakimbizi wanapewa hifadhi bila kujali nchi wanazotoka.
Waziri mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dusalegn alisisitiza wanachama kuwa wakimbizi lazima wahifadhiwe kwa vyovyote vile Kulingana na sheria za kulinda wakimbizi za kimataifa.
Hadi sasa raia wa Somalia wapatao Milioni mbili wameyakimbia makwao huku wengi wakiishi nchini Kenya, Ethiopia na nchini Uganda.
Umoja wa Mataifa umekuwa ukitoa wito kwa nchi za hasa Kenya kuendelea kuwapa hifadhi wakimbizi wa Somalia.

WANAJESHI KADHAA WA MISRI WAUAWA KATIKA MRIPUKO WA BOMU SINAI

Wanajeshi wanne wa Misri wameuawa baada ya gari lao kulengwa kwa bomu katika Peninsula ya Sinai.
Duru za kijeshi zimearifu kuwa, mlipuko huo ulitokea yapata kilomita 20, kusini mwa mji wa al-Arish, kaskazini mwa eneo la Sinai.
Habari zaidi zinasema kuwa, watu kadhaa wamejeruhiwa katika shambulizi hilo la bomu, linaloaminika kufanywa na magenge ya kigaidi yanayofungamana na kundi la kitakfiri la Daesh.
Vikosi vya Misri eneo la Sinai
Shambulizi hilo la jana limefanyika siku mbili baada ya hujuma nyingine kama hiyo ya bomu kuua askari 10 wa jeshi la Misri katikati mwa Peninsula ya Sinai. Hata hivyo, vyombo vya usalama vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika vilifanikiwa kuangamiza magaidi 15 katika operesheni hiyo, mbali ya kuwatia mbaroni wengine 7. 
Eneo la Sinai Kaskazini limekuwa likishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi la Ansar Baytul Muqaddas, tawi la genge la kigaidi la Daesh nchini Misri, hujuma zilizoshadidi baada ya kundi hilo kutangaza utiifu kwa kundi la kigaidi la Daesh mwaka 2014.

MAANDAMANO SANA'A KULAANI VITA VYA SAUDIA DHIDI YA YEMEN

Mamilioni ya wananchi wa Yemen wameandamana leo katika mji mkuu Sana'a na maeneo mengine nchini humo katika mwanzo wa mwaka wa tatu tokea Saudia ianzishe vita vyake vya kinyama dhidi ya nchi hiyo ambavyo vimesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na wengine wengi kupoteza makazi yao.
Katika maandamano hayo yaliyofanyika leo Jumapili katika Medani ya Al Sabin mjini Sana'a, Wayemen walikuwa wamebeba bendera za nchi yao huku wakitoa nara dhidi ya umwagaji damu unaofanywa na Saudia nchini humo kwa muda wa miaka miwili.
Akizungumza katika maandamano hayo, Saleh al Samad, Rais wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amewapongeza Wayemen kwa kusimama kidete kupambana na wavamizi wa Aal Saud. Amesema Saudi Arabia imeshindwa kufikia malengo yake nchini Yemen pamoja na kuwa imetumia kiasi kikubwa cha fedha na silaha za kisasa.
Lengo kuu la mashambuliai ya Saudia dhidi ya Yemen ni kumrejesha madarakani kibaraka wake, Rais wa zamani wa nchi hiyio aliyejiuzulu na kutoroka nchi Abdu Rabuh Mansour Hadi. Lengo jingine ni kutaka kuwaondoa madarakani wanamapinduzi wa Ansarullah.
Uharibifu wa Saudia katika makazi ya raia nchini Yemen
Tangu ulipoanzisha uvamizi wake wa kijeshi dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka 2015 hadi sasa, muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na utawala wa Aal Saud na kuungwa mkono na Marekani na Israel umeshaua zaidi ya watu 12,000 katika mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu. Kwa mujibu wa televisheni ya Al Masira, kati ya waliopoteza maisha katika hujuma ya Saudia ni watoto 2,646 na wanawake 1,922.
Aidha  muungano huo vamizi umeshazishambulia skuli, hospitali, makaazi ya raia, barabara, masoko na kambi za wakimbizi na kuua maelfu ya raia wasio na hatia wa Yemen. Ndege za kivita za Saudia aidha zimebomoa nyumba za raia zipatazo 403,039 na misikiti 712.

WENGI WAJITOKEZA KATIKA UCHAGUZI WA SAARLAND UJERUMANI KULIKO 2012

Idadi ya Wajerumani waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa jimbo dogo la magharibi la Saarland ni juu kidogo kuliko idadi ya waliojitokeza katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2012. Hadi kufikia saa nane mchana wa leo takriban asilimia 32.6 ya wapiga kura walishapiga kura zao, tofauti na uchaguzi uliopita ambapo wakati sawa na huo, ni asilimia 31.1 ya wapiga kura ndio walikuwa wamejitokeza. Ongezeko la asilimia hiyo ndogo inatizamwa kuwa ishara za awali ya jinsi hali itakavyokuwa katika uchaguzi mkuu wa Ujerumani mwezi Septemba. Uchaguzi huo unaojiri miezi sita kabla ya uchaguzi mkuu mwezi Septemba, unatizamwa kama kipimo kinachoweza kubaini ushawishi wa Kansela Angela Merkel dhidi ya washindani wake wa siasa za wastani za mrengo wa kushoto. Uchaguzi huo ni wa kwanza miongoni mwa chaguzi tatu za majimbo zitakazofanyika kabla ya uchaguzi mkuu. Kadhalika ndio uchaguzi wa kwanza tangu Martin Schulz kuidhinishwa na chama chake cha SPD kugombea ukansela dhidi ya Merkel.

MAGAIDI WATANO WAUAWA , 16 WATIWA MBARONI KASKAZINI MWA MISRI

Wanajeshi wa Misri katika operesheni ya kupambana na mgaidi, Sinai Kaskazini
Jeshi la Misri leo limetoa taarifa na kusema kuwa, limefanikiwa kuua magaidi watano na kuwatia mbaroni wengine 16 katika operesheni maalumu iliyofanywa na jeshi hilo kaskazini mwa Misri.
Msemaji wa jeshi la Misri, Kanali Tamer el  Refae amesema, magaidi watano wakufurishaji akiwem mmoja wa viongozi wa kundi la kigaidi Baytul Muqaddas linalofanya mashambulizi yake mengi kaskazini mwa Rasi ya Sinai wameuawa kwenye operesheni hiyo. Amesema, magaidi wengine 16 wametiwa mbaroni katika opereseheni hiyo.
Kwa mujibu wa Kanali Tamer el Refae, jeshi la Misri limekamata pia kiwango kikubwa cha silaha pamoja na kutegua mabomu yaliyokuwa yametegwa na wanamgambo hao.
Magaidi wa Daesh wakijiandaa kushambulia makazi ya raia kwa roketi wanaloliita "Jahannam"

Eneo la Sinai Kaskazini huko Misri limeshuhudia mashambulizi mengi ya kigaidi tangu mwaka 2013 baada ya jeshi la nchi hiyo kufanya mapinduzi yaliyoongozwa na Rais wa hivi sasa wa Misri, Jenerali Abdul Fattah el Sisi. Mapinduzi hayo ya kijeshi yalimuondoa marakani rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri, Mohammad Morsi ambaye hivi sasa yuko jela. Al Arish ambayo ndiyo makao makuu ya mkoa huo wa kaskazini mwa Misri ndio mji unaoshuhudia mashambulizi mengi ya kigaidi.
Hadi hivi sasa kundi la Ansar Baytul Muqaddas limeshafanya makumi ya mashambulizi dhidi ya maeneo ya wanajeshi na raia wa kawaida wa Misri na kuua watu wengi sambamba na kuharibu miundombinu ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.