Sunday, May 27, 2018

WATU 30 WAUAWA KATIKA MAPIGANO MASHARIKI MWA KONGO DR

Watu 30 wameuawa katika mapigano kati ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wanamgambo wa Mai-Mai mashariki mwa nchi hiyo.
Duru za eneo hilo zimeripoti kuwa katika mapigano hayo yaliyotokea jana na kuendelea kwa saa kadhaa wanajeshi 18 waliuawa akiwemo afisa mmoja na kamanda wa polisi wa polisi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa duru hizo, wanamgambo wanane waliohusika katika hujuma hiyo pamoja na raia watatu pia waliuawa katika mapigano hayo. Raia hao waliuliwa kwa risasi walipokuwa wakikimbia mapigano.


Mnamo siku ya Alkhamisi iliyopita, wanamgambo wa kundi la Mai-Mai walilidhibiti eneo lenye utajiri wa madini la Salamambila mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, lakini wakalazimika kuliacha na kukimbia baada ya vikosi vya jeshi la serikali kufika katika eneo hilo.
Wanamgambo wa Mai-Mai wanatokana na makundi ya wabeba silaha waliopata mafunzo ya kijeshi katika eneo la mashariki mwa Kongo DR ambalo limekuwa uwanja wa mapigano kwa zaidi ya miaka 20 sasa.../

RAIS ROUHSNI: HATUA ZILIZOCHUKULIWA HADI SASA NI CHANYA KWA AJILI YA KUENDELEZA JCPOA

Rais Hassan Rouhani amesema, baada ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya JCPOA waliowengi katika jamii ya kimataifa wameipa haki Iran na kuyatetea makubaliano hayo na kuongeza kwamba hatua zilizochukuliwa hadi sasa ni nzuri kwa ajili ya kuendeleza makubaliano hayo ya nyuklia.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyaeleza hayo mbele ya hadhara ya maulamaa na wanazuoni wa mjini Tehran na kubainisha kuwa: Leo akthari ya nchi zinaitakidi kuwa njia iliyofuata Iran ilikuwa sahihi na Marekani ndio iliyofanya makosa, na hayo ni mafanikio makubwa.
Rais Rouhani amefafanua kuwa Marekani inatoa mashinikizo kwa nchi za Ulaya kwamba zichague kati ya Marekani na Iran lakini nchi hizo zinasema 'sisi tunachagua makubaliano ya JCPOA'.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa msingi inaofungamana nao Iran ni kwamba kama itaweza kupata haki zake kwa kubaki kwenye makubaliano ya JCPOA itaendelea kufungamana na makubaliano hayo ya kimataifa.
Rais Hassan akihutubia hadhara ya maulamaa
Ikumbukwe kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza Mei 8 kuwa nchi yake imejiondoa katika mapatano hayo ya nyuklia ya Iran ambayo rasmi yanajulikana kama JCPOA. Trump aidha alisema ataiwekea Jamhuri ya Kiislamu vikwazo vya nyuklia katika kipindi cha miezi mitatu hadi sita ijayo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza kusikitishwa mno na uamuzi huo wa upande mmoja uliochukuliwa na rais wa Marekani.
Hii ni katika hali ambayo nchi zilizosalia katika JCPOA, yaani Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Ujerumani na Umoja wa Ulaya, zimesisitiza kuwa zitandelea kuunga mkono mapatano hayo.
Wakati huohuo katika siku za karibuni Iran na nchi za Ulaya zimefanya mazungumzo kadhaa kwa lengo la kuyaendeleza makubaliano ya JCPOA baada ya Washington kujiondoa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa.
Inafaa kukumbusha pia kuwa mnamo siku ya Jumatano iliyopita Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei alibainisha masharti ya Iran kuendelea kubakia katika JCPOA na kusisitiza kuwa: "Nchi za Ulaya zinapaswa kuwasilisha azimio dhidi ya Marekani katika Baraza la Usalama, ziahidi pia kuwa kadhia za makombora na ushawishi wa Iran katika eneo hazitajadiliwa na pia zikabiliane na vikwazo vyovyote vya Marekani dhidi ya Iran." Aidha Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa nchi za Ulaya zinapaswa kutoa dhamana ya kununua mafuta ya Iran kwa kiwango ambacho Iran inahitaji na pia benki za Ulaya zinapaswa kutoa dhamana ya kutekeleza malipo ya kifedha kwa ajili ya biashara na serikali pamoja na sekta binafsi ya  Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.../

BAYTU ZAKAT YA KUWAIT YAZINDUA PROGRAMU YA DOLA 26400 KWA AJILI YA KUFUTURISHA KATIKA MWEZI WA RAMADHAN NCHINI TANZANIA


 Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Mhe. Jasem Al-Najem anashiriki katika utekelezaji wa programu ya kufuturisha ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambayo inafadhiliwa na Chombo cha Baytu Zakat, Wakfu na Mali ya Amana ya Kuwait. Programu kama hii huandaliwa kila mwaka kutoka kwa wasamaria wa nchi ya Kuwait.  
Programu hii thamani yake ni dola elfu 26 na mia nne sawa na shilingi milioni 60.
Awamu ya kwanza ya programu hii ilikuwa ni kugawa vikapu 400 vyenye vyakula kama mchele, sukari,unga,mafuta ya kula, tende na sukari ambapo katika moja ya zoezi la ugawaji alihudhuria Mkuu wa Wilaya ya Ilala. Bi Sophia Mjema.
Ubalozi wa Kuwait umedhamiria mwaka huu kuwasilisha misaada ya futari katika miji, vitongoji, kata, mitaa, vijiji na maeneo ya mbali kote Tanzania ambapo hadi sasa mikoa ya Tanga, Iringa, Dar es salaam na visiwa vya Zanzibar imefaidika na misaada hiyo ambayo Ubalozi hushirikiana na asasi zisizokuwa za kiserikali za Tanzania katika kuwafikia walengwa.







Monday, May 21, 2018

KIMBUNGA CHA KITROPIKI CHAIKUMBA SOMALILAND; WATU WASIOPUNGUA 15B WAAGA DUNIA

Watu wasiopungua 15 wameaga dunia huko Somaliland baada ya mvua kubwa zilizosababishwa na kimbunga cha kitropiki kwa jina la Sagar kuiathiri nchi hiyo ya Pembe ya Afrika mwishoni mwa wiki.
Somaliland ilijitenga  na Somalia mwaka 1991. Abdirahman Ahmed Ali Gavana wa eneo la Awdal amesema kuwa mvua kubwa zilizonyesha katika muda wa masaa 24 yaliyopita zimeua watu 16 katika wilaya za Lughaya na Baki. Serikali ya Somaliland tayari imeanza kutoa misaada ya dharura kwa wahanga wa kimbunga hicho. Wakati huo huo upepo mkali uliosababishwa na kimbunga cha Sagar umewasomba wanaume wawili pamoja na gari yao huko katika mji wa Bosaso katika eneo la Puntland, huko kaskazini mashariki mwa Somalia. Hayo yameelezwa na Yusuf Mohamed Waeys Gavana wa Bari katika eneo la Puntland.
Wakati huo huo Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayohusika na Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu imesema kuwa maelfu ya watu wameathirika na mafuriko hayo, wamepoteza makazi na miundo mbinu kuharibiwa huko Puntland.   
Kimbunga cha kitropiki cha Sagar kilivyoiathiri Somaliland

Saturday, May 19, 2018

WATUWATATU TU WAMENUSURIKA KATIKA AJALI YA NDEGE ILIYOKUWA IMEBEBA WATU 110 NCHINI CUBA

Watu watatu tu wameripotiwa kunusurika katika ajali ya ndege iliyochakaa aina ya Boeing 737 ambayo ilianguka hapo jana muda mfupi baada ya kuruka katika uwanja wa ndege wa Havana nchini Cuba huku wachunguzi wakijaribu kubaini chanzo cha ajali hiyo kupitia mabaki ya ndege hiyo.
Kwa mujibu wa televisheni ya taifa ya Cuba hali ya hewa ilikuwa ya mawingu na mvua ilikuwa inanyesha wakati ndege hiyo ambayo imeshatumika kwa muda wa miaka 39 ilipoanguka ikiwa katika safari za ndani kuelekea mji wa Holguin mashariki mwa nchi hiyo.
Rais Miguel Diaz-Canel wa Cuba amesema tume maalumu imeundwa kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.
Rais Miguel Diaz-Canel wa Cuba (katikati ya askari na raia) alipokagua tukio la ajali
Ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria 104, akthari yao wakiwa ni Wacuba pamoja na wahudumu sita.
Abiria wanne walionusurika walipelekwa hospitali ya Havana, ambapo hadi kufikia jana usiku watatu miongoni mwao walikuwa wangali hai.
Ajali hiyo ya jana ya ndege imetajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini Cuba katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita na ya tatu kwa ukubwa kutokea duniani tangu mwaka 2010.../

RAIS RTUMP WA MAREKANI AWATUSI TENA WAHIJIRI KWA KUWAITA KUWA NI WANYAMA

Rais Donald Trump wa Marekani kwa mara nyingine ametoa matamshi mabaya yenye kuwavunjia heshima wahajiri au wahamiaji nchini humo kwa kuwataja kuwa ni wanyama.
Matamshi hayo ya Trump si ya kwanza ya aina yake kwani miezi kadhaa iliyopita katika kikao chake na wajumbe wa vyama vya Democrat na Republican katika Ikulu ya White House aliashiria kuhusu wahajiri kutoka Haiti, El Salvador na baadhi ya nchi za Afrika na kuzitaja kuwa sawa na shimo la kinyesi.
Matamshi hayo ya mara kwa mara ya Trump ya kuwavunjia heshima wahamiaji hasa wenye asili ya Afrika yamekosolewa na wajumbe wa chama cha upinzani cha Democrat ambao wanasema ni ishara ya wazi kuwa mtawala huyo ni mbaguzi wa rangi.
Ikulu ya White House ilijaribiu kuonyuesha kuwa matamshi hayo yalitokana na hisia za kitaifa za rais huyo, lakini baada ya kuendelea malalamikio kuhusu matamshi hayo ya kishenzi ya Trump, rais huyo akiwa katika mkutano na Katibu Mkuu wa Shirika la Kijeshi la Nato, katika kujaribu kutetea matusi yake kuhusu wahajiri wanaoingia nchini humo kinyume cha sheria, amesema wakati alipowahutubu kwa kuwaita kuwa ni 'Wanyama' siku ya Jumatano, alikusudia genge la wahalifu linalojulikana kama  'MS 13'.
Matamshi hayo ya Trump kuhusu wahajiri ambayo aliyatoa wakati wa mkutano wake na wakuu wa jimbo la California, yamekosolewa vikali na wajumbe wa Bunge la Kongresi.
Mtu mwenye asili ya Afrika akikandamizwa nchini Marekani
Aghalabu ya wajumbe wa Kongresi wanaamini kuwa matamshi hayo yasiyokubalika hata kidogo ya Trump, yanaonyesha wazi kuwa hawajibiki na ni mchochezi.
Matamshi hayo ya Trump ya kuwavunjia heshima na kuwadhalilisha wahajiri yameandamana na hatua za kivitendo za kuwatenganisha watoto wahajiri na wazazi wao.
Hali kadhalika Trump amewawekea Waislamu vizingiti kuingia Marekani sambamba na hatua zingine nyingi za kibaguzi. Hatua hizo za Trump zinalenga kuwashinikiza wahajiri na wahamiaji ili kuwazuia wasiingie Marekani.
Matamshi ya kibaguzi ya rais wa Marekani ni chanzo cha wasiwasi na hofu katika jamii ya Marekani hasa miongoni mwa wasomi nchini humo ambao wanaamini kuwa matamshi hayo yasiyofaa hata kidogo yataharibu itibari iliyobakia ya nchi hiyo duniani.
Rupert Colville, Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa anasema matamshi ya Trump ni ya kushtua na ya kuaibisha.
Ikulu ya White House na hata Donald Trump mwenyewe wamejaribu kukanusha matamshi hayo ya kibaguzi, lakini ukweli usioweza kupingika ni huu kuwa, ubaguzi wa rangi ni sehemu ya utambulisho wa wazi wa utawala wa Rais Trump na Ikulu ya White House.