Mshauri mkuu wa rais Donald Trump amejiuzulu baada ya
kukabiliwa na kushfa ya udanganyifu, kuhusiana na mazungumzo
aliyoyafanya na balozi wa Urusi. Ikulu ya White House imekwishatangaza
atakayekaimu katika nafasi hiyo.
Michael Flynn, mshauri mkuu wa Rais Trump kuhusu masuala ya usalama ambaye amejuzulu
Mshauri huyo, Michael Flynn hapo awali alikuwa amekanusha kuhusisha
suala la vikwazo dhidi ya Urusi, katika mazungumzo na balozi wa Urusi
nchini Marekani Sergei Kislyak, wakati ambapo alikuwa hajaanza rasmi
majukumu yake.
Hili linachukuliwa kama pigo kubwa kwa utawala wa
Donald Trump ambao haujadumu hata kwa kipindi cha mwezi mmoja. Kwa siku
kadhaa uvumi umekuwa ukienea, kwamba Flynn ambaye ni Jenerali mstaafu,
alimdanganya Makamu Rais Mike Pence, ambaye alijitokeza hadharani
kumtetea.
Katika barua yake ya kujiuzulu, Flynn amesema ''bila
kukusudia'' alimpa Makamu Rais ''taarifa ambazo sio kamilifu'' kuhusu
mazungumzo yake ya simu na balozi Kislyak wa Urusi.
Ikulu ya
White House mjini Washington imesema imemteuwa Luteni Jenerali Joseph
Kellogg ambaye amekuwa mwenyekiti wa baraza la majenerali, kukaimu
katika nafasi iliyoachwa wazi na Michael Flynn. Vyombo vya habari nchini
Marekani viliripoti jana Jumatatu, kwamba utawala wa Donald Trump
ulikwishatahadharishwa mapema mwaka huu kuhusu mahusiano kati ya Michael
Flynn na Urusi.
Mwanzo wa maswali magumu
Maswali
sasa yanaanza kuulizwa kuhusu watu katika utawala wa Marekani ambao
walijua kuwepo kwa mazungumzo hayo, na kwa nini Rais Trump hakuchukua
hatu mapema kumvua Flynn majukumu yake.
Msemaji wa Ikulu ya Washington amesema Rais Trump hakujua chochote kuhusu udanganyifu wa Michael Flynn
Kabla
ya Michael Flynn kuwasilisha barua yake ya kujiuzulu, msemaji wa Ikulu
ya White House Sean Spencer alisisitiza kuwa Rais Trump hakufahamishwa
chochote kuhusU mazungumzo kati ya Michael Flynn na balozi wa Urusi
kuhusu vikwazo ilivyowekewa nchi hiyo.
Yeyote atakayechukua
nafasi ya Flynn ataliongoza Baraza la Usalama wa Taifa mnamo wakati
utawala mchanga wa Rais Trump ukikabiliana na changamoto kubwa, likiwemo
jaribio la hivi karibuni la makombora ya kivita lililofanywa na Korea
Kaskazini.
Vile vile utawala wa Trump unaogelea katika dimbwi la
msukosuko uliotokana na amri ya rais huyo kuwapiga marufuku kuingia
Marekani, watu wote kutoka mataifa saba yenye waislamu wengi, amri
ambayo hivi sasa imesimamishwa na mahakama.
Michael Flynn ambaye
alikuwa muungaji mkubwa wa Donald Trump tangu hatua za awali za kampeni
yake, amekuwa akihimiza msimamo mkali dhidi ya Iran na kulegeza sera
dhidi ya Urusi, mtazamo ambao ni kunyume kabisa na ule wa utawala
uliotangulia wa Rais Barack Obama.
No comments:
Post a Comment