Thursday, February 9, 2017

MAHAKAMA KUU YA KENYA YABATILISHA UAMUZI WA KUIFUNGA KAMBI YA WAKIMBIZI YA DADAAB

Mahakama Kuu ya Kenya imebatilisha mpango uliotangazwa na serikali ya nchi hiyo wa kuifunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab.
Akitoa hukumu hiyo leo, Jaji John Mativo amesema Waziri wa Usalama wa Ndani Joseph Nkaissery na Katibu wake Mkuu Karanja Kibicho walichukua hatua nje ya mamlaka yao kwa kuagiza kambi hiyo kubwa zaidi ya wakimbizi duniani ifungwe.
Mahakama hiyo aidha imetangaza kuwa uamuzi wa kuwahamisha wakimbizi umekiuka Katiba na ni wa kibaguzi.
Mahakama Kuu ya Kenya imetoa hukumu hiyo kufuatia shauri la madai lililowasilishwa na Kamisheni ya Taifa ya Haki za Binadamu ya nchi hiyo (KNCHR) na asasi ya Kituo cha Sheria.
Jaji Mativo ameiagiza serikali ya Kenya iandae utaratibu utakaohakikisha uhamishaji wa wakimbizi unafanyika kwa njia sahihi na mwafaka.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama Kuu, notisi zilizochapishwa kwenye gazeti kuu la serikali za kutangaza uhamishaji wa wakimbizi zimeelezwa pia kuwa ni batili na zisizo na itibari.
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya Joseph Nkaissery
Mwezi Mei mwaka uliopita wa 2006, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya Joseph Nkaissery, alitangaza kuwa ifikapo mwezi Novemba, serikali itaifunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab kutokana na sababu za kiusalama, kimazingira na kiuchumi pamoja na kuwatuhumu wafadhili wa kimataifa kuwa hawachukui hatua za kutosha kuwasaidia wakimbizi hao.
Uamuzi huo ulilaaniwa na kukosolewa vikali na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) pamoja na mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch na Amnesty International.
Wakati huohuo, masaa machache baada ya kutangazwa uamuzi huo wa Mahakama Kuu hii leo, serikali ya Kenya kupitia msemaji wake Eric Keraithe imetangaza kuwa sambamba na serikali hiyo ya muungano tawala wa Jubilee kuheshimu sharia itakata rufaa kupinga hukumu hiyo…/

No comments:

Post a Comment