Muungano na misimamo ya aina moja dhidi ya
Iran ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Waziri wa Vita wa
utawala ghasibu wa Israel na mwenzao wa Uturuki katika Mkutano wa
Usalama wa Munich si jambo jipya wala lililotokea kwa sadfa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu matamshi
yaliyotolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Adel
al-Jubeir na bwabwaja za Waziri wa Vita wa Israel kwa kusema kwamba,
tawala hizo mbili zinadhani kuwa ili kuweza kufidia kufeli na kushindwa
kwao mara kwa mara katika Mashariki ya Kati zinapaswa kuchochea anga ya
kimataifa dhidi ya Iran. Bahram Qasemi ameongeza kuwa, lugha iliyotumiwa
na mawaziri hao wawili pia ni ya kukaririwa na inayoakisi kufilisika
na kukata tamaa kunakoambatana na machungu na maumivu.
Katika hotuba yake kwenye Mkutano wa Usalama wa Munich, Waziri wa
Mambo ya Nje wa Saudi Arabia amesema kuwa: Eneo la Mashariki ya Kati
limejaa mivutano. Migogoro ya Syria, Iraq, Yemen na Libya inazidi
kupambana moto, tunakabiliwa na ugaidi, uharamia na matatizo ya
kiuchumi... Tunapaswa kufanya jitihada za kupatanisha kati ya Waarabu na
Israel..", mwisho wa kunukuu.
Matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia katika upande
mmoja yanaakisi sehemu ya hali halisi ya Mashariki ya Kati. Hata hivyo
kuna shaka kubwa kuhusu alichodai kuwa ni sababu za kujitokeza
changamoto hizo. Katika matamshi yake hayo Adel al-Jubeir amefanya
jitihada kubwa za kuituhumu Iran kuwa inaunga mkono ugaidi na kusema,
Tehran inaingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. Matamshi hayo kwa
hakika ni aina fulani ya kubadili na kugeuza ukweli na hali halisi ya
mambo. Vilevile kunaonekana ushirikiano mkubwa na mfanano wa aina yake
katika matamshi hayo na yale yaliyotolewa na maafisa wa serikali ya
Israel katika Mkutano wa Usalama wa Munich.
Katika hotuba yake kwenye mkutano huo, Waziri wa Vita wa Israel,
Avigdor Lieberman ameituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa inavuruga
amani na usalama wa eneo la magharibi mwa Asia na kudai kuwa: Iran ndiyo
nchi inayoongoza katika kuunga mkono ugaidi duniani. Avigdor Lieberman
amedai kuwa, maudhui ya Palestina si tatizo muhimu la eneo la magharibi
mwa Asia kwa sasa. Matamshi kama haya haya pia yametolewa na Waziri wa
Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlüt Çavuşoğlu katika mkutano wa Munich.
Jumla ya misimamo hiyo kwa hakika ni mithili ya vipande vya fumbo na
chemsha bongo ambayo picha yake ya mwisho ni kudhihirisha sura ya
kutisha kuhusu Iran. Hata hivyo na licha ya mshabaha unaoshuhudiwa
katika matamshi na misimamo hiyo ya Saudi Arabia, Israel na Uturuki
lakini kila mmoja wao anafuatilia malengo yake makhsusi.
Marekani
kwa upande wake inafuatilia malengo ya kuzusha hofu na wahka kwa nchi za
Kiarabu ili kuweza kuuza silaha zaidi kwa nchi hizo na kuyaingizia
faida kubwa makampuni ya kuuza silaha ya nchi hiyo.
Lengo kuu la utawala haramu wa Israel katika mchezo huo mchafu ni
kufuta kabisa kadhia ya Palestina. Hivyo basi kauli ya Waziri wa Mambo
ya Nje wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir aliyedai kuwa maudhui kuu ya eneo
la Mashariki ya Kati kwa sasa ni kujenga suluhu na mapatano baina ya
Waarabu na Israel, yanaonekana kuhudumia ipasavyo malengo ya utawala huo
ghasibu unaoendelea kuukalia kwa mabavu Msikiti wa al Aqsa na kibla cha
kwanza cha Waislamu.
Hapa
bado haijajulikana vyema nafasi ya Uturuki katika kundi hili lenye
pande tatu. Inaoneka kuwa, Uturuki imenasa katika nafasi kadhaa na
kukosa msimamo thabiti na wa wazi. Katika upande mmoja, Ankara inataka
kuwa na nafasi katika matukio ya Syria, siku moja inalisaidia na
kulihami kundi la kigaidi la Daesh na kesho yake inafanya mashambulizi
dhidi ya kundi hilo na kuwatia nguvuni raia wa Uturuki kwa madai ya
kuunga mkono na kushirikiana na kundi hilo!
Katika
hatua yake nyingine Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan amezitembelea
nchi kadhaa za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi ambako ametangaza uungaji
mkono wa nchi yake kwa nchi hizo na wakati huo huo Waziri wake wa Mambo
ya Nje amehutubia Mkutano wa Usalama wa Minich na kuituhumu Iran kuwa
inaunga mkono ugaidi na kuchochea mapigano ya kimadhehebu!
Madai haya yametolewa wakati hakuna asiyejua kwamba, Uturuki na Saudi
Arabia ni miongoni mwa vinara waliokuwa mstari wa mbele katika
kuanzisha mgogoro wa sasa wa eneo la Mashariki ya Kati. Kwa mfano tu
Uturuki imetuma kinyume cha sheria majeshi yake katika ardhi ya nchi za
Iraq na Syria na kukiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi hizo. Nchi hiyo
hiyo siku chache zilizopita ilitia saini taarifa ya pande tatu na Iran
na Russia ambayo imesisitiza suala la kuheshimiwa ardhi ya Syria.
Alaa kulli hal, pande hizo tatu (Saudia, Israel na Uturuki) na
washirika wao zinaelewa vyema kwamba, Iran haikubaliani na mchezo huo
mchafu na wa kinafiki; kwa sababu hiyo zimeungana na kupiga ngoma za
propaganda dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Hata hivyo walimwengu wamekomaa
na wanaelewa vyema ni kina nani walioanzisha makundi ya kigaidi kama
Daesh na Jabhatu Nusra, kuyapa silaha, kuyaruhusu kutumia ardhi na
mipaka yao kuingia Syria na Iraq na hatimaye kujitokeza hali
inayoshuhudiwa sasa katika eneo la Mashariki ya Kati na kwengineko
duniani.
No comments:
Post a Comment