Sunday, December 31, 2017

KOREA KASKAZINI YAAPA KUIMARISHA ZANA ZAKE ZA NYUKLIA MWAKA 2018

Korea Kaskazini yaapa kuimarisha zana zake za nyuklia mwaka 2018
Korea Kaskazini imeapa kufanyia majaribio zaidi ya zana zake za nyuklia mwaka 2018 huku ikisisitiza kuwa uwezo wake hauwezi kuangamizwa au kuvurugwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa kupitia shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini KCNA, wakuu wa Korea Kaskazini wameilamu Marekani kwa kuendeleza njama dhidi yake katika sekta za kiuchumi, kisiasa, kijeshi na kidiplomasia katika mwaka huu unaomalizika wa 2017. Taarifa hiyo imesema pamoja na kuwepo njama hizo za Marekani Korea Kaskazini haikusita katika mkondo wake na ina yakini ya kupata ushindi.
Aidha Korea Kaskazini imesema itazidi kuimarisha uwezo wake wa kujihami ili kukabiliana na vitisho vya nyuklia vya Marekani. Wakuu wa Pyongyang pia wameilaumu vikali Marekani kwa kuendeleza uchochezi kupitia vitisho vya nyuklia na mazoezi ya kijeshi katika mipaka yake.
Rais Donald Trump wa Marekani na Kiongozi wa Korea Kaskazini  Kim Jong-u
Septemba mwaka huu, Korea Kaskazini ilifanyia majaribio kwa mafanikio bomu la nyuklia, hilo likiwa ni jaribio la sita la aina hii kufanywa na nchi hiyo.
Marekani, ambayo ni mchochezi mkuu wa mivutano kwenye eneo la Peninsula ya Korea imekuwa kila mara ikishikilia Korea Kaskazini isimamishe majaribio yake ya nyuklia, lakini viongozi wa Pyongyang wanasisitiza kwamba madamu Marekani na waitifaki wake wanaendelea kutoa vitisho dhidi ya Korea Kaskazini, nchi hiyo nayo itaendelea kujiimarisha kijeshi.

Wednesday, December 27, 2017

JESHI LA UGANDA LAUA WAASI ZAIDI YA 100 WA ADF KONGO DR

Jeshi la Uganda laua waasi zaidi ya 100 wa ADF Kongo DR
Jeshi la Uganda limetangaza habari ya kuua wanachama wasiopungua 100 wa kundi la waasi wa ADF katika makabiliano makali yaliyojiri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Taarifa iliyotolewa jana Jumatano na Jeshi la Ulinzi la Uganda UPDF imesema kuwa, vikosi vyake vimefanya mashambulizi ya angani na ardhini dhidi ya maficho ya waasi hao katika mpaka wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki na Kongo DR, na kufanikiwa kuua zaidi ya 100 miongoni mwao na kujeruhi wengine wengi.
Hujuma hii dhidi ya waasi wa ADF imefanyika siku chache baada ya Uganda na Kongo DR kukubaliana kuimarisha utaratibu wa mawasiliano na kupeana taarifa za kiintelijensia kwa ajili ya kupambana na waasi hao wanaotokea Uganda, ambao wanaendesha harakati zao mashariki mwa DRC.
Askari wa Umoja wa Mataifa DRC
Itakumbukwa kuwa, askari 14 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)  waliuawa mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba, na 44 wengine walijeruhiwa katika kambi ya Semuliki mkoani Kivu Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kufuatia hujuma ya waasi hao wa ADF.
Wanajeshi waliouawa walikuwa ni sehemu ya askari 3,000 wa timu ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa MONUSCO yenye askari kutoka Tanzania, Malawi na Afrika Kusini.

Tuesday, December 26, 2017

RAILA ODINGA : NITAAPISHWA MAPEMA MWAKA 2018 KAMA RAIS WA WATU

media
Kiongozi wa Muungano wa Upinzani Kenya, Raila Odinga.
Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya NASA, Raila Odinga amesema ataapishwa kama rais wa watu mapema mwaka 2018.
Katika ujumbe wake wa Krismasi, Odinga ameonya kuwa Kenya inaelekea kuwa taifa la Kidikteta na kuwataka wafuasi wake kuendelea kuunga mkono mikakati ya upinzani.
Serikali imeonya kuwa Odinga atafunguliwa mashtaka ya uhaini iwapo ataapishwa, onyo ambalo kiongozi huyo wa NASA amesema yuko tayari kukabiliana nalo  ikiwa ndio itakuwa njia ya kuleta haki ya kisiasa katika taifa hilo.
Iwapo Odinga, atatekeleza mipango yake, itaendeleza kuzua mvutano wa kisiasa katika taifa hilo ambalo limemaliza Uchaguzi hivi karibuni.
Marekani imetaka kuwepo kwa mazungumzo kati ya Odinga na Kenyatta, na kumhimiza kiongozi huyo wa NASA kutojiapisha kwa kile inachosema kitendo hicho kitaendelea kuzua mzozo wa kisiasa.
Kenyatta amenukuliwa mara kadhaa akisema kuwa, yuko tayari kuzungumza na Odinga lakini mazungumzo hayo yawe ni kuhusu maendeleo ya nchi huku Odinga akisema atashiriki tu kuhusu mazungumzo yatakayokuwa na ajenda ya namna ya kuwa na Uchaguzi wa urais utakaokuwa huru na haki.
Chanzo:RFI

ISRAEL INAFANYA NJAMA ZA KUDHIBITI KIKAMILIFU ENEO LA UKINGO WA MAGHARIBI

Israel inafanya njama za kudhibiti kikamilifu eneo la Ukingo wa Magharibi
Chama cha Kizayuni cha Likud kimewataka viongozi na wawakilishi wa Bunge la utawala haramu la Israel kuhudhuria kikao cha dharura cha chama kwa ajili ya kuchunguza uamuzi wa kudhibitiwa kikamilifu na utawala huo, eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina.
Televisheni namba mbili ya Israel imetangaza kwamba, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho, maamuzi yoyote yatakayochukuliwa na kikao hicho, yatatakiwa kutekelezwa na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel ambapo kwanza atatakiwa kuyawasilisha katika Bunge la utawala huo (Knesset) kwa ajili ya kupasishwa.
Rais Trump wa Marekani, anayeibebea Israel
Aidha televisheni ya Israel imetangaza kuwa, lengo la kikao hicho ni kupasisha sheria ya kuliunganisha eneo la Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel. Taarifa hiyo imedai kwamba, harakati hiyo ilianza tangu Rais Donald Trump wa Marekani alipoutangaza mji wa Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa Israel sambamba na kutaka kuanzishwa maandalizi kwa ajili ya kuhamishia ubalozi wa nchi hiyo kwenda mji huo.

NJAMA ZA SERIKALI YA NIGERIA DHIDI YA SHEIKH IBRAHIMU ZAKZAKY

Njama za serikali ya Nigeria dhidi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky
Mjumbe wa ngazi ya juu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa, serikali ya nchi hiyo inatekeleza njama za kumuua shahidi Sheikh Ibrahim Zakzaky kiongozi wa harakati hiyo.
Ibrahim Suleiman ameashiria pingamizi la kila mara la serikali ya Nigeria kuhusiana na takwa la familia ya Sheikh Zakzaky la kumpeleka nje ya nchi kiongozi huyo wa Kiislamu kwa ajili ya matibabu licha ya hali ya mwanazuoni huyo kuwa mbaya. Mwakilishi huyo wa ngazi ya juu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ameongeza kuwa upo uwezekano kuwa njama zinafanywa ili kumuua shahidi pole pole Sheikh Zakzaky. Sheikh Ibrahim Zakzaky Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria na mkewe walitiwa mbaroni katika shambulizi lililofanywa Disemba 13 mwaka juzi na wanajeshi wa Nigeria katika Husseiniya iliyopo katika mji wa Zaria jimboni Kaduna kaskazini mwa nchi hiyo. Mamia ya waumini wa Kiislamu wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Zakzaky waliuliwa shahidi katika tukio hilo.
Hassan al-Banna, mjumbe wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria sambamba na kuashiria mashtaka ya harakati hiyo dhidi ya serikali ya Nigeria katika Umoja wa Afrika amesema kuwa, licha ya kutolewa amri ya mahakama ya kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky pamoja na mkewe, lakini serikali ya Abuja imekataa katakata kutekeleza amri hiyo. Kwa muda sasa serikali imekuwa ikitekeleza siasa za chuki na adawa dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Maandamano ya kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky
Kutiwa mbaroni Sheikh Ibrahim Zakzaky na kushadidi mashinikizo dhidi ya Waislamu sambamba na kupigwa marufuku mkusanyiko wa aina yoyote ile wa Waislamu wa nchi hiyo ni miongoni mwa siasa ambazo zimekuwa zikitekelezwa na serikali ya Rais Muhammadu Buhari dhidi ya Waislamu wa Nigeria. 
Hatua hizo zinatekelezwa katika hali ambayo, hivi karibuni Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International sambamba na kutahadharisha kuhusiana na kutoweka idadi kadhaa ya Waislamu wa Nigeria, lilikosoa vikali utendaji wa serikali ya Abuja katika uwanja huo na kuitaka serikali hiyo ianzishe uchunguzi kuhusiana na kutoweka wanachama 600 wa Harakati hiyo ya Kishia.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, serikali ya Nigeria inachukua hatua hizo chini ya ushawishi wa siasa za utawala wa Saudia, Marekani na utawala dhalimu wa Israel. Ni kwa muda sasa ambapo Wazayuni baada ya siasa zao kugonga mwamba katika eneo la Mashariki ya Kati na kutengwa, sasa wameligeukia bara la Afrika na wamo mbioni kutafuta washirika wao wapya katika bara hilo. 
Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria
Katika fremu hiyo, hivi karibuni baadhi ya makamanda wa jeshi la Nigeria  walikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Saudia ni nchi nyingine ambayo imekuwa ikihaha kuhakikisha kuwa inakuwa na satuwa na ushawishi barani Afrika. 
Misaada ya siri na dhahiri ya kifedha na kijeshi ya Saudia kwa nchi za bara hilo na mkabala wake nchi hizo zisalimu amri mbele ya matakwa ya utawala wa Riyadh ni baadhi ya mikakati inayofanywa na watawala wa Aal Saud. Marekani nayo kwa kuiuzia silaha na zana za kijeshi serikali ya Nigeria imekuwa ikisaidia katika kukandamizwa Waislamu wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Katika uga huo, hivi karibuni Abdul-Rahman Abubakar Mkuu wa Kamati ya Kufuatilia Kuachiliwa Huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, sanjari na kuitumia barua serikali ya Marekani na kuashiria rekodi ambayo haijawahi kushuhudiwa ya serikali ya Nigeria kukiuka na kukandamiza haki za binadamu, ameitaka Washington iache kuiuzia silaha nchi hiyo.
Filihali kwa kuzingatia uadui wa tawala tatu za Israel, Saudia na Marekani dhidi ya harakati za kupigania uhuru za Kiislamu na ushawishi wa tawala hizo nchini Nigeria, suala la hatari ya kuuawa shahidi Sheikh Ibrahim Zakzaky na setikali ya Nigeria kufanya hilo kwa makusudi ni jambo ambalo linazidi kupata nguvu

Monday, December 25, 2017

WATU WASIOPUNGUA 15 WAUAWA KATIKA MASHAMBULIZI YA ANGA YA SAUDI HUKO SANA'A NA KATIKA MIJI MINGINE

Watu wasiopungua 15 wauawa katika mashambulizi ya anga ya Saudi huko Sana'a na katika miji mingine
Televisheni ya al Masirah imetangaza kuwa watu wasiopungua 15 wameuawa katika mashambulizi mapya ya anga ya Saudi Arabia katika maeneo mbalimbali huko Yemen, ukiwemo mji mkuu Sana'a.
Ndege za kivita za Saudi Arabia mapema leo zimeyashambulia mashamba mawili katika wilaya ya Zabid katika mkoa wa Hudaydah na kuua watu wanane wakiwemo wanawake wawili. Wanawake wengine wawili wamejeruhiwa pia katika mashambulizi hayo.
Makazi ya raia katika mkoa wa Hudayadah yaliyoshambuliwa na ndege za kivita za Saudia 
Ndege hizo za kivita za Saudia leo pia zilifanya mashambulizi kadhaa katika mji mkuu wa Yemen Sana'a na kuua raia saba na kujeruhi wengine watano. Watoto watatu na wanawake wawili ni miongoni mwa raia waliojeruhiwa huko Sana'a huku watu wengine wawili wakiwa hawajulikani walipo. Televisheni ya al Masirah imeripoti kuwa nyumba moja iliyolengwa na ndege za kivita za Saudi Arabia katika mji mkuu Sana'a imeharibiwa kikamilifu na kwamba wafanyakazi wa huduma za uokoaji waliokuwa wakiwatafuta majeruhi waliofunikwa na vifusi vya nyumba hiyo nao pia wamelengwa na ndege hizo za kivita za Saudia. Watu walioshuhudia wamesema kuwa idadi ya watu waliouawa kwenye mashambulizi hayo ya Saudia huenda ikaongezeka. 

JAMUHURI YA AL WIFAQ YALAANI HUKUMU YA KUNYONGWA ILIYOTOLEWA NA MAHAKAMA KUU YA KIJESHI YA BAHRAIN

Jumuiya ya al Wifaq yalaani hukumu ya kunyongwa iliyotolewa na mahakama kuu ya kijeshi ya Bahrain
Jumuiya ya Kiislamu ya al Wifaq ya Bahrain imelaani hukumu iliyotolewa na mahakama ya kijeshi ya nchi hiyo kwa raia wa nchi hiyo na kuitaja kuwa ni batili.
Jumuiya hiyo imesisitiza leo ikijibu hatua ya mahakama kuu ya kijeshi ya Bahrain ya kuwakatia hukumu ya kifo raia wa nchi hiyo kwamba kutishiwa kuuawa, kulazimishwa kukiri chini ya mateso kama kuadhibiwa kwa kushtushwa na umeme, kutishia kuwabaka ndugu na familia, kutekwa na kutiwa mbaroni kwa kificho kuwa ni vitendo visivyo vya kibinadamu wanavyofanyiwa raia wa Bahrain. 
Taaarifa ya Jumuiya ya Kiislamu ya al Wifaq imeongeza kuwa jamii ya kimataifa inapasa kuvunja kimya chake na kujiondoa katika kifungo cha wenzo wa mashinikizo wa mafuta na dola, na badala yake ionyeshe msimamo na ichukue hatua mkabala na maafa na jinai hizo zinazojiri huko Bahrain chini ya kivuli cha kukosekana uadilifu. 
Vikosi eti vya usalama vya Bahrain vikitawanya maandamano ya wananchi kwa gesi ya kutoa machozi  
Jumuiya ya al Wifaq imesisitiza kuwa fikra za ulipizaji kisasi haziwezi kudhibiti irada ya wananchi na kwamba vyombo vya mahakama vinawanyima wananchi wa Bahrain haki zao za msingi huku mahakama za kijeshi na vyombo vya usalama vikigeuzwa na kutumiwa kama wenzo na utawala ulioko madarakani katika kuwatesa raia wanaopinga utawala wa kidikteta na wa kifisadi wa nchi hiyo. Mahakama ya kijeshi ya Bahrain leo Jumatatu imewahukumu kunyongwa raia sita wengine wa nchi hiyo kwa tuhuma zisizo na msingi kwamba walihusika katika kupanga njama ya kumuuwa Sheikh Khalifa bin Ahmed Al Khalifah kamanda mkuu wa jeshi la nchi hiyo na vitendo vingine vya kigaidi. 

BUNGE LAIRAN LAPITISHA: QUDS NI MJI MKUU WA KUDUMU WA PALESTINA

Bunge la Iran lapitisha: Quds ni mji mkuu wa kudumu wa Palestina
Wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran leo wamepitisha mpango wa dharura wa kuunga mkono Mapinduzi ya Kiislamu ya watu wa Palestina na kusisitiza kwamba Baitul Muqaddas utakuwa mji mkuu wa kudumu wa nchi ya Palestina.
Mpango huo wa dharura umepitishwa kwa kura 187 za ndiyo, 15 za hapana huku wabunge tisa kati ya wabunge wote 233 waliohudhuria kikao hicho cha wazi cha bunge la Iran wakiamua kutopiga kura.
Mpango huo uliopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unaunganishwa kwenye Ibara nambari moja ya sheria ya kuunga mkono Mapinduzi ya Kiislamu ya watu wa Palestina.
Mpango huo utawasilishwa kwenye kamati husika ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na kuwekwa kwenye ajenda za kujadiliwa na kupitishwa rasmi na bunge hilo ndani ya muda wa masaa 48 yajayo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni muungaji mkono thabiti wa mapambano ya Wapalestina na imekuwa ikitoa wito kwa Waislamu wote duniani kuungana dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel ambao Tehran haiutambui asilani kuwa ni moja ya nchi za ulimwengu.
Rais Hassan Rouhani akishiriki kwenye maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds kuunga mkono ukombozi wa Palestina
Itakumbukwa kuwa tarehe 6 Desemba, Rais Donald Trump wa Marekani aliamsha hasira za walimwengu kwa kutangaza kuitambua Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel na kuagiza zichukuliwe hatua za maandalizi ya kuuhamishia katika mji huo ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv.
Hata hivyo siku ya Alkhamisi iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio kwa wingi mkubwa wa kura 128 za 'ndiyo' dhidi ya 9 tu za 'la' kupinga tangazo hilo la rais wa Marekani na kumtaka abadilishe uamuzi wake huo. 
Kwa mujibu wa azimio hilo, Umoja wa Mataifa hautoitambua Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.../

GUATEMALA KUHAMISHA UBALOZI WAKE KWENDA JERUSALEM

Rais wa Guatemala Jimmy Morales ameamrisha ubalozi wa nchi hiyo nchini Israel kuhamishwa kwenda Jurusalen.
Katika ujumbe kupitia Facebook, Bw. Morales alisema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kuzungumza na waziri mkuu Benjamin Netanyahu.
Wiki iliyopita Guatemala ilikuwa moja ya nchi tisa zilizopiga kura kupinga azimio la Umoja wa Mataifa la kuitaka Marekani kufuta hatua ya kuitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel.
Donald Trump alitishia kupunguza misaada kwa nchi ambazo zilipiga kura dhidi ya Marekani.
Marekani ni mtoaji muhimu wa misaada kwa Guatemala, nchi maskini ya kati kati mwa Amerika.
Siku ya Jumapili Bw. Morales alisema kuwa alikuwa ameamrisha mmlaka za nchi hiyo kufanya mikakati ya kuhamisha ubalozi kutoka Tel Aviv kwenda Jerusalem.
Hali ya mji wa Jerusalem ndio chanzo cha mzozo kati ya Israel na Palestiona.
Israel ilitwaa mji huo ambao awali ulikuwa ukikaliwa na Jordan wakati wa vita vya mwaka 1967 vya Mashariki ya Kati na inaitaja mji wote huo kuwa mji wake mkuu.
Wapalestina wanadai kuwa East Jerusalem ni mji wao mkuu taifa lake la baadaye.
Jerusalem haujatambuliwa kimataifa na nchi zote kwa sasa zina balozi zao huko Tel Aviv.


MAGAIDI WA ISIS WASHAMBULIA IDARA YA USALAMA AFGHANISTAN,

Magaidi wa ISIS washambulia Idara ya Usalama Afghanistan, Sita wauawa
Kundi la kigaidi la ISIS limedai kuhusika na hujuma ya kigaidi iliyolenga Idara ya Usalama wa Taifa ya Afghanistan katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul.
Watu wasiopungua sita wameuawa katika hujuma hiyo huku wengine wawili wakijeruhiwa baada ya gaidi aliyekuwa amejishehenesha mabomu kujiripua katika mlango mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (NDS) mjini Kabul.
Hujuma hiyo imetokea wakati wafanyakazi walipokuwa wakiwasili katika ofisi kwa ajili ya kuanza kazi. Taarifa zinasema mwanamke mmoja ni miongoni mwa waliouawa katika hujuma hiyo.
Wiki iliyopita kituo kimoja cha Idara ya Usalama wa Taifa cha Afghanistan kilishambuliwa na magaidi na katika makabiliano hayo magaidi watatu waliuawa baada ya masaa matatu ya mapigano.
Wanajeshi wa Afghanistan katika oparesheni dhidi ya magaidi
Hayo yanajiri wakati Mjumbe maalumu wa rais wa Russia nchini Afghanistan akiwa ametoa indhari kuwa wanachama zaidi ya elfu kumi wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la ISIS hivi sasa wako nchini Afghanistan na kwamba idadi yao inazidi kuongezeka kutokana na kubadilisha maskani yake kundi hilo baada ya kusambaratishwa katika nchi za Syria na Iraq.
Zamir Kabulov ametoa indhari hiyo katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la Sputnik na kuongeza kuwa Russia ina wasiwasi wa kupanuka harakati za ISIS kwenye mikoa ya kaskazini mwa Afghanistan inayopakana na Tajikistan na Turkmenistan.
Ikumbukwe kuwa hivi sasa kuna wanajeshi wapatao 11,000 wa Marekani nchini Afghanistan. Washington na washirika wake katika muungano wa kijeshi wa NATO waliivamia kijeshi nchi hiyo mwaka 2001 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi lakini si tu kuwa hawajafanikiwa bali pia ugaidi umeongezeka nchini humo.

CHINA YAZINDUA NDEGE KUBWA INAYOWEZ KUTUA NCHI KAVU NA MAJINI

China yazindua ndege kubwa zaidi inayoweza kutua nchi kavu na majini
China imezindua ndege ya "Jiaolong" AG600 ambayo ni ndege kubwa zaidi duniani inayoweza kutua nchi kavu na majini.
Ndege hiyo imeundwa kikamilifu nchini China na jana ilifanikiwa kuruka kwa majaribio. Ndege hiyo ni kwa ajili ya kukabiliana na ajali za moto misituni, na uokoaji watu majini. Inaweza kuvuta maji tani 20 ndani ya sekunde 20, na kuzima moto katika eneo la mita za mraba zaidi ya 4,000 mara moja, huku ikiweza kuwaokoa watu 50 baharini mara moja. Mbali na kuzima moto na kuwaokoa watu, pia inaweza kutumiwa katika uchunguzi na uhifadhi wa mazingira baharini.
Meli ya kivita ya China yenye uwezo wa kusheheni ndege
Ndege hiyo pia inaweza kutumika kijeshi na inatathminiwa kuwa uzinduzi wake ni katika jitiahda za China za kuimarisha uwezo wake wa kiulinzi.
Mapema mwaka huu, China ilizindua meli yake ya kwanza ya kivita yenye kusheheni ndege (aircraft carrier) iliyoundwa nchini humo.

SAUDI ARABIA ILIMDHALILISHA WAZIRI MKUU WA LEBANON, SAAD HARIRI

Saudi Arabia ilimdhalilisha Waziri Mkuu wa Lebanon, Saad Hariri
Saudi Arabia ilimdhalilisha vibaya sana Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri katika safari yake ya hivi karibuni mjini Riyadh wakati alipolazimishwa kusoma taarifa ya kujiuzulu mbele ya televisheni.
Gazeti la The New York Times limeandika Hariri alikuwa ni kama mateka na alilazimishwa kusoma barua ya kujiuzulu akiwa sehemu isiyojulikana Saudia mnamo Novemba 4 ambapo pia alitoa tuhuma zisizo na msingi kuwa eti Iran na Hizbullah zinaingilia masuala ya ndani ya eneo na hivyo amelazimika kujiuzulu.
Lakini Rais wa Lebanon Michel Aoun alishuku kuwa Hariri alijiuzulu chini ya mashinikizo na hivyo hakukubali hatua hiyo na alimtaka arejee nyumbani kutoka Saudia. Vyombo vya usalama vya Lebanon vilithibitisha kuwa Hariri  alilazimishwa kujiuzulu na hatimaye alirejea Lebanon Novemba 22 baada ya upatanishi wa Ufaransa. Hariri hatimaye alibatilisha uamuzi wake wa kujiuzulu Disemba 5.
Rais Michel Aoun wa Lebanon
Taarifa zinasema kuwa Hariri alipowasili Saudia alidhani atapokewa rasmi lakini alipofika katika kasri ya mfalme alipokonywa simu zake za mkononi na walinzi wake walitimuliwa huku wakitukanwa na maafisa wa usalama wa Saudia. Hapo alikabidhiwa barua ya kujiuzulu na akaambiwa aisome katika televisheni ya taifa ya Saudia. Badala ya kuenda hotelini alipelekwa katika nyumba maalumu iliyokuwa chini ya ulinzi mkali wa askari wa Saudia na wala hakuruhusiwa kuonana na mke na watoto wake. Lengo la Saudia lilikuwa ni kupunguza ushawishi wa harakati ya Hizbullah katika serikali ya Lebanon lakini njama hizo zimegonga mwamba. 

Wednesday, December 20, 2017

RSF: JUMLA YA WAANDISHI WA HABARI 65 WAMEUAWA MWAKA 2017

media
Waandishi wa habari wakiwa kwenye moja ya harakati za kuripoti matukio kwenye eneo la Israel na Palestina
Waandishi wa habari 65 na wafanyakazi wa vyombo vya habari wameuawa katika mwaka 2017, hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na shirika la wanahabari wasio na mipaka RSF.
Miongoni mwao 50 walikuwa ni maripota, hii ikiwa ni idadi ndogo zaidi katika kipindi cha miaka 14.
Hata hivyo ripoti inasema kuwa huenda kupungua kwa idadi ya vifo vya wanahabari imetokana na waandishi na ripota wengi kuacha kuripoti habari kwenye maeneo yenye vita.
Nchi ya Syria ambao kwa zaidi ya miaka 6 imeshuhudia vita vya wenywe kwa wenyewe, imesalia kuwa nchi hatari zaidi kwa waandishi wa habari kufanya kazi, imeonesha ripiti ya RSF ambayo imesema waandishi wa habari 12 waliuawa nchini humo, ikifuatiwa na Mexico ambako 11 waliuawa.
Miongoni mwa waliouawa nchini Mexico ni mwanahabari maarufu wa habari za biashara haramu ya dawa za kulevya nchini humo Javier Valdez ambaye mauaji yake yalitamausha wengi.
Waandamanaji nchini Kenya wakiwarushia mawe polisi na waandishi wa habari, waliokuwa wakiripoti maandamano ya kupinga vitendo vya rushwa, Nairobi, 3 Novemba, 2016.REUTERS/Thomas Mukoya
Mwandishi mwingine wa habari wa shirika la AFP aliuawa kwa kupigwa risasi nchini Mexico katika mji wa Kaskazini wa Sinaloa.
Nchi ya Ufilipino imekuwa ni taifa jingine hatari kwenye ukanda wa Asia kwa waandishi wa habari kufanya kazi ambapo ripiti inaonesha waandishi wa habari watano waliuawa kwa kupigwa risasi mwaka uliopita.
Ongezeko hili lilitokana na matamshi ya rais Rodrigo Duterte ambaye alisema “haimaanishi ukiwa muandishi wa habari basi ndio usiuawe ikiwa unajihusisha na biashara haramu”.
Hata hivyo hakukuwa na mwanahabari aliyeuawa mwaka uliotangulia nchini Ufilipino.
Waandishi wa habari nchini Misri wakiwa wamebeba kamera zao nje ya ofisi ya chama cha waandishi wa habari Reuters
Kiujumla ripoti ya RSF inasema kuwa idadi ya vifo vya wanataaluma wa habari imepungua kidunia katika kipindi cha miaka 14.
Katika vifo vya wanahabari 65, ripoti inaonesha kuwa wanahabari 39 waliuawa huku wengine wakipoteza maisha wakiwa kwenye majukumu yao ya kazi kama vile mashambulizi ya anga au yale ya kujitoa muhanga.
RSF inasema kuwa huenda pia vifo vimepungua kutokana na waandishi wengi wa habari kutopokea mafunzo ya kujilinda wakati wa vita.
Nchi ya Uturuki inatajwa kwenye ripoti hii kwa kuwa na magereza mengi ambayo waandishi wa habari wanashikiliwa, ambapo kwa sasa zaidi ya wanahabari 42 wanazuiliwa.
Nchi nyingine zinazofunga waandishi wa habari kwenye jela zake ni pamoja na Syria ambako kuna wanahabari 24, Iran wapo 23 na Vietnam ambako wako 19.

DRC: MKUTANO KATI YA RAIS KABILA NA MAGAVANA WAMALIZIKA GOMA

media
Rais wa DRC Joseph Kabila
Rais JOSEPH KABILA pamoja na viongozi wa ngazi za juu nchini DRC, waliokutana jijini GOMA tangu jumatatu wamehitimisha mkutano wao usiku wa kuamkia leo huku wakiwataka raia wa nchi hiyo kutojihusisha wala kujiunga na makundi ya waasi yanayotatiza usalama kwenye eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
"Tumewaalika raia wa Congo kuilinda nchi yao piya twa shukuru wana jeshi ambao hivi sasa wajitahidi katika ulinzi wa raïa wilayani KASAI."
Huko magaavana walio shiriki mkutano huo walijulisha umuhimu wa mazungumzo yao dhidi ya raïa wa Congo DRC, kama alivyo julisha LOLA KISANGA liwali wa Jimbo la UELE.
"Twatazama yote tukiona jinsi gani usalama wa kweli waweza rejea na kusaidia kwa ujenzi bora wa nchi yetu"
Raia wamepokeaje yaliyo zungumziwa jijini Goma na viongozi serikali ya Congo DRC !
"Ikiwa hakuna upendo haya yote ni kupoteza mda.cha maana magavana hao watimize waliyo zungumza."
Licha ya kutozungumza na wanahabari kwenye mkutano huo, duru za ndani zinaeleza kuwa rais Joseph Kabila aliwakosoa viongozi ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa na ubadhirifu wakati huu wakijua anaelekea kumaliza muda wake.
Viongozi hao wa serikali ya Congo DRC wamethibitisha kuendesha mkutano kama na huo jijini MBANDAKA mwezi machi mwaka ujao kwa lengo la kuboresha zaidi uchumi na maendeleo ya jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

UGANDA NA DRC KUSHIRIKIANA KATIKA KUPAMBANA NA WAASI WA ADF

Uganda na DRC kushirikiana katika kupambana na waasi wa ADF
Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimekubaliana kuimarisha utaratibu wa mawasiliano na kupeana taarifa za kiintelijensia kwa ajili ya kupambana na waasi wa ADF kufuatia mashambulizi yao dhidi ya vikosi vya walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa jeshi la Uganda Brigedia Richard Karemire amesema serikali ya Uganda na maofisa wa Kivu ya Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamekuwa na mkutano wa usalama.
Msemaji huyo amesema kupeana taarifa kutasaidia vikosi vijiandae kuwazuia waasi kujipenyeza ndani na mashambulizi yanayoweza kufanywa na ADF.
Hivi karibuni askari 14 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)  waliuawa , 44 walijeruhiwa na wengine wawili  hawajulikani walipo kufuatia hujuma ya waasi wa ADF.
Askari wa Tanzania walio katika kikosi cha kulinda amani cha UN nchini DRC
Tukio hilo lilitokea Desemba 7,2017 katika kambi ndogo iliyopo katika daraja la Mto Simulike, kaskazini mashariki mwa Wilaya ya Beni, Jimbo la Kivu.
Askari waliouawa walikuwa ni sehemu ya askari 3,000 wa tume ya kulinda amani ya umoja wa mataifa MONUSCO yenye askari kutoka Tanzania, Malawi na Afrika Kusini.

MAREKANI YATENGWA KATIKA KIKAO BARAZA LA USALAMA KILICHAJADILI MAPATANO YA NYUKLIA YA IRANI

Marekani yatengwa katika kikao cha Baraza la Usalama kilichojadili mapatano ya nyuklia ya Iran
Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameashiria kufanyika Kikao cha Baraza la Usalama la umoja huo kuhusu azimio nambari 2231 la mapatano ya nyuklia ya Iran na kusema washiriki wa kikao hicho walitangaza kuunga mkono mapatano hayo na kwamba kikao hicho kilithibitisha namna Marekani ilivyotengwa.
Siku ya Jumanne, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitisha kikao kujadili mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji JCPOA yaliyofikiwa mwaka 2015 baina ya Iran na Russia, China, Uingereza, Ufaransa, Marekani na Ujerumani. Baada ya mapatano hayo, Baraza la Usalama lilipasisha azimio nambari 2231 kuhusu kuunga mkono utekelezwaji mapatano hayo.
Katika kikao cha Jumanne, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley alitengwa na washiriki wote wa kikao wakiwemo Jeffrey Feltman Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Joanne Adamson Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya ambao wote waliunga mkono JCPOA.
Akizungumza katika kikao hicho, Gholamali Khoshroo mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa alisisitiza kuwa, Iran, kinyume na Marekani, inafungamana kikamilifu na JCPOA na hilo limethibitishwa katika ripoti 9 za Wakala wa Nyuklia wa Umoja wa Mataifa IAEA.
Gholamali Khoshroo mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa
Mwakilishi wa Iran pia akijibu madai ya Nikki Haley katika kikao hicho kuwa eti Iran inatoa msaada wa kijeshi kwa Yemen alisema: "Mwakilishi wa Marekani anatoa tuhuma bandia dhidi ya Iran pasina kuashiria namna harakati za kijeshi za serikali yake zinavyovuruga uthabiti wa eneo kwa kuuza silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola na kukabidhi baadhi ya silaha hizo kwa makundi ya kigaidi kama vile ISIS au Daesh."
Katika kikao hicho Feltman pia amepinga madai hayo ya Haley.
Ikumbukwe kuwa tokea Machi 2015 hadi sasa, Marekani imekuwa ikiunga mkono hujuma ya kinyama ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen na imekuwa ikiupa utawala huo wa Riyadh silaha ambazo hadi sasa zimewaua Wayemen zaidi ya 13,000, wengi wakiwa ni wanawake na watoto. 

UN YALAANI KITENDO CHA ISRAEL KUMPIGA RISASI KUMUUA MPALESTINA MLEMAVU

UN yalaani kitendo cha Israel kumpiga risasi na kumuua Mpalestina mlemavu
Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa amesema amestaajabishwa sana na kitendo cha jeshi la Israel kumuua kwa kumpiga risasi mtu mwenye ulemavu aliyekuwa anaelekea msikitini siku ya Ijumaa.
Zeid Ra'ad Al Hussein  Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa ametoa kauli hiyo kufuatia ripoti kwamba mtu huyo Ibrahim Abu Thurayeh aliuawa shahidi akiwa kwenye kitimwendo chake.
Ibrahim alikuwa miongoni mwa mamia ya Wapalestina walioandamana Ijumaa karibu na uzio kati ya Ukanda wa Gaza na Israel, wakipinga hatua ya Marekani kutambua mji wa Quds (Jerusalem) kuwa eti ni mji mkuu wa utawala bandia wa Israel.
Zeid amesema taarifa zinadhihirisha kuwa jeshi la Israel lilitumia nguvu nyingi kupita kiasi kitendo ambacho ni kinyume na sheria za kimataifa za kibinadamu.
Shahidi Ibrahim Abu Thureya
Hili ni janga la pili kumkuta Ibrahim ambapo mwaka 2008 makombora yaliyorushwa na Israel yalimkataa miguu yake miwili.
Afisa huyo wa Umoja wa Maaifa ametaka hatua za kisheria zichuliwe dhidi ya waliotekeza jinai hiyo.

Saturday, December 16, 2017

UINGEREZA YALAUMIWA KWA KUZIUZIA SILAHA TAWALA KANDAMIZI KAMA SAUDIA

Uingereza yalaumiwa kwa kuziuzia silaha tawala kandamizi kama Saudia
Mjumbe wa ngazi ya juu wa harakati ya kupambana na biashara ya silaha nchini Uingereza amesema London inaiunga mkono na kuihami Saudi Arabia na tawala nyingine kandamizaji duniani.
Andrew Smith ameliambia Shirika la Habari la Iran (IRNA) kwamba, asilimia 60 ya silaha za Uingereza zinauzwa kwa tawala zinazokiuka haki za binadamu na kwa watawala madikteta wa Mashariki ya Kati.
Smith ameongeza kuwa, serikali kama ya Uingereza ambazo zimekuwa zikimimina silaha katika maeneo yenye vita zinaiangalia maudhui hiyo kwa mtazamo wa kibiashara ili ziweze kujikurubisha zaidi kwa tawala kama Saudi Arabia na Bahrain.
Ameongeza kuwa Uingereza inaendelea kuiuzia silaha Saudi Arabia licha ya mauaji na mgogoro mkubwa wa kibinadamu unaoshuhudiwa sasa nchini Yemen ambao umesababishwa na mashambulizi na mzingiro wa serikali ya Riyadh dhidi ya nchi hiyo. 
Andrew Smith ameongeza kuwa, tangu mwanzoni mwa mgogoro wa Yemen, Uingereza imeuizia Saudi Arabia silaha zenye thamani ya pauni bilioni 4 na milioni mia 600. 
Vilevile harakati inayopinga biashara ya silaha nchini Uingereza imewasilisha mashtaka dhidi ya serikali ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Theresa May na kutoa wito wa kusitishwa mara moja mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia.

ZARIF: IRAN ITAISTAKI MAREMAKNI UMOJA WA MATAIFA

Zarif: Iran itaishtaki Marekani Umoja wa Mataifa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu itayawasilisha Umoja wa Mataifa madai ya Nikki Haley, balozi wa Marekani katika umoja huo kwamba eti Iran imeipatia silaha harakati ya Ansarullah ya Yemen.
Katika ujumbe wa baruapepe aliotuma kwa shirika la habari la Russia la Sputnik, Dakta Zarif ameandika: Jamhuri ya Kiislamu itawasilisha malalamiko Umoja wa Mataifa dhidi ya madai yaliyotolewa na Marekani.
Siku ya Alkhamisi iliyopita, huku akiwa amesimama kando ya mabaki kadhaa ya vyuma, Haley alianzisha propaganda mpya dhidi ya Iran kwa kudai kwamba vyuma hivyo ni mabaki ya makombora ya Iran.
Pasi na kuashiria misaada ya silaha inayotolewa na Marekani kwa Saudi Arabia, silaha ambazo zinatumika kuwashambulia raia madhulumu wa Yemen, Haley aliituhumu Iran kuwa eti inaizatiti kwa silaha harakati ya Ansarullah ya Yemen kwa ajili ya kuishambulia kwa makombora Saudia.
Nikki Haley akiwa amesimama kando ya vyuma alivyodai kuwa ni mabaki ya makombora ya Iran
Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq ameyakanusha madai hayo yaliyotolewa na balozi wa Marekani katika umoja huo.
Kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani, tangu mwezi Machi mwaka 2015 Saudi Arabia imeanzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa ardhini, baharini na angani. Moto wa vita uliowashwa na Saudia na waitifaki wake hadi sasa umesababisha makumi ya maelfu ya watu kuuawa na kujeruhiwa na mamilioni ya wengine kubaki bila makaazi.
Muungano huo vamizi wa kijeshi unaoongozwa na utawala wa Aal Saud umekuwa kila mara ukidai kwamba Iran inavipatia vikosi vya wananchi wa Yemen silaha na makombora na kwamba eti kwa kufanya hivyo inakwamisha utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo.
Hata hivyo viongozi wa Yemen wamesisitiza mara kadhaa kuwa uwezo wa kiulinzi na wa kujihami wa jeshi la nchi hiyo unatokana na nguvu zake za ndani na kwamba licha ya mzingiro wa kila upande uliowekwa na utawala wa Aal Saud, uwezo huo unaongezeka siku baada ya siku.
Utawala wa Aal Saud na Marekani hadi sasa zimeshindwa kufikia malengo yao nchini Yemen ya kuwaweka vibaraka wao madarakani kutokana na muqawama wa wananchi wa nchi hiyo.../

Tuesday, December 12, 2017

ZAIDI YA WATOTO LAKI NNE DRC WANAKABILIWA NA HATARI YA KIFO KUTOKANA NA UTAPIAMLO

Zaidi ya watoto laki nne DRC wanakabiliwa na hatari ya kifo kutokana na utapiamlo
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF limeonya kuwa, zaidi ya watoto laki nne walio chini ya umri wa miaka mitano wanakumbwa na utapiamlo mkubwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Taarifa ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF imetahadharisha kuwa,  watoto hao wanaweza kufariki dunia katika kipindi cha miezi michache kutoka sasa kama hatua za haraka hazitachukuliwa.
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF limetangaza katikka taarifa yake kwamba, mgogoro uliopo kwenye jimbo la Kasai na kudorora kwa shughuli za kilimo ni sababu kubwa ya tatizo hilo. 
Aidha shirika hilo la kimataifa limesema kuwa, licha ya usalama kuboreka katika baadhi ya maeneo na hata raia kuanza kurejea katika makazi yao, lakini hali ya kibinadamu bado ni mbaya  kutokana na kukosekana huduma muhimu.
Nembo ya UNICEF
Ripoti ya UNICEF inaonyesha kuwa, baadhi yya maeneo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hayana kabisa huduma za afya kutokana na baadhi ya vituo kuporwa vifaa vyake au kuharibiwa.
Maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa uwanja wa mapigano na mauaji kwa miaka 20 sasa. Kushindwa jeshi la serikali na askari wa kofia buluu wa kikosi cha Umoja wa Mataifa kukabiliana vilivyo na waasi ni moja ya sababu kuu za kukosekana utulivu na amani katika maeneo hayo kwa miaka 20 sasa.

Monday, December 11, 2017

WATU 9 WAUAWA NA KUJERUHIWA KATIKA SHAMBULIO LA WANAMGAMBO KASKAZINI MWA MALI

Hata askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wameshindwa kuzima uasi nchini Mali Hata askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wameshindwa kuzima uasi nchini Mali
Duru za kiusalama za Mali zimetangaza kuwa watu sita wameuawa na wengine watatu kujeruhiwa katika shambulizi lililofanywa na watu wenye silaha katika mji wa Timbuktu wa kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Duru hizo zimesema, baadhi ya watu waliouawa ni wanachama wa kundi linalojulikana kwa jina la Tawariq.
Watu hao wameuawa baada ya gari lao kushambuliwa na watu wenye silaha ambapo mbali na kuuawa watu sita na kujeruhiwa wengine watatu, watu wengine wawili waliokuwemo kwenye gari hiyo hadi hivi sasa hawajulikani waliko.
Mwanajeshi wa Ufaransa nchini Mali
Nchi ya Mali ilikumbwa na machafuko tangu mwaka 2012 wakati yalipotokea mapinduzi ya kijeshi na hapo hapo ukazuka uasi kaskazini mwa nchi hiyo uliopelekea kutekwa na waasi, eneo kubwa la nchi hiyo.
Askari wa Umoja wa Mataifa pamoja na wale wa mkoloni Ufaransa walitumwa nchini Mali katikati ya mwaka 2013, lakini pamoja na hayo wameshindwa kuzima uasi huo licha ya kukomboa baadhi ya maeneo yaliyokuwa yametekwa.
Licha ya kutiwa saini makubaliano ya amani baina ya serikali ya Mali na makundi yenye silaha ya kaskaizni mwa nchi hiyo mwaka 2015, lakini machafuko bado yanaendelea huku mauaji ya mara kwa mara na mashambulizi ya kushitukiza yakiripotiwa katika maeneo tofauti ya kaskazini mwa nchi hiyo.

WANANCHI WA MAURITANIA WAANDAMANA KUMLAANI DONALD TRUMP

Wananchi wa Mauritania waandamana kumlaani Donald Trump
Wananchi wa Mauritania wameungana na Waislamu na wapenda haki katika kona zote za dunia kuendeleza maandamano ya kumlaani rais wa Marekani, Donald Trump kwa hatua yake ya kuitambua Quds kuwa mji mkuu wa utawala pandikizi wa Israel.
Mtandao wa gazeti la al Quds al Arabi umetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, maeneo mbalimbali ya Mauritania yameendelea kushuhudia maandamano ya kupinga uamuzi wa Trump kuhusiana na mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas huku maelfu ya watu walioshiriki kwenye maandamano hayo wakitoa nara za "Mauti kwa Marekani," "Quds ni Yetu," "Mtake Msitake, Quds ni Mji Mkuu wa Palestina" na "Hatutoruhusu Kuporwa Quds." 
Wananchi na viongozi muhimu wa Mauritania katika maandamano

Watu wa matabaka mbalimbali nchini Mauritania wametoa matamko wakiitaka serikali ya nchi hiyo na nchi nyingine za Kiarabu na Kiislamu kukata uhusiano wao na Marekani kama njia ya kupinga uamuzi wa Donald Trump wa kuitambua rasmi Baytul Muqaddas kuwa kuwa eti ni mji mkuu wa Israel.
Donald Trump alitumia hotuba yake ya siku ya Jumatano kufanya uchokozi wa wazi kwa kuitangaza Quds ambayo ina Kibla cha Kwanza cha Waislamu kuwa eti ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni na hapo hapo akatoa amri ya kuanza mchakato wa kuhamishiwa Baytul Muqaddas, ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv, mji mkuu wa utawala wa Kizayuni.
Viongozi wa nchi mbalimbali duniani nao wamelaani hatua hiyo wakiwemo wa Ulaya kama Uingereza na Papa Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani. Hata Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini ameubeza uamuzi huo wa rais wa Marekani wa kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa Israel na kusema kuwa, hakuna nchi inayoitwa Israel hata Baitul Muqaddas uwe mji mkuu wake.

WANAWAKE WALIONYANYASWA KINGONO NA TRUMP WAITAKA KONGRESI KUFANYA UCHUNGUZI

Wanawake walionyanyaswa kingono na Trump waitaka Kongresi kufanya uchunguzi
Wanawake wanaomtuhumu Rais Donald Trump wa Marekani kwamba aliwanyanyasa kingono wamelitaka Bunge la nchi hiyo (Kongresi) kufanya uchunguzi kuhusu kashfa za kimaadili za kiongozi huyo.
Wanawake hao wanaosema walinyanyaswa kijinsia na Trump walitarajiwa kukutana leo kwa mara ya kwanza na kutoa wito wa kuanza uchunguzi kuhusu kashfa za kingono za Donald Trump.
Wakati huo huo balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley amesema kuwa wanawake wanaomtuhumu Rais Donald Trump kuwa aliwanyanyasa kijinsia wanapaswa kuzikilizwa.
Haley amesema wanawake hao wanapaswa kusikilizwa na kesi yao inapaswa kushughulikiwa.
Gavana huyo wa zamani na mmoja kati ya wanawake wenye vyeo vya juu katika utawala wa Trump, amesema wakati umefika wa kutafakari kwa kina kuhusu jinsi wanawake wanavyotendewa nchini Marekani.
Nikki Haley
Matamshi hayo ya balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa yanakwenda kinyume kabisa na sisitizo la serikali ya nchi hiyo ambayo imekuwa ikidai kuwa kashfa za kuwanyanyasa kijinsia wanawake zinazomkabili Donald Trump hazina msingi.
Makumi ya wanawake wamemtuhumu Rais Donald Trump wa Marekani kuwa aliwanyanyasa kingono ikiwa ni pamoja na kuwapapasa papasa, kuwabusu kwa kuwalazimisha na kutumia maneno machafu na ya utovu wa maadili.

DUNIA IMEUNGANA KUMLAANI DONALD TRUMP

Iran: Dunia imeungana kumlaani Donald Trump
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran leo amezungumza na waandishi wa habari kuhusiana na masuala mengi tofauti ikiwemo ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Uingereza hapa mjini Tehran, suala la Quds, Yemen na masuala mengine mbalimbali.
Akijibu swali la mwandishi wa Radio Tehran kuhusiana na ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Uingereza hapa Iran ambayo imekwenda sambamba na hatua ya rais wa Marekani la kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa Israel, Bahram Qassemi amesema, ziara ya Boris Johnson waziri wa mambo ya nje wa Uingereza hapa Tehran ilikuwa imepangwa tangu zamani na haina uhusiano wowote na hatua hiyo ya Donald Trump.
Donald Trump analaaniwa katika kila kona ya dunia

Vile vile amesema, dunia nzima imeungana hivi sasa kumlaani Donald Trump kwa hatua yake hiyo na nchi nyingi za dunia zikiwemo za Kiarabu zinaendelea kukabiliana na uchokozi huo wa rais wa Marekani kwa njia mbalimbali.
Amma kuhusiana na msimamo wa Iran kuhusu Yemen, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, msimamo wetu kuhusu Yemen haujabadilika na hautobadilika, kwanza sera zetu ni kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine lakini pia tutaendelea kufanya juhudi za kuwatangazia walimwengu dhulma wanayofanyiwa wananchi wa Yemen.
Amma kuhusiana na hatua ya Bahrain kutuma ujumbe wake kwenda kuonana na viongozi wa utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, Qasemi amesema, ziara hiyo haina maana, ni kosa na ni kitendo cha aibu ambacho kimeonesha sura halisi ya baadhi ya nchi za Kiarabu zinazoiunga mkono Israel inayozikaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina kikiwemo Kibla cha Kwanza cha Waislamu.