Kufuatia uamuzi wa Robert Harward kukataa
ombi la Rais Donald Trump wa Marekani la kusimamia usalama wa taifa,
timu ya usalama ya rais huyo imeingia katika hatua mpya ya mgogoro ambao
haujawahi kushuhudiwa katika historia ya Ikulu ya White House.
Katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja tokea serikali mpya ya
Marekani iingie madarakani, mshauri wa masuala ya usalama wa taifa
amelazimishwa kujiuzulu na mwingine aliyependekezwa kuchukua nafasi hiyo
muhimu kukataa pendekezo hilo. Baada ya kujiuzulu Michael Flynn
kutokana na tuhuma za kuwa na mawasiliano ya karibu na Warussia, Rais
Donald Trump alimuarifisha Robert Harward kuwa mshauri mpya wa usalama
wa taifa wa nchi hiyo. Pamoja na hayo lakini jenerali huyo mstaafu
hakuwa tayari kushirikiana na serikali ya Trump. Licha ya White House
kudai kwamba Robert Harward alikataa ombi hilo kutokana na sababu za
kifamilia lakini wajuzi wa mambo wanasema kuwa jenerali huyo mstaafu
alikataa ombi hilo kutokana na hitalafu kubwa za mitazamo zilizopo baina
yake na washauri wa karibu wa Trump.
Inasemekana kuwa Harward alikusudia kuipa makao timu yake ya masuala
ya usalama wa taifa katika majengo ya White House jambo ambalo
lilipingwa vikali na watu walio na ushawishi katika ikulu hiyo.
Inasemekana kuwa sisitizo la White House la kuendelea kulinda nafasi za
wasaidizi wa Flynn ni moja ya mambo yaliyozua hitilafu hizo. Wakati
huohuo inasemekana kwamba uingiliaji wa mara kwa mara wa Stephen Kevin
Bannon, mwanastratejia mkuu wa Trump katika masuala ya uendeshaji wa
Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani ni moja ya sababu ambazo
zimempelekea Harward kukataa nafasi ya kusimamia masuala ya usalama wa
taifa. Hali ni mbaya kiasia kwamba hata baadhi ya ripoti zinasema kwamba
Flynn alilazimishwa kujiuzulu si kutokana na mawasiliano yake na
maafisa wa Russia bali kwa sababu ya vita vya ndani katika Baraza la
Usalama wa Kitaifa ambavyo vimetokana na mabadiliko makubwa ambayo
yamefanywa kwenye baraza hilo na Rais Trump. Kabla ya kuingia White
House Trump alikuwa na ugomvi mkubwa na vyombo vya upelelezi na usalama
vya nchi hiyo.
Akiwa rais mteule wa Marekani, alipinga ripoti muhimu zilizoonyesha
kuwa Warussia waliathiri mkondo wa uchaguzi wa hivi karibuni wa nchi
hiyo na kutumia maneneo makali na ya dharau dhidi ya viongozi wa jamii
ya wanahabari wa masuala ya usalama wa Marekani, jambo ambalo liliamsha
wimbi la hasira na ukosoaji dhidi ya rais huyo. Hata baada ya kuingia
ikulu ukosoaji huo bado haujapungua bali umeongezeka na kuchukua sura
mpya. Uingiliaji wa Bannon ambaye ana misimamo mikali na ya kibaguzi ya
mrengo wa kulia katika Baraza la Usalama wa Taifa umezidisha mivutano
katika bara hilo na hata kupelekea baadhi ya ripoti za siri kuvuja na
kuenea kwenye vyombo vya habari. Suala hilo limempelekea Rais Trump
kuvituhumu vyombo vya habari za siri na usalama vya Marekani kuwa ndivyo
vimekuwa vikivujisha habari hizo.
Katika hali hiyo ya kuwepo mvutano kati ya Rais Trump na vyombo vya
habari za siri na usalama vya Marekani ni wazi kuwa juhudi za rais huyo
za kujaribu kumketisha Bannon kwenye kiti kilichoachwa wazi na Flynn
zitakabiliwa na upinzani mkubwa wa mahasimu wa Bannon. Hii ni katika
hali ambayo serikali ya Trump ndio kwanza imeanza shughuli za kuandaa
sera za nje na masuala ya usalama za nchi hiyo. Mshauri wa Usalama wa
Taifa wa Marekani ana jukumu muhimu la kuratibu shughuli za vyombo
vilivyo chini yake katika masuala ya siasa za nje, ulinzi na usalama wa
Marekani na kwa msingi huo kutokuwepo kwake tena katika mazingira haya
ambapo viongozi wa nchi hiyo wanakabiliwa na kashfa na matatizo makubwa
ya kiuongozi kutatoa pigo kubwa kwa uwezo, nguvu na hadhi ya Marekani
dunaini.
No comments:
Post a Comment