Mwito wa Marekani kwa wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO
kuongeza matumizi yao ya ulinzi ulitarajiwa na umepokelewa vizuri,
waziri wa ulinzi wa Marekani James Mattis alisema leo baada ya
kuhudhuria mkutano wake wa kwanza na mawaziri wa ulinzi wa NATO mjini
Brussels. Jana Mattis aliwaambia mawaziri wenzake wa NATO kwamba
Marekani itapunguza ushiriki wake kwa muungano huo hadi pale mataifa
wanachama yatakapofanya mipango kufikia kiwango kinachotakiwa na NATO
cha matumizi ya ulinzi cha asilimia 2 ya pato jumla la taifa. Siku ya
Jumatano Mattis aliwaambia wanachama wa NATO kwamba wanapaswa
kutayarisha mpango hadi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu juu ya njia za
kufikia kiwango hicho cha asilimia 2, ambacho kiliwekwa mwaka 2014 kwa
mujibu wa mabadiliko ya hali ya usalama wa dunia. Muda wa mwisho kufikia
lengo hilo ni mwaka 2024.
No comments:
Post a Comment