Makumi ya watu wameuawa hadi sasa tangu
kuanza tena mapigano katika mkoa wa Tanganyika nchini Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo mwezi Julai mwaka jana.
Richard Ngoie Kiatngala, Gavana wa mkoa wa Tanganyika mashariki
mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesisitiza wakati wa kuanza
kikao cha kujadili amani na suluhu kati ya makabila ya Luba (Bantu) na
Pygmees kuwa, katika mapigano hayo watu 150 wameuawa hadi sasa, 200
wamejeruhiwa, shule 400 zimebomolewa na vijiji 422 kuchomwa moto. Gavana
huyo wa mkoa wa Tanganyika ameongeza kuwa kesi 200 za ubakaji
zimethibitishwa kutokea kufuatia mapigano hayo ya kikabila; huku
asilimia 76.4 ya wakazi wa mkoa wa Tanganyika wakikabiliwa na uhaba wa
chakula na mlipuko wa maradhi ya kipindupindu na surua.
Gavana wa mkoa wa Tanganyika ametaka kurejeshwa haraka amani na
utulivu katika mkoa huo. Wakati huo huo Emmanuel Ramazani Shadary Waziri
wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
amesema kuwa hali ya mkoa wa Tanganyika inatia wasiwasi na kuzitolea
mwito pande zinazozozana kufanya mazungumzo. Mkoa wa Tanganyika
umekumbwa na mapigano ya umwagaji damu baina ya makabila mawili ya Luba
na Pygmees tangu miezi kadhaa iliyopita hadi sasa.
No comments:
Post a Comment