Saturday, February 25, 2017

WASHIRIKA WA MUGABE KUSHIRIKI SHEREHE YA KUZAKIWA

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe aliyefikisha miaka 93 wiki hii, leo anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kufanya sherehe ya kifahari itakayohudhuriwa na maelfu ya wanaomuunga mkono nje ya mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa Bulawayo. Chama tawala, ZANU-PF kinaandaa sherehe ya kiongozi huyo aliyeko madarakani tangu mwaka 1980 na utawala wake ukiwa umegubikwa na ukandamizaji wa wapinzani, udanganyifu wa kura na kuanguka kwa uchumi. Kiongozi huyo wa taifa mwenye umri mkubwa zaidi duniani kwa sasa, amekuwa akisherehekea siku hii kwa wiki nzima, huku kituo cha televisheni cha taifa kikimmwagia sifa kemkem na pongezi. Sherehe hiyo inagharimu Dola Milioni 1, hatua iliyowaghadhabisha Wazimbawe wengi kufuatia upungufu wa chakula unaoikabili nchi hiyo. Kufanyika kwa sherehe hiyo katika shule ya Matobo kumewachukiza wakazi wa eneo hilo kwa kile kinachoaminika kuwa wahanga wa machafuko dhidi ya wapinzani chini ya utawala wake katika miaka ya 1980 walizikwa eneo hilo.

No comments:

Post a Comment