Sunday, February 19, 2017

39 WAUAWA KATIKA HUJUMA YA KIGAIDI MOGADISHU

Watu wasiopungua 39 wameuawa leo Jumapili wakati gari lililokuwa limesheheni mabomu liliporipuka katika makutano ya barabara katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Mlipuko huo ni hujuma ya kwanza kubwa kujiri Somalia tokea aingie madarakani rais mpya wa Somalia Mohammad Abdullahi Mohamad, maarufu kama Farmaajo, wiki jana.
Walioshuhudia wanasema mlipuko huo ulilenga makutano ya barabara katika mtaa wa Madina, kusini mwa Mogadishu. Mlipuko huo ulilenga wanajeshi na wafanyabiashara pamoja na wapita njia katika eneo hilo lenye msongamano mkubwa wa watu na magari. Baadhi ya walioshuhudia wanasema idadi iliyotangazwa ni chini ya wale waliouawa katika hujuma hiyo ya kigaidi.
Shambulizi hilo linaashiria changamoto alizonazo rais mpya wa Somalia ambaye amerithi serikali ambayo haikuwa na udhibiti katika maeneo mengi ya nchi hiyo ambayo yanakaliwa kwa mabavu na kundi la kigaidi la Al Shabab.
Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika Somalia AMISOM waliwatimua magaidi wa Al Shabab kutoka Mogadishu Agosti mwaka 2011 lakini magaidi hao wanaendelea kushikilia maeneo mengine ya nchi hiyo na hujipenyeza mara kwa mara katika mji mkuu kutekeleza mashambulizi.

No comments:

Post a Comment