Saturday, February 18, 2017

HUENDA SHEIKH ZAKZAKY AKAFUNGULIWA MASHTAKA KATIKA JIMBO LA KADUNA

Duru za kuaminika nchini Nigeria zimeripoti kuwa huenda kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky akafunguliwa mashtaka katika jimbo la kaskazini la Kaduna.
Licha ya Mahakama Kuu ya Nigeria kutoa hukumu kwamba Sheikh Zakzaky hana hatia na kuamuru kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu pamoja na mkewe waachiliwe huru, baadhi ya duru zimetangaza kuwa Sheikh Zakazky amekabidhiwa kwa mamlaka za jimbo la Kaduna kaskazini mwa nchi hiyo kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka kuhusiana na harakati alizoendesha katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita.
Kwa mujibu wa ripoti hizo, Mkuu wa Mashtaka wa Serikali ndiye aliyewasilisha ombi la kutaka Sheikh Zakzaky akabidhiwe kwa mamlaka za jimbo la Kaduna.
Sheikh Ibrahim Zakzaky
Hayo yanajiri huku ripoti zikieleza kuwa hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky ni mbaya. Mahakama Kuu ya Nigeria ya mjini Abuja, mbali na kutoa hukumu ya kuamuru kiongozi huyo wa kidini aachiliwe huru imewataka pia viongozi wa mamlaka husika kuijenga upya nyumba yake iliyobomolewa na askari wa jeshi la serikali pamoja na kumlipa fidia.
Wakati huohuo, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imetoa onyo kwa maafisa wa serikali na wa vyombo vya mahakama kutokana na kupuuza kwao agizo la Mahakama la kumwachia huru Sheikh Zakzaky na kusisitiza kwamba serikali ya Nigeria inapaswa iheshimu shughuli za kijamii na za kisheria za Waislamu wa Kishia wa nchi hiyo.
Waislamu wa Nigeria wakiandamana kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru
Matukio ya kisiasa na kijamii yanayojiri nchini Nigeria yanaonyesha kuwa Marekani, Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel zina hofu ya kuongezeka ushawishi wa kimaanawi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia barani Afrika na kuimarika nafasi ya Mapinduzi ya Kiislamu miongoni mwa watu wa jamii za bara hilo. Kwa sababu hiyo, zimekuwa zikiongeza msukumo na uungaji mkono wao kwa hatua za serikali ya Nigeria dhidi ya Waislamu wa Kishia katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Wimbi la ukandamizaji dhidi ya Waislamu nchini Nigeria lilishtadi tarehe 13 ya mwezi Desemba mwaka 2015 wakati askari wa jeshi walipovamia Husainiyyah ya mji wa Zaria katika jimbo la Kaduna. Katika jinai hiyo jeshi la Nigeria liliwaua shahidi mamia ya Waislamu wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky…/

No comments:

Post a Comment