Umri wa kuishi waongezeka kwa wanawake na wanaume
Utafiti mpya umebaini watu wataendelea kuishi umri
mrefu zaidi katika nchi zinazoendelea. Katika nchi hizo watu watafikisha
umri wa miaka 90 na zaidi. Tofauti ya kuishi kati ya wanaume na
wanawake pia imepungua
Watafiti kwa muda mrefu wamekuwa na mashaka mashaka iwapo kweli watu
wanaweza kuishi kwa umri mrefu wa zaidi ya miaka 90 lakini wanasayansi
wa chuo cha Imperial cha mjini London wamebainisha rasmi kuwa kwa sasa
kuna uwezekano mkubwa kwa watu kuendelea kuishi zaidi kuliko ilivyokuwa
hapo awali.
kwa mujibu wa Profesa Majid Ezzati, kufikia mwaka
2030 nchi kama Korea ya Kusini, Australia na uswizi miongoni mwa nchi
nyingine zitajivunia kuwa watu wake wanaishi maisha marefu. Korea ya
Kusini ndio nchi ya kwanza duniani ambapo wanawake wa nchi hiyo wana
matumaini ya kuishi na umri mrefu wa zaidi ya miaka 90 huku nchi
nyingine zilizoendelea zikifuata kwa ukaribu kwa raia wake kuweza kuishi
hadi kufikia miaka 88.
Profesa Ezzati hata hivyo anazishauri
nchi husika kuanza kuweka mikakati kabambe ya kuwatunza vizee, amesema
pia mabadiliko kama hayo yanahitaji mipango mingine pia ibadilike ili
kuweka mambo sawa ametolea mfano mpango wa mafao ya uzeeni au pensheni.
Vipimo vya uhai katika nchi mbalimbali
Wanasayansi
hao walizingatia vipengele mbalimbali katika utafiti wao juu ya hali
ya binadamu na jinsi anavyozeeka na kwa kiwango gani. Wanasayaansi hao
wa chuo cha Imperial cha mjini London wamesema matibabu mazuri,
uwezekano mkubwa wa kupata maji safi, lishe bora na kupungua kwa maradhi
ya hatari ni mambo yanayochangia kwa kiwango kikubwa katika kuongezeka
umri wa kuishi ikiwa ni pamoja na kuepuka vita, majanga asilia, njaa na
magonjwa ya mripuko. Wanasayansi hao wamesema sababu nyingine kama
simanzi, shinikizo, umasikini, mfumo wa maisha pamoja na kufanya mazoezi
ni mambo yanayochangia zaidi katika kupatikana jawabu iwapo watu wa
eneo fulani wanaweza kuishi kwa umri mrefu zaidi au la.
Mnamo
mwaka 2015 utafiti kama huo ulibaini nchi tano ambazo raia wake
wangekuwa na umri mfupi zaidi wa kuishi ukiwa ni kati ya miaka 50 hadi
chini ya miaka 55 kwa wanawake na wanaume zilikuwa ni nchi za barani
Afrika.
Ripoti hiyo imeionyesha Marekani ikiburuza mkia katika
nchi zilizo na utajiri mkubwa duniani. Watafiti wanasema kutokana hali
inayoongezeka ya vifo vya watoto, mauaji na magonjwa sugu ni mambo
yanachochea kupunguza umri wa kuishi. Wataalamu hao wamesema vifo vingi
vya watoto hutokea baada kuzaliwa nchini Marekani kuliko nchi nyingine
yoyote yenye kiwango cha juu cha mapato, wanahofia kuwa hali hiyo
itaendelea.
No comments:
Post a Comment