Katika kusaidia
Tanzania kuwa moja ya nchi ambazo wananchi wake wana lishe salama, Umoja
wa Ulaya (EU) umechangia Euro milioni 9.5 (Tsh. 22 Bilioni) kwa ajili
ya kusaidia kutekelezwa kwa mradi wa Lishe na Usalama wa Chakula
unaotekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula
Duniani (WFP) wenye thamani ya Euro milioni 24.5 (Tsh. 57.7 bilioni)
unaotarajiwa kufanyika katika mikoa ya kanda ya kati.
Akizungumza kuhusu
msaada huo, Mkuu wa Ubalozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Roeland Van De
Geer alisema EU imeamua kusaidia jamii ya Tanzania kupata lishe bora
kwani wao wanaamini kuwa pasipo lishe bora mambo mengi ambayo yanahusu
maendeleo ya taifa hayawezi kufanyika kwa kasi ambayo yanatakiwa kwenda
nayo lakini pia mpango wa kusaidia lishe salama ni moja ya mambo ambayo
EU imepanga kusaidia.
Mkuu
wa Ubalozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Roeland Van De Geer akizungumza
kuhusu mchango wa Euro milioni 9.5 (Tsh. 22 Bilioni) kwa ajili ya
kusaidia kutekelezwa kwa mradi wa Lishe na Usalama wa Chakula wa Shirika
la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP). (Picha zote na
Rabi Hume)
“Kupitia mradi huu EU
pamoja na WFP ziko katika nafasi nzuri ya kubaini na kuunga mkono
uhusiano katika kilimo, afya, usalama wa chakula na lishe ambao hapo
kabla haukuwa umeelezwa kwa kina na kufuatiliwa kikamilifu, matumaini
yetu ni kuwa viongozi na wananchi kwa pamoja wataungana kufanikisha
mradi huu,” alisema Van De Geer.
Nae Mwakilishi wa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Michael
Dunford aliishukuru EU kwa kutoa msaada ambao utawezesha jamii ya
Tanzania katika mikoa wa Dodoma na Singida kusaidiwa kupata lishe salama
ikiwa ni sehemu ya Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDGs).
Mwakilishi
wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP),
Michael Dunford akizungumza kuhusu mradi wa Lishe na Usalama wa Chakula.
“Tunashukuru kwa
mchango huu kutoka Umoja wa Ulaya kwani umeiwezesha WFP kuendelea na
programu hii bunifu inayolenga kukidhi mahitaji ya watu walio hatarini
zaidi na hasa watoto katika kipindi cha ukuaji wao” alisema Dunford.
Kwa upande wa Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk.
Mpoki Ulisubisya alisema mradi huo utafanyika kwa mikoa miwili ya
Dodoma na Singida ambapo takwimu za kudumaa kitaifa ni aslimia 34 na
Dodoma ni asilimia 34 na Singida ni 36.5 na utafanyika kwa miaka mitano.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Dk. Mpoki Ulisubisya akielezea jinsi mradi wa Lishe na Usalama wa
Chakula utakavyofanyika nchini, takwimu za kudumaa na mikoa ambayo
utafanyika.
Aidha Dk. Ulisubisya
alisema uwekezaji huo wa WFP utahusisha kuwapa chakula, kutoa elimu
jinsi ya kuzalisha vyakula vya aina mbalimbali, kuwawezesha kuwa na
wanyama, jinsi ya kuwa na mazao ya kuuza na walengwa wakubwa ni kina
mama wajawazito na watoto.
Mkuu
wa Ubalozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Roeland Van De Geer na Mwakilishi
wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP),
Michael Dunford wakisaini makubaliano ya Umoja wa Ulaya (EU) kutoa
mchango wa Euro milioni 9.5 (Tsh. 22 Bilioni) kwa ajili ya kusaidia
kutekelezwa kwa mradi wa Lishe na Usalama wa Chakula.
No comments:
Post a Comment