Waislamu nchini Marekani wamechangisha maelfu
ya dola kusaidia ukarabati wa makaburi ya Mayahudi yaliyobomolewa
katika jimbo la Missouri.
Kampeni hiyo iliyoanzishwa siku ya Jumanne kwa anuani ya "Umoja
wa Waislamu kwa ajili ya kukarabati makaburi ya Mayahudi" hadi kufikia
jana iliweza kukusanya zaidi ya dola 91,000 za Kimarekani japokuwa lengo
la awali lilikuwa ni kukusanya dola 20,000.
Mchango huo wa fedha umetolewa kusaidia kukarabati eneo la kihistoria
la makaburi ya Mayahudi ambayo yalibomolewa katika hujuma iliyofanywa
wiki iliyopita.
Taasisi ya Kiislamu iliyoanzisha mchango huo imeeleza kuwa katika
kuonyesha mshikamano na jamii ya Mayahudi ya Marekani Waislamu wa nchi
hiyo wanalaani kitendo hicho cha kuvunjia heshima eneo hilo la makaburi.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa lengo kila hatua ni kudhihirisha "maisha
na shakhsia ya Bwana Mtume Muhammad SAW" na kufikisha ujumbe kuwa
vitendo vya aina hiyo vya uenezaji chuki na uvunjiaji heshima matukufu
ya kidini havina nafasi ndani ya jamii ya Marekani.
Kwa mujibu wa Polisi ya jimbo la Missouri zaidi ya makaburi 170 yamebomolewa katika hujuma hiyo.
Hujuma hiyo imefanywa katika hali ambayo vitisho vya utegaji mabomu
vimetolewa dhidi ya vituo kadhaa vya Mayahudi katika maeneo mbalimbali
ya Marekani.
Ripoti zinaeleza kuwa tangu ulipoanza mwaka huu wa 2017 hadi siku ya
Jumatatu iliyopita vimetolewa vitisho visivyopungua 69 vya utegaji
mabomu dhidi ya vituo 54 vya Mayahudi katika nchi za Marekani na
Canada.
Tayari Polisi ya Upelelezi ya Marekani (FBI) imeanzisha uchunguzi juu ya suala hilo.../
No comments:
Post a Comment