Tuesday, April 25, 2017

MAREKANI YAWAWEKEA VIKWAZO WANASAYANSI 271 WA SYRIA

Marekani imewawekea vikwazo wafanyakazi zaidi ya 270 wa shirika la serikali ya Syria linalotuhumiwa kwa uundaji wa silaha za sumu, wiki kadhaa baada ya mashambulizi ya gesi ya sumu katika jimbo la Idlib.

IS Chemiewaffen Reaktionen Aleppo Syrien (picture-alliance/AP Photo)

Katika mojawapo ya hatua madhubuti kuwahi kuchukuliwa na Marekani, wizara ya fedha ya nchi hiyo imetangaza vikwazo vipya dhidi ya wanasayansi na baadhi ya maafisa wa nchini Syria kutokana na kuhusika kwao katika kuunda silaha za sumu, ambazo zinadaiwa kutumika kuwauwa raia zaidi ya watu 80 katika jimbo hilo la Idlib mapema mwezi huu.
Waziri wa fedha wa Marekani, Steven Mnuchin, amesema vikwazo hivyo vipya vinakilenga kituo cha kisayansi kinachomuunga mkono Rais Bashar al-Assad na pia wafanyakazi 271 wa kituo hicho kinachoshughulikia mitaala na utafiti wa kisanyansi (SSRC).  Marekani inadai kwamba kituo hicho kilihusika na utengenezaji wa gesi ya sumu aina ya Sarin iliyotumika katika mashambulizi hayo.
Mnuchin ameeleza kwamba Marekani inatoa ujumbe madhubuti na pia haitavumilia matumizi ya silaha za sumu yatakayofanywa na yeyote yule. "Marekani inadhamiria kuuwajibisha utawala wa Assad kwa tabia yake isiyokubalika," alisema Munchin, aliyeongeza kuwa vikwazo hivyo ni pamoja na kuwazuia Wamarekani kufanya biashara na watu hao waliotajwa.
Vikwazo baada ya mashambulizi
USA Steven Mnuchin in New York (picture-alliance/Newscom)
Waziri wa Fedha wa Marekani, Steven Mnuchin, anasema vikwazo dhidi ya wanasayansi hao vinajumuisha kugomea kushirikiana nao kibiashara na kitaaluma.
Vikwazo hivyo vinakuja wiki chache baada ya jeshi la nchi hiyo kuushambulia uwanja wa ndege za kivita wa Syria mnamo tarehe 7 Aprili ili kuuadhibu utawala wa Assad na kutoa onyo dhidi ya kufanya mashambulizi zaidi kwa kutumia silaha za sumu. 
Uwanja huo ulishambuliwa kwa makombora 59 ya masafa ya kati aina ya "Tomahawk". Huko nyuma, tayari wizara ya fedha ya Marekani ilishawawekea vikwazo maafisa wengine 18 wa Syria mnamo Januari mwaka huu.
Mashambulizi hayo ya silaha za sumu pia yalijadiliwa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini Urusi, ambayo nbi mshirika mkubwa wa Assad, iliitumia kura yake ya turufu kulizuia azimio lililoitaka serikali ya Syria itoe ushirikiano ili kuwezesha uchunguzi, huku Rais Assad akikanusha madai hayo dhidi ya nchi yake na kusema kwamba huo ni uzushi wa nchi za Magharibi.
Mnuchin amesema wizara yake "itashirikiana na wizara ya mambo ya nje pamoja na washirika wa kimataifa ili kuendeleza juhudi za kuhakikisha kwamba shughuli za kifedha za wote waliowekewa vikwazo zinafungwa."

SIKU YA MALARIA DUNIANI

Wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya malaria leo, shirika la afya duniani WHO limefahamisha hapo jana kuwa chanjo ya kwanza ya ugonjwa huo itaanza kufanyiwa majaribio nchini Kenya, Malawi na Ghana kuanzia mwaka 2018.

Malaria Mücke (picture alliance/blickwinkel/Hecker/Sauer)
Anopheles-mbu anayesababisha malaria
Chanjo hiyo ya kiwango kikubwa ilichukua miongo na mamilioni ya Dola kubuniwa.
Mratibu wa mpango wa kutekeleza chanjo hiyo Mary Hamel anasema chanjo hiyo kwa sasa imeshavuka ngazi ya kufanyiwa uchunguzi katika maabara na shirika la kudhibiti dawa la Ulaya limeisifu chanjo hiyo.
Chanjo hiyo iitwayo RTS,S ni kwaajili ya kuwakinga watoto wadogo dhidi ya aina mbaya ya malaria inayosababishwa na mbu aitwae Plasmodium falciparum. Itafanyiwa majaribio katika maeneo yatakayochaguliwa na nchi hizo tatu na maeneo hayo yanatakiwa kuwa na visa vingi vya maradhi ya malaria na pia kampeni za kupambana na ugonjwa huo.
Kulingana na Hamel, chanjo hiyo itatolewa kwa jumla ya watoto 360,000 walio kati ya umri wa miezi mitano na kumi na saba ili kubainisha iwapo dalili za kinga zilizooneshwa katika uchunguzi wa kliniki, zitaonekana pia katika hali ya kawaida ya maisha. Watoto watapokea chanjo hiyo mara tatu kwa mwezi wakiwa na umri wa miezi mitano na watapewa chanjo ya nne watakapotimiza miaka miwili.
Kenya, Ghana na Malawi zina mipango thabiti ya kinga ya malaria
Daktari Edward Mwangi ni afisa mkuu mtendaji wa muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali dhidi ya malaria nchini Kenya KeNaam, na anasema kinga hiyo ni muhimu na itasaidia pakubwa.
"Kwa mfano badala ya mtoto kuwa mgonjwa mara mbili au tatu kwa mwaka kutokana na malaria," alisema Edward, "atakuwa mgonjwa mara moja tu na jambo hili linapunguza idadi pia ya wale wanaokuwa wagonjwa ama wale wanaofariki kutokana na malaria mwisho wa siku," aliongeza afisa huyo wa KeNaam.
WHO inasema Kenya Ghana na Malawi ndizo nchi zilizochaguliwa kwa uchunguzi huo kutokana na kuwa nchi zote hizo zina mipango thabiti ya kinga lakini bado zina visa vingi vya malaria.
Pedro Alonso (picture-alliance/dpa/M. Trezzini)
Mkuu wa kitengo cha malaria WHO Pedro Alonso
WHO inatazamia kuangamiza malaria ifikiapo mwaka 2040 licha ya changamoto zilizoko katika vidonge na dawa zinazotumika kuwauwa mbu.
Daktari Mwangi lakini anasema kwamba chanjo hiyo haitokuwa mwisho wa malaria barani Afrika na sehemu zilizoathirika na maradhi hayo duniani.
Malaria ni changamoto kubwa ya kiafya inayoikabili dunia
"Chanjo hiyo ni nyongeza tu ya kupambana na malaria na labda kuuangamiza ugonjwa huo barani Afrika na sehemu nyengine," alisema Edward, "kwa hiyo kitakachofanyika ni kuwa, chanjo hiyo itatolewa, lakini zile mbinu zengine zinazotumika ili kujikinga dhidi ya malaria zitakuwa zikitumika pia, kama vile matumizi ya vyandarua na hata unapokuwa mgonjwa utaweza kutibiwa bado," aliongeza mkuu huyo wa KeNaam.
Simbabwe Moskitozelt (DW/P. Musvanh)
Utumizi wa vyandarua bado utaendelea hata baada ya chanjo hiyo kutolewa
Malaria inasalia kuwa mojawapo ya changamoto kubwa zaidi za kiafya zinazoikabili dunia, kwani zaidi ya watu milioni 200 huambukizwa kila mwaka na takriban nusu milioni kuaga dunia, wengi wao wakiwa watoto kutoka Afrika. Utumiaji wa vyandarua na dawa za kuuwa mbu ndiyo njia za pekee ambazo zimetumika kujikinga dhidi ya malaria.
Nchi zilizo chini ya jangwa la Sahara barani Afrika ndizo zilizoathirika pakubwa, huku ikiwa asilimia 90 ya visa vya malaria kote duniani mwaka 2015 vikitoka barani humo.
WHO inasema, juhudi za dunia za kukabiliana na malaria, zimepelekea visa vya vifo vinavyotokana na malaria kupungua kwa asilimia 62 kati ya mwaka 2000 na 2015. Lakini shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa linasema pia kwamba, takwimu kama hizo mara nyingi hutumiwa kwa masuala ya hesabu tu ila hali ni mbaya mno katika nchi 31 Afrika, kiasi ya kwamba haliwezi kuelezea iwapo kiwango kimekuwa kikiongezeka ama kushuka katika miaka 15 iliyopita.

Monday, April 24, 2017

UCHAGUZI WA RAIS WA IRAN KUFANYIKA KATIKA NCHI 102 DUNIANI

Tume ya Uchaguzi ya Iran imetangaza kuwa, uchaguzi wa rais wa awamu ya 12 wa Iran utafanyika katika nchi 102 kote duniani.
Katika taarifa, Katibu wa Tume ya Uchaguzi Ali Pur-Ali Mutlaq amesema Wairani wanaoishi nje ya nchi wataweza kupiga kura katika viituo 269 vya upigaji kura vilivyoko katika ofisi 131 za kidiplomasia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi 102 kote duniani.
Ameongeza kuwa, wawakilishi wa Iran katika nchi hizo  tayari wameshapokea kila kitu kinachohusu uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Wagombea sita wa urais mwaka huu ni pamoja na Mostafa Aqa-Mirsalim ambaye ni waziri wa zamani wa utamaduni na muongozo wa Kiislamu, Mostafa Hashemi-Taba makamu wa rais wa zamani ambaye pia aliwahi mkuwa mkuu wa kamati ya kitaifa ya Olimpiki, Es'haq Jahangiri makamu wa kwanza wa serikali ya sasa, Mohammad-Baqer Qalibaf meya wa mji wa Tehran, Seyyed Ebrahim Raeisi msimamizi wa Haram Takatifu ya Imam Ridha AS na rais wa sasa  Hassan Rouhani ambaye anatetea nafasi yake ili amalize kipindi chake cha pili.
Zoezi la upigaji kura Iran
Uchaguzi wa 12 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya tarehe 19 mwezi ujao wa Mei sambamba na uchaguzi wa tano wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji kote nchini Iran. Wairani wanaoishi nje ya nchi wanaweza kushiriki katika uchaguzi wa rais pekee.

Saturday, April 22, 2017

KOREA KASKAZINI: TUMEJIANDAA KUIKABILI MAREKANI NA HATUTISHIKI NA MELI ZAKE ZA KIVITA

Serikali ya Korea Kaskazini imetangaza utayarifu wake wa kukabiliana na hatua yoyote ya kichokozi ya Marekani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini sambamba na kutangaza habari hiyo imesema kuwa, katika kufuatilia nyendo za Marekani, Pyongyang imejiandaa kukabiliana na chokochoko za Washington. Katika ripoti hiyo, Pyongyang imezungumzia hatua ya hivi karibuni ya Marekani ya kutuma meli zake za kivita katika maji ya Peninsula ya Korea na kuongeza kuwa, Pyongyang haitishiki na jambo hilo.
Kim Jong-un akiwa na makomando wa nchi yake
Kadhalika Korea Kaskazini imesisitiza kuwa, hatua hizo za Marekani kamwe haziiogofyi nchi hiyo na kwamba jeshi lake linasubiri amri ya kukabiliana haraka na Marekani. Marekani ilituma meli zake za kivita katika Peninsula ya Korea baada ya kushtadi mgogoro baina yake na Korea Kaskazini. Hii ni katika hali ambayo China na Korea Kaskazini zimesisitiza mara kadhaa kwamba, uwepo wa majeshi ya Marekani katika eneo, unatishia usalama wa nchi hizo sambamba na kusababisha kuibuka mashindano ya silaha katika eneo. Katika hatua nyingine, serikali ya Pyongyang imeionya China kwamba kuendelea vikwazo vya nchi hiyo dhidi yake, kutaharibu mahusiano ya nchi mbili.
Viongozi wa Uchina na Korea Kaskazini
Taarifa iliyotolewa na Korea Kaskazini imesisitiza kuwa, kuendelea mwenendo huo wa vikwazo vya Uchina ni suala ambalo litakuwa na hatima mbaya katika mahusiano ya nchi hizo. Siku chache zilizopita, Beijing ilitangaza kusimamisha safari za ndege zake kwenda Korea Kaskazini huku ikisema kuwa, hatua hiyo haijatokana na sababu za kisiasa. Kabla ya hapo China ililalamikia hatua ya Pyongyang ya kufyatua kombora la balestiki kuelekea maji ya China na kukitaja kitendo hicho kuwa hatari. China na Korea Kaskazini zinafahamika kwa kuwa na mahusiano ya karibu kwa muda mrefu.

BOKO HARAM LASHAMBULIA KIJIJI NA KUTEKA NYARA WASICHANA HUKO KASKAZINI MWA CAMEROON

Duru za habari nchini Cameroon zimearifu kwamba, kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram limetekeleza shambulio katika kijiji cha Mbreché, kaskazini mwa nchi hiyo na kuteka nyara wasichana kadhaa wenye umri wa miaka kati ya minane hadi 14.
Taarifa iliyotolewa na vyombo vya salama nchini Cameroon imesema kuwa, katika shambulizi hilo, wanachama wa kundi hilo la kigaidi wamesababisha hasara kubwa kwenye nyumba za kijiji hicho kilichoko karibu na mpaka wa pamoja na Nigeria. Hadi sasa hakujatolewa taarifa kamili juu ya kiwango cha hasara iliyosababishwa na hujuma hiyo.
Baada ya kujiri hujuma hizo kijijini hapo Mbreché

Katika shambulizi lililofanywa siku chache zilizopita na kundi hilo la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram dhidi ya mji wa Kolofata, kaskazini mwa Cameroon, karibu watu 10 waliuawa na wengine kadhaa walijeruhiwa. Inafaa kuashiria kuwa, wanachama wa kundi hilo walivamia mji wa Kolofata mwezi Julai mwaka 2014 na tangu wakati huo wameendelea kuwepo mjini hapo. Utekaji nyara wanawake na wasichana kunakofanywa na wanachama wa kundi hilo la kigaidi kunajiri katika hali ambayo, hadi sasa serikali ya Nigeria bado inaendeleza juhudi za kuwakomboa wasichana wa shule ya Chibok waliotekwa nyara mwaka 2014.
Sehemu ya wasichana wanaoshikiliwa na wanachama wa kundi la Boko Haram

Katika fremu hiyo, hivi karibuni jeshi la Nigeria lilitangaza kuwa, jumla ya mateka 1,623 wamekombolewa kutoka mikononi mwa magaidi wa kundi la Boko Haram katika operesheni maalumu iliyofanywa na jeshi katika jimbo la Borno na kwamba katika operesheni hizo magaidi 21 waliangamizwa.

UMOJA WA MATAIFA WATOA TADHARI YA KUTIKEA MAAFA YA NYUKLIA DUNIANI

Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Utafiti wa Utokomezaji Silaha (UNIDIR) imeonya kuwa mivutano inayoendelea kujiri duniani inaweza kusababisha maafa ya nyuklia.
Kwa mujibu wa tovuti ya gazeti la Daily Telegraph linalochapishwa London, Uingereza ripoti kamili iliyotolewa na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Utokomezaji Silaha, inatoa taswira ya kuhuzunisha kuhusu kile kinachotarajiwa kuikumba dunia.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa kutotumiwa silaha za nyuklia tangu iliposhambuliwa kwa mabomu ya atomiki miji ya Hiroshima na Nagasaki hakumaanishi kuwa kuna uwezekano mdogo wa kutokea tena tukio kama hilo.
Kwa mujibu wa taasisi ya utafiti ya Umoja wa Mataifa japokuwa hakukutokea mripuko wa nyuklia wakati wa enzi za Vita Baridi lakini ripoti mbalimbali zilizopokewa kutoka nchi zenye kumiliki silaha za nyuklia zilikuwa zikionyesha kuwa ulitokea uripuaji mara kadhaa karibu na silaha hizo kufikia hadi ya kupigwa vingóra vya hali ya hatari.
Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Utafiti wa Utokomezaji Silaha (UNIDIR) imeonya kuwa kutokana na kuongezeka mifumo ya otomatiki ya uongozaji mitambo ya nyuklia hatari za kutokea miripuko ya silaha hizo imeongezeka.../

WAZIRI WA ELIMU: IRAN INAONGOZA DUNIANI KWA KASI YA MAENDELEO YA KIELIMU

Waziri wa Sayansi, Utafiti na Teknolojia wa Iran amesema, kwa mujibu wa takwimu mpya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaongoza kwa kuwa na kasi kubwa zaidi ya maendeleo ya kielimu duniani.
Muhammad Farhadi ameyasema hayo leo pembeni ya ufunguzi wa shughuli za utendaji wa kituo cha makongamano ya kisayansi cha Chuo Kikuu cha Abu Ali Sinaa kilichoko mkoani Hamedan magharibi mwa Iran.
Amefafanua kuwa, katika mashindano na nchi 25 zenye ustawi wa kuendelea wa kielimu na kisayansi, Iran inongoza kwa kuwa na kasi ya ukuaji wa kielimu wa asilimia 14.
Waziri wa Sayansi, Utafiti na Teknolojia wa Iran ameongeza kuwa Russia na China ndizo zinazofuatia baada ya Iran katika orodha hiyo.
Amesema katika nyanja nyenginezo ikiwemo ya teknolojia pia, nafasi ya Iran imepanda kutoka 113 hadi 78 duniani; na kwa upande wa kieneo na Ulimwengu wa Kiislamu ndiyo inayoshika nafasi ya kwanza.
Mwanasayansi wa Kiirani akiwa katika utafiti
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Sayansi, Utafiti na Teknolojia, anayehusika na masuala ya kimataifa Hussein Salar Aamoli alisema, kiwango cha ushirikiano wa kielimu baina ya vyuo vikuu vya Iran na vituo vya elimu duniani kimeongezeka.
Salar Aamoli aidha ameashiria utekelezwaji wa miradi tisa ya vyuo vikuu vya Iran kwa ushirikiano na vyuo vikuu vya juu duniani itakayogharimu zaidi ya yuro milioni moja  na kueleza kwamba idadi ya miradi ya pamoja ya kielimu baina ya Iran na wahadhiri wa vyuo vikuu vya nje katika mwaka uliopita ilifikia 235.../

ULINZI MKALI COLOGNE WAKATI AfD KIKIKUTANA

Chama cha sera kali za mrengo wa kulia AfD kimekuwa na mkutano wake uliotiwa dosari na mapambano ya kuwania madaraka huku maelfu ya wafuasi wa sera za mrengo wa kushoto wakiandamana kutaka kuuvuruga mkutano huo.

Deutschland Bundesparteitag der AfD in Köln (Reuters/W. Rattay)

Wakati wajumbe wa mkutano huo walipokuwa wakianza kuwasili Jumamosi (22.04.2017) mahala pa mkutano kwenye hoteli ilioko mji wa Golgne magharibi mwa Ujerumani, waandamanaji waliokuwa wakiimba na kupiga mayowe walijaribu kuwazuwiya kupita vizuizi vya usalama na kusababisha mapambano na polisi ambapo poilsi wawili walijeruhiwa.Gari moja la polisi lilitiwa moto.
Waandamanaji 50,000 wanatarajiwa kukusanyika wakati wa mkutano huo wa siku mbili wa chama hicho kinachopinga wahamiaji cha Mbadala kwa Ujerumani huku polisi 4,000 wakimwagwa kuweka amani.
Wakati mkutano huo ukianza kiongozi mwenza wa chama cha AfD Frauke Petry ameshindwa katika jaribio la kutaka uungaji mkono wa wanachama zaidi kwa msimamo wa wastani chini ya msingi wa kutambuwa ukweli kama vile ulivyo wa "Uhalisia wa siasa." kwa nia ya kuzinyamazisha sauti za wale wenye misimamo mikali zaidi katika chama hicho.
Pigo kwa Petry
Proteste gegen Bundesparteitag der AfD (picture alliance/dpa/O.Berg) Maandamano dhidi ya chama cha Afd mjini Cologne.
Gazeti mashuhuri la Bild limeuita uamuzi huo wa wajumbe wa hata kutoijadili hoja hiyo ya Petry mtaalamu wa zamani wa kemia mwenye umri wa miaka 41 ni pigo kwa mama huyo ambaye ni mja mzito akitegemea kupata mtoto wake wa tano.
Akitowa wito wa hamasa wakati akifunguwa mkutano huo,Petry amesema chama hicho cha AfD bado kinaweza kudhamiria kuwa chama kikuu nchini Ujerumani ifikapo uchaguzi mwengine katika kipindi cha miaka minne iwapo kitaregeza kauli zake kali katika ujumbe wake.
Amesema wajumbe inabidi waamuwe "iwapo na vipi chama hicho cha AfD kinaweza kuchagua uhalisia kushika madaraka kwa wapiga kura ifikapo mwaka 2021 ili kwamba hatuiachilii serikali moja kwa moja kwa vyama vikuu vilivyozoeleka.
AfD ambayo hivi sasa inawakilishwa katika majimbo 11 kati ya 16 ya Ujerumani kinakusudia kusaini mpango ambao utafunguwa njia kwa chama hicho kuingia katika bunge la taifa kwa mara ya kwanza katika hisoria yake ya miaka minne.
Umashuhuri washuka
Deutschland Bundesparteitag der AfD in Köln Proteste (Reuters/T. Schmuelgen) Polisi wakibuburushana na waandamanaji Cologne.
Kikiwa kimeasisiwa mwaka 2013 kwa ilani ya kuwa na mashaka na Umoja wa UIaya chama hicho kimetumia kwa faida yake uamuzi wa Kansela Angela Merkel wa kuruhusu kuingia nchini kwa zaidi ya watafuta hifadhi milioni moja tokea mwaka 2015 na kubadili ramani ya kisiasa ya Ujerumani.
Lakini neema zake zimeanza kupunguwa kutokana na kupunguwa kwa wanachama wapya na vyama vyote vikuu vya Ujerumani vikifuta uwezekano wa kushirikiana nacho  iwapo kitavuka kiwango cha asilimia tano kupata uwakilishi wakati wa uchaguzi huo  wa tarehe 24 Septemba.
Uchunguzi wa maoni unaonyesha chama hicho cha AfD kikiwa na asilimia kati ya saba na kumi na moja kikiwa kimeshuka sana kutoka asilimia kumi na tano ilizokuwa imepata mwishoni  tu mwa mwaka jana.Merkel anawania muhula wa nne baada ya kuwa madarakani kwa takriban miaka 12 na chama chake cha kihafidhina hivi sasa kinaongoza katika uchunguzi wa kura za maoni.
Kufuatia malumbano ya wiki kadhaa ya ndani ya chama ,Petry ametowa tangazo la fadhaa kwamba hatowania kuongoza kampeni za Afd mwaka huu.Habari hizo zimekiacha chama hicho kikiyumba na kufunguwa medani ya mzozo kati ya wale wa sera kali za mrengo wa kulia na wale wenye siasa kali zaidi ndani ya chama hicho.
Mpinzani wake mkuu Alexander Gauland mwenye umri wa miaka 76 ambaye amekiasi chama cha CDU cha Merkel amewahimiza wajumbe kuishinda hoja ya mama huyo ya "siasa za uhalisia" kwa kusema kwamba inawagawa wanachama.

Thursday, April 20, 2017

KENYATTA AONYA WANAOVURUGA AMANI

Wagombea watakaozusha ghasia kwenye mchujo wa chama cha Jubilee hawataruhusiwa kuwania viti mbalimbali chamani. Rais Uhuru Kenyatta amesema pia sheria itazingatiwa bila upendelea kwa mtu yeyote.
Rais Uhuru Kenyatta (picture-alliance/dpa/B.v. Jutrczenka)
Ujumbe wa Rais Uhuru Kenyatta unajiri siku nne kabla ya zoezi la mchujo wa chama chake cha Jubilee kuanza. Zoezi hilo lilikuwa linastahili kuanza siku ya Ijumaa lakini likaahirishwa na hapajatolewa sababu za hatua hiyo. Akionekana mwenye ghadhabu, Rais Kenyatta alisisitiza kuwa hakuna wawaniaji ambao wameteuliwa ama kupendekezwa na chama chake. Aliwahakikishia wananchi kuwa wao ndio wenye uwezo wa kuchagua viongozi wao. Rais alikuwa na onyo kwa wanachama ambao wana nia ya kuzusha ghasia kwenye mchujo huo na wakati wa uchaguzi mkuu Agosti tarehe nane.
Ghasia na madai ya wizi wa kura kwenye mchujo wala hayajakisaza chama cha upinzani cha ODM. Zoezi la mchujo wa chama cha ODM ulioanza juma lililopita, umesababisha baadhi ya wanachama kuhamia vyama vingine kwa madai ya kubaguliwa.
Huku joto la kisiasa likizidi kuongezeka nchini, Muungano wa Upinzani NASA hatimaye umeondoa taharuki kwa wafuasi wake kwa kutangaza kwamba mgombea wa kiti cha urais kwa tikiti ya muungano atatajwa kwenye mkutano mkubwa wa siasa tarehe 27 Aprili. Kwenye Mkutano uliotumiwa kumkaribisha kiongozi wa chama cha Mashinani Gavana wa Bomet Isaac Ruto kuwa kinara mwenza wa muungano wa NASA viongozi wa upinzani wameitaja siku ya leo kuwa siku ya kihistoria katika siasa za Kenya.
Muungano wa upinzani  umezindua mkakati wake wa kushinda uchaguzi mkuu ujao kwenye hafla hafla ya leo. Kalonzo Musyoka ni mmoja wa vinara anayetarajia kutajwa kupeperusha bendera ya NASA
Viongozi hao wameutaja muungano wa NASA kuwa muungano wa Wakenya wote. Muungano wa NASA sasa unajumuisha vyama vitano vya ODM, Wiper Democratic Movement, Ford Kenya, Amani National Congress na Chama cha Mashinani.
Viongozi wa Muungano wa upinzani NASA: Musalia Mudavadi, Raila Odinga, Isaac Ruto, Kalonzo Musyoka, and Moses Wetangula in Nairobi (Reuters/T. Mukoya) Viongozi wa Muungano wa upinzani NASA: Musalia Mudavadi, Raila Odinga, Isaac Ruto, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula
Siku 109 zimesalia uchaguzi mkuu kufanyika na uteuzi wa wagombea urais unatakiwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi Mei. Kura za Mchujo za vyama tanzu vya muungano wa NASA zilianza wiki iliyopita na kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Uchaguzi kura za mchujo zinapasa kumalizika tarehe 27 Aprili. 
Kuingia kwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto katika Muungano wa NASA kumeanza kuleta tumbojoto kwa chama kinachotawala cha Julilee huku taswira ya siasa za Mwaka 2002 ikijitokeza wakati ambapo chama tawala cha KANU kilibanduliwa mamlakani na muungano wa upinzani wa National Rainbow Coalition NARC.

UAMUZI WA MAHAKAMA KUU INDIA DHIDI YA VIONGOZI WA CHAMA TAWALA, KUBOMOLEWA MSIKITI WA BABRI

Mahakama Kuu ya India imetangaza kuwa, viongozi watatu wa ngazi za juu wa chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) wanapaswa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuharibu Msikiti wa Babri na mauaji ya Waislamu.
Watu hao watatu wanatuhumiwa kwamba, waliwachochea Wahindu wenye misimamo mikali kuharibu Msikiti wa Babri katika mji wa Ayodhya, jimbo la Uttar Pradesh, kaskazini mwa India tarehe 6 Disemba 1992, suala ambalo lilizusha hitilafu na machafuko makubwa ya kikaumu na kusababisha mauaji ya maelfu ya watu. Wahindu wenye misimamo mikali waliharibu msikiti huo kwa lengo la kujenga hekalu la Ram mahala pale.
Majaji wa Mahakama Kuu ya India wamesema, Uma Bharti, waziri wa maji, L K Advani, Naibu Waziri Mkuu wa zamani pamoja na mwanasiasa mashuhuri M M Joshi, wote hao wa chama tawala BJP wanapaswa kufunguliwa mashtaka ya jinai na kula njama, kwa kuwachochea vijana wenye misimamo mikali wa Kihindu kuubomoa Msikiti wa Babri uliojengwa karne ya 16.
Machafuko yuliyosababishwa na kubomolewa msikiti huo na hitilafu zilizotokea baina ya Waislamu na Wahindu vimesababisha mauaji ya Waislamu zaidi ya elfu mbili na kujeruhiwa wengine wengi.  
Awali mahakama hiyo ilitosheka kwa kumkosoa aliyekuwa mkuu wa chama cha Bharatiya Janata, Subramanian Swamy kwa kufanya njama za kuboa Msikiti wa kihistoria wa Babri na kutaka kujenga maabadi ya Wahindu mahala pale.  Mahakama Kuu ya India ilisisitiza kuwa, chama cha Bharatiya Janata hakiwezi kufikia malengo yake katika jimbo la Uttar Pradesh kwa kutumia mabavu. 
Wahindu wakibomoa Msikiti wa Babri
Rai ya sasa ya Mahakama Kuu ya India inayotaka kupandishwa kizimbani viongozi wa ngazi za juu wa chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) kwa kuhusuka na kuharibiwa Msikiti wa Babri na mauaji ya maelfu ya Waislamu inaweza kutambuliwa kuwa ni mpambano baina ya serikali na Idara ya Mahakama ya nchi hiyo. Chama cha Bharatiya Janata ambacho kilishika hatamu za uongozi nchini India baada ya kushinda uchaguzi wa Bunge mwaka 2014 - kama ilivyokuwa imetabiriwa- kilizidisha mashinikizo na ukandamizaji dhidi ya Waislamu katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Katika mkondo huo huo, kwa wiki kadhaa sasa chama hicho kimekuwa kikishinikiza Mahakama Kuu ya India kwa shabaha ya kuilazimisha itoe hukumu kwa maslahi ya viongozi wake. Hata hivyo hukumu ya mahakama hiyo imekwenda kinyume na matakwa yake.
Waislamu wa India wana wasiwasi mkubwa kuhusu utendaji wa chombo hicho cha sheria na uwezo wake wa kulinda msingi wa kutopendelea upande wowote katika kesi muhimu sana baina ya Wahindu na Waislamu. Vilevile duru mbalimbali za India zinasema kuwa, Wahindu wenye misimamo mikali wangali wanashikilia misimamo yao kuhusu ujenzi wa maabadi ya Ram sehemu ya Msikiti wa kihistoria wa Babri licha ya uamuzi wa mahakama hiyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mpango wa kujenga maabadi hiyo sehemu ya Msikti wa Babri umekuwa ukitajwa sana katika ahadi za chama tawala cha Bharatiya Janata katika kampeni za uchaguzi. 
Msikiti wa Kihistoria wa Babri
Wahindu wenye misimamo mikali wanadai kuwa, kabla ya kujengwa Msikiti wa Babri kulikuwepo hekalu au maabadi ya Ram mahala hapo, madai ambayo hayana mashiko ya kihistoria.
Hivi sasa baada ya Mahakama Kuu ya India kutoa hukumu ya kupandishwa kizimbani viongozi wakuu watatu wa chama tawala kwa tuhuma za kuhusika na ubomoaji wa Msikiti wa Babri na mauaji ya maelfu ya Waislamu wa India, kuna wasiwasi kwamba chama cha Bharatiya Janata Party (BJP) kitatumia njia mbalimbali za vishawishi na vitisho kwa ajili ya kumshinikiza jaji anayeshughulikia faili hilo ili atoa hukumu dhidi yua Waislamu. Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema itakuwa vigumu sana kwa chama hicho kufikia malengo yake baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu ya India ya kupandishwa kizimbani viongozi hao watatu wa chama cha BJP.

UN YAIONYA SAUDIA DHIDI YA KUSHAMBULIA KWA MABOMU BANDARI YA YEMEN

Umoja wa Mataifa umeutaka muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia usishambulie kwa mabomu bandari ya kistaratejia ya Yemen.
Jamie McGoldrick, Mshirikishi wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen ametahadharisha kuwa, iwapo Bandari ya al-Hudaydah iliyopo katika Bahari Nyekundu itashambuliwa kwa mabomu na Saudia, basi yumkini idadi kubwa ya raia wa Yemen wakatumbukia katika mgogoro mkubwa wa kibinadamu.
Katika kikao na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Jordan, Amman hii leo, afisa huyo wa UN amefafanua kuwa: "Bandari ya al-Hudayda ni kituo nyeti kwa raia wa Yemen, hatuoni iwapo kuna haja ya eneo hilo la kistaratajia kushambuliwa na muungano wa kijeshi wa Saudia. Muungano huo unafaa kulipa uzito na umuhimu suala la kibinadamu unapokuwa katika kampeni na operesheni zake. Iwapo bandari hiyo itashambuliwa, sisi pamoja na asasi zingine za kufikisha misaada ya kibinadamu hatutaweza kufikisha chakula, dawa na mahitaji mengine ya msingi kwa raia wa Yemen."
Jamie McGoldrick, Mshirikishi wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Bandari ya al-Hudaydah ndiyo bandari muhimu zaidi ya Yemen ambapo karibu asilimia 80 ya shehena za chakula na dawa zinazofikishwa kwa wananchi, hupitishwa kupitia bandari hiyo.
Hii ni katika hali ambayo, wananchi wa Yemen hapo jana walikusanyika mbele ya ofisi ya Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa nchi hiyo Sana'a kulaani kufungwa Bandari ya al-Hudaydah sambamba na kukosoa mauaji ya kikatili dhidi ya watu wa taifa hilo, yanayofanywa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, tangu Machi mwaka 2015.

WAZIRI MKUU WA KOREA KUSINI, ATOA AMRI KULITAKA JESHI LA NCHI HIYO LIJIWEKE TAYARI KUKABILIANA NA PYONGYANGA

Waziri Mkuu wa Korea Kusini anayekaimu nafasi ya rais, amelitaka jeshi na vikosi vya nchi hiyo kujiweka tayari kutokana na kile alichokisema kuwa ni kushadidi kwa harakati za kijeshi za Pyongyang.
Hwang Kyo-ahn ameyasema hayo Alkhamis ya leo katika kikao cha Baraza la Mawaziri la Korea Kusini kufuatia kuenea kwa habari zinazohusiana na uwezekano wa Korea Kaskazini kufanya jaribio la sita la silaha ya nyuklia hivi karibuni. Kufuatia hali hiyo Hwang Kyo-ahn ametoa amri kwa jeshi la nchi yake kujiweka tayari kwa ajili ya kukabiliana na hatua yoyote ya kijeshi na harakati za Korea Kaskazini.
Jeshi la Korea Kusini
Kadhalika Waziri Mkuu wa Korea Kusini amelitaka jeshi la nchi hiyo kufuatilia kwa karibu mabadiliko na harakati zote za Pyongyang. Mgogoro katika eneo la Peninsula ya Korea ulishadidi baada ya Rais Donald Trum wa Marekani na makamu wake wa rais, Mike Pence kutoa matamshi ya vitisho kuilenga Pyongyang, vitisho ambavyo vilienda sambamba na kutumwa kwa meli tatu za kijeshi zinazobeba ndege za kivita karibu na pwani ya Korea Kaskazini.
Hwang Kyo-ahn, Waziri Mkuu wa Korea Kusini
Hatua hiyo ya Marekani ilitajwa na Korea Kaskazini kuwa, ya kichokozi na inayohatarisha usalama na amani ya peninsula hiyo. Mbali na hayo ni kwamba Korea Kaskazini imesisitiza mara kadhaa kwamba, madamu Marekani na waitifaki wake zitaendelea kutishia usalama wake, basi nayo itazidi kuimarisha uwezo wake wa kijeshi kukabiliana na chokochoko za adui.

SERA ZA MAREKANI KATIKA MASHARIKI YA KATI NI KUENEZA HOFU NA VITISHO DHIDI YA IRAN

James Mattis, Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Riyadh Saudi Arabia baada ya kukutana na mwenyeji wake kwamba, timu ya Rais Donald Trump inaandaa mikakati ya kuidhibiti na kuikwamisha Iran kupitia njia ya kuimarisha uratibu na Saudi Arabia na waitifaki wengine wa Marekani.
Jenerali Mattis amedai kwamba, Iran imekuwa ikivuruga amani na uthabiti katika Mashariki ya Kati hivyo kuna haja ya kuzuia satwa na ushawishi wa taifa hili ili ipatikane njia ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen kupitia mazungumzo kwa upataishi wa Umoja wa Mataifa. Kwa hakika matamshi haya ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani si jambo jipya. Viongozi wa Marekani bila kujali ni wa chama cha Democrats au cha Repulican wamekuwa wakitumia lugha hizo za vitisho tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipopata ushindi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ulipokuja na kukata mikono ya Marekani hapa nchini.
Kwa muktadha huo, uadui wa madola yanayotumia mabavu ulimwenguni hususan Marekani kwa taifa taifa la Iran ni jambo lisilo na shaka hata kidogo. Hii inatokana na kuwa, uadui wao uliendelea kushuhudiwa katika kipindi chote ambacho serikali mbalimbali na zenye utashi tofauti zilipoingia madarakani nchini Marekani.
Safari ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani nchini Saudia
Pamoja na hayo, inaonekana kuwa, lengo la viongozi wa Marekani katika kipindi hiki la kutumia lugha hizi za vitisho ni kutoa ishara ya kuweko mabadiliko ya kimsingi katika sera za Marekani katika kukabiliana na Iran. Hivi sasa siasa za Marekani dhidi ya Iran kwa namna fulani zinaonekana kuipa Saudi Arabia baadhi ya majukumu. Kiasi kwamba, akitoa natija jumla ya mazungumzo yake huko Riyadh, Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema kuwa, Washington imefikia natija na Riyadh kuhusiana na jambo hilo.  Mattis amesema: Kwa hakika sisi tunapaswa kufanya kitu na kuimarisha muqawama wa Saudia mbele ya miamala ya Iran. Kama ambavyo tunafanya kazi tukiwa washirika, tunapaswa kuchukua hatua ambazo zitakufanyeni nyinyi viongozi wa Saudia na jeshi lenu muwe na utendaji mzuri zaidi.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani ameyatoa matamshi na madai haya mjini Riyadh katika hali ambayo, kila mahala ambako kuna matatizo katika Mashariki ya Kati na popote pale ambako kunafukuta moto wa vita kuanzia Asia mpaka Ulaya na Afrika mpaka Amerika ya Latini basi kunashuhudiwa mkono wa Marekani na waitifaki wake.
Aidha stratejia ya Marekani katika Mashariki ya Kati inaeleweka wazi. Stratejia hiyo haina tofauti sana na duru zilizopita za uongozi nchini Marekani kabla ya Rais wa sasa wa nchi hiyo Donald Trump. Marekani ingali inawategemea watawala wa nchi za Kiarabu wa eneo hili katika uuzaji silaha zake kwa kisingizio cha kukabilia na vitisho ambavyo Marekani yenyewe imevipandikiza. Utawala wa Aal Saud nao ukitumia mbinu ya kale umekuwa ukinunua silaha nyingi kwa kutumia fedha za mafuta ikiwa na lengo la kununua muda zaidi kwa utawala wake unaotetereka na kulegalega.
Katika uwanja huo, himaya ya Marekani kwa uvamizi wa Saudia katika vita vya Yemen ni jambo muhimu, kwani kivitendo siasa za chokochoko za Saudia katika vita hivyo na vile vile katika kuyaunga mkono makundi ya kigaidi huko Syria na Iraq zimeshindwa na kugonga mwamba. Njia pekee iliyobakia kwa Aal Saud ni kutoa upendeleo kwa Marekani usio na masharti yoyote. Hata hivyo inawezekana kuyatazama matamshi haya ya Mattis katika engo nyingine. Waziri huyo wa Ulinzi wa Marekani anasema kuwa, Washington na washirika wake wanataka kuikwamisha Iran.
Matamshi haya kwa namna fulani yanaweza kuwa yana lengo la kupima radiamali ya Iran mkabala na lugha za vitisho za Marekani. Kwani viongozi wa White House wanatambua vyema msimamo wa Iran kuhusiana na jambo hilo. 
Ayatullah Ali Khamenei, alipokuna na makamanda wa jeshi kwa mnasaba wa Siku ya Jeshi nchini Iran
Akihutubia Jumatano ya jana kwa mnasaba wa Siku ya Jeshi hapa nchini, wakati alipokutana na kundi la makamanda wa jeshi, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kuwa, moja ya nukta imara za mfumo wa Kiislamu hapa nchini ni kuwa na moyo wa kishujaa na kusimama kwake kidete mbele ya makeke na upayukaji wa madola ya kibeberu. Aidha alisema kuwa, moja ya hila na ujanja unaotumiwa na madola vamizi ni kuyatisha mataifa na tawala za nchi nyingine na kutumia woga wa mataifa hayo kufanikisha malengo haramu ya madola hayo ya kibeberu na ndio maana mara zote utayaona madola hayo ya kiistikbari yakipenda kujigamba na kujionesha kuwa yana nguvu kubwa.
Kiongozi Muadhamu amesema bayana kwamba, kama Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran lingeyaogopa madola ya kibeberu na kulegeza kamba mbele yao, basi leo hii kusingekuwa na athari yoyote ile ya Iran na Uirani. Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, adui yeyote yule, awe Mmarekani au mkubwa kuliko Marekani hawezi kufanya lolote mbele ya mfumo wa utawala unaotegemea vizuri nguvu za wananchi wake na ambao umesimama kidete mbele ya adui.

Tuesday, April 18, 2017

JESHI LA YEMEN LAENDELEA KUPATA MAFANIKIO DHIDI YA VIBARAKAWA SAUDIA

Askari wa serikali ya Yemen kwa kushirikiana na Harakati ya Wananchi ya Answarullah limeendelea kupata mafanikio katika operesheni kadhaa lilizozifanya katika mikoa ya Lahij, Dhale na Taiz na kufanikiwa kuwaangamiza askari wengi vibaraka wa Saudia sambamba na kuwatia hasara kubwa.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la Yemen imesema kuwa, askari wa serikali na harakati hiyo ya Answarullah, wameweza kuwazuia askari vamizi wa Saudia na waungaji mkono wao kuelekea mji wa Kirsh mkoa wa Lahij, kusini mwa Yemen ambapo kumejiri mapigano makali yaliyowafanya askari wa Saudia kurudi nyuma na kukimbia.
Baadhi ya askari wa Saudia walioangamizwa na jeshi la Yemen
Hii ni katika hali ambayo kikosi cha mizinga cha jeshi na harakati ya Answarullah kilichopewa jina la 'al-Swaderain' kimelilenga eneo la 'Maris' la mkoa wa Dhale, kusini mwa nchi ambapo kumewekwa kambi ya jeshi la askari wa Saudia na kufanikiwa kuangamiza baadhi yao. Kadhalika magari kadhaa ya kijeshi ya Saudia yaliyokuwa yamewabeba askari wa nchi hiyo vamizi wameangamizwa huko magharibi mwa mkoa wa Taiz. Makumi ya askari wa Saudia na vibaraka wake wameangamizwa katika siku za hivi karibuni katika maeneo tofauti ndani na nje ya Yemen na hivyo kuitia hasara kubwa Saudi Arabia na washirika wake.
Baadhi ya magari na vifaru vya jeshi la Saudia vilivyoharibiwa na jeshi la Yemen
Wakati huo huo duru za kuaminika zimeripoti kuibuka mapigano makali baina ya askari wanaomuunga mkono Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu na kutoroka nchi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mapigano hayo yametokea huko mkoa wa Aden, baada ya kundi moja kati ya askari hao kutaka kudhibiti kituo cha upekuzi mkoani hapo.

KAMPALA KUWASTAAFISHA WAKONGWE UPDF WAKIWEMO MAJENERALI


Rais Yoweri Museveni
Baada ya kutumikia jeshi la Uganda (UPDF) kwa zaidi ya miaka 36 wanajeshi wote wakongwe wanastaafishwa na nafasi zao kuchukuliwa na vijana.
Hata hivyo serikali haijatoa sababu maalum ya uamuzi huo wa kuwastaafisha wanajeshi hao ambao wanajulikana kwa ushujaa wao wa kupigana vita vilivyomwezesha Rais Yoweri Museveni kuingia madarakani mwaka 1986.

Lakini kwa mujibu wa msemaji wa Jeshi hilo Brigedia Richard Karemire hiyo ni hatua ya kawaida.
“Tutakuwa na uwezo wa kuwastaafisha zaidi ya maafisa 2000, wakiwemo majenerali,” amesema msemaji huyo.

Ameongeza kusema kuwa: “Tunalenga kuwastaafisha wanajeshi zaidi ya 2000 wakiwemo majenerali na zaidi ya wanajeshi wengine 10,000 watastaafu.”
“Hii ni sehemu ya zoezi ambalo limekuwa likiendelea kwa miaka mingi. Tunalenga kuimarisha utendaji kazi wa jeshi letu, kwani huko nyuma tayari tumewastaafisha baadhi yao,” amesema Brig Karemire.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa baadhi ya wanajeshi hawa wamekuwa wakitaka kuondoka jeshini bila ya mafanikio.

Ametoa mfano wa Generali David Tinyefuza ambaye tayari amefungua kesi ilioendelea katika mahakama nchini Uganda kwa muda wa miaka 8 akidai haki yake ya kustaafu bila ya mafanikio.

Kwa upande mwengine kumekuwa na baadhi ya wachambuzi ambao wamekuwa na maoni kuwa kulazimishwa kwa wanajeshi hao kubakia jeshini kunatokana na hofu kwamba wakiruhusiwa kustaafu wanaweza kujiingiza katika siasa na kuuporomosha utawala wa Museveni.

Mmoja wa wakongwe hao Jeshini Brigedia Generali Kasirye Gwanga anasema: “ Ni hatua nzuri waruhusu vijana wachukue usukani. Nina umri wa miaka 65 sasa, nafanya nini katika jeshi, siwezi kukimbia na kushiriki katika vita.”

Wanajeshi hao wakongwe walishiriki katika vita vya mwaka 1980 na 1985 pamoja na Rais Museveni dhidi ya utawala wake Apolo Milton Obote na Jenerali Tito Okello na kufanikiwa kumwezesha Museveni kuingia madarakani mwaka 1986 kwa mtutu wa bunduki.

KIPLAGAT, KIRUI WASHINDA MBIO ZA MARATHON BOSTON


Edna Kiplagat na Geoffrey Kirui baada ya ushindi wao huko Boston.
Mkimbiaji maarufu Edna Kiplagat kutoka Kenya ametwaa ushindi (mbio za wanawake) kwa kuongoza mashindano ya marathon ya 121 huko Boston, Marekani. Kwa upande wake Geoffrey Kirui ambaye pia ni Mkenya ameshinda mbio za upande wa wanaume.
Kwa mujibu wa mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA Kiplagat ambaye ni afisa wa jeshi la polisi la Kenya alianza mbio hizo kwa kuwaacha wapinzani wake nyuma sana.

Hata hivyo wakati anaelekea katika milima ya Newton akaongeza kasi kufikia ushindi katika muda (usio rasmi) wa masaa 2, dakika 21, sekunde 53 katika mbio hizo za 121, siku ya Jumatatu April 17, 2017.

Ni mara ya kwanza Kiplagat, ambaye ni mshindi wa kimataifa kwa mara mbili ameshiriki katika mbio hizo za Boston.
Mshindi huyu amewahi kushinda London, New York City na Los Angeles.

Kwa upande wa mbio za wanaume, Mkenya Geoffrey Kirui ameshinda mbio za Marathon katika mashindano haya kwa mara ya kwanza.

Kirui alimshinda mpinzani wake Galen Rupp wa Marekani na kunyakua ubingwa huo wa mbio hizo za 121 katika muda usio rasmi wa masaa 2, dakika 9 na sekunde 36. Hata hivyo alikuwa mshindi mwaka jana katika mbio za marathon za Amsterdam na watatu katika mbio za Rotterdam. Rupp alimaliza mbio hizo kwa muda usio rasmi wa masaa 2, dakika 9 na sekunde 58.

Katika mbio hizo za wanawake Chelimo wa Bahrain alichukua nafasi ya pili, akiwa nyuma kwa dakika 59 na Jordan Hasay wa Marekani ametwaa nafasi ya tatu katika uzinduzi wa mashindano hayo ya Marathon.

Desi Linden, ambaye alitwaa ushindi wa pili huko Boston kwa tofauti ya dakika mbili mwaka 2011, alimaliza akiwa mshindi wanne—kwa mara ya kwanza tangu 1991ambapo wanawake wawili wa Kimarekani kumaliza katika wanne bora.

PENCE AITAKA KOREA KASKAZINI KUTOIJARIBU MAREKANI


Makamu wa Rais Mike Pence akiangalia upande wa Korea Kaskazini wakati wa ziara yake huko Seoul.
Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence ametoa onyo kali kwa Korea Kaskazini April 17, 2017, akirejea kutaja mashambulizi ya angani yaliofanywa hivi karibuni na Marekani huko Syria na Afghanistan.

Katika onyo hilo amesema Rais Donald Trump atatumia nguvu za kijeshi ikiwa atahitajika kufanya hivyo katika kukabiliana na serikali ya Kim Jong Un ambayo imeendelea kukuza tishio la kinyuklia.

“Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita dunia imeshuhudia nguvu na maamuzi ya rais wetu mpya akichukua hatua huko Syria na Afghanistan. Korea Kaskazini itafanya vizuri iwapo haitojaribu kupingana na maamuzi ya rais,” Makamu wa Rais Pence amesema.
Makamu wa rais huyo anatembelea Korea Kusini katika mwanzo wa ziara yake ya mataifa manne ya Asia kusisitiza nia ya Marekani thabiti kwa kuendelea kuwasaidia washirika wake katika ongezeko la hali tete inayoendelea kujitokeza katika eneo hilo na kujenga mshikamano wa kimataifa kwa kuongeza shinikizo kwa serikali ya Kim Jong Un kukomesha programu zake zakutengeneza silaha za nyuklia na makombora ya ballistiki.


Umoja usiotetereka

Wakati wa mkutano wa waandishi mjini Seoul Jumatatu alioufanya pamoja na kaimu Rais wa Korea Kusini Hwang Kyoahn, Pence amesisitiza msaada wa Marekani “usiotetereka” katika kulinda mshirika wake wa muda mrefu na kushirikiana naye katika maamuzi yote yanayohusiana na usalama wa eneo hilo.

“Tutaendelea kushauriana kwa karibu na Korea Kusini na uongozi wenu tunapoendelea kufanya maamuzi,” alisema.

Wengi huko Korea Kusini wameendelea kuwa na wasiwasi kwamba Marekani inaweza kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini peke yake kitendo ambacho kinaweza kuliingiza eneo hilo katika vita.


Katika maoni yake kaimu rais wa Korea Kusini amesisitiza ulazima wa kuongeza vikwazo vya uchumi dhidi ya Korea na hakuzungumzia suala la kuchukua hatua za kijeshi.

“Tunakubaliana katika uelewa wa uzito na umuhimu wa tishio la nyuklia na makombora ya Korea Kaskazini, na kuongeza maradufu juhudi zetu kubadilisha mikakati iliowekwa na Korea Kaskazini kwa kuendelea kuongeza shinikizo la mtandao wa kimataifa juu ya Korea Kaskazini,” amesema Hwang.

Mshauri wa Usalama wa Taifa Marekani
Kadhalika April 16, 2017 Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani H.R. McMaster alionekana kuweka kando tishio lililokuwepo juu ya uwezekano wa Majeshi ya Marekani kufanya mashambulizi dhidi ya Korea Kaskazini, angalau kwa wakati huu.

“Ni wakati mwafaka kwetu kuchukua hatua zote zinazowezekana, bila ya hatua za kijeshi, katika kujaribu kulitatua suala hili kwa njia ya amani,” amesema kwenye kipindi cha “This Week” cha shirika la habari la ABC. “Tunafanya kazi na washirika wetu na wadau wengine na uongozi wa China kuandaa njia mbalimbali mbadala za kukabiliana na suala hili.”

Uongozi wa Trump umeripotiwa kuwa umejikita katika kuweka vikwazo madhubuti vya kiuchumi, kukiwa na uwezekano wa kuhusisha kuzuia mafuta kuingia nchi hiyo, kupiga marufuku shirika la ndege la nchi hiyo kimataifa, kukamata meli za mizigo na kuziadhibu Benki za China zinazofanya biashara na Pyongyang.

Pongezi za Trump kwa China
Makamu wa rais amerudia kueleza pongezi za Trump kwa hatua zaidi ilizochukua China katika ongezeko la vikwazo vya uchumi ukiwemo uamuzi wa kuzirejesha meli za mizigo zilizokuwa zimebeba makaa ya mawe, moja ya biashara ya nje muhimu kwa Korea Kaskazini na pia kufuta safari za ndege kwenda Pyongyang.

Wakati China ikiendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika kuweka shinikizo la vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini ilikufikia mazungumzo ya kuondoa silaha za nyuklia, imekuwa ikisita kuchukua hatua kali ambazo zinaweza kusababisha kukosekana amani katika nchi za jirani na kuongeza nguvu za kijeshi za Marekani katika eneo hilo.

RUSSIA NA CHINA ZATUMA MELI ZAO ZA KIJESHI KARIBU NA ENEO ZILIPO MELI ZA US, KOREA

Russia na China zimetuma meli zao za kijeshi katika eneo zilipo meli za Marekani karibu na pwani ya Korea Kaskazini kwa lengo la kufuatilia nyendo za meli za Marekani katika eneo hilo.
Gazeti la Japan la Yomiuri Shimbun limeandika kuwa, serikali ya Uchina imeomba msaada kwa Russia kwa ajili ya kuzuia kutokea mgogoro wa kivita huko Korea Kaskazini. Kwa mujibu wa gazeti hilo, Beijinga na Moscow zimeamua kutuma meli zao za kivita kwa ajili ya kukusanya taarifa za kiintelijensia kutoka meli za Marekani, ili kuzuia kuongezeka kwa mgogoro baina ya Marekani na Korea Kaskazini.
Moja ya meli za kivita za Marekani zilizotumwa Korea
Wakati huo huo gazeti la Japan News, linaloandikwa kwa lugha ya Kingereza limesema kuwa, meli hizo za Uchina na Russia zitakuwa na kazi ya kutoa indhari na kupiga doria sambamba na kuzidisha ulinzi wa kujitawala anga na bahari ya eneo hilo. Awali Rais Donald Trump wa Marekani alitoa amri ya kutumwa meli tatu za kubeba ndege za kivita za 'USS Carl Vinson' 'Ronald Reagan' na 'USS Nimitz' kwenda pwani ya Korea, hatua ambayo ilitajwa na serikali ya Pyongyang kuwa ni ya kichokozi.
Moja ya meli za kivita za Uchina
Katika hatua nyingine serikali ya Korea Kusini imesisitiza azma yake ya kuweka ngao ya makombora ya Marekani aina ya THAAD katika ardhi yake na kwamba hakuna mabadiliko yoyote katika suala hilo. Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo ilisema Jumatatu ya jana katika kujibu baadhi ya tetesi zilizoashiria kuwa Seoul na Washington zimeamua kusitisha zoezi la uwekaji ngao hiyo,  kwamba habari hizo hazina ukweli wowote.

UPINZANI CONGO WATAKA UCHUNGUZI KUHUSU PASIPOTI

Viongozi wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamewataka maafisa wa serikali kuchunguza ripoti ya shirika la habari la Reuters iliyochapishwa wiki iliyopita, ikisema sehemu kubwa ya fedha zinazolipwa na raia kwa ajili ya Pasipoti zinakwenda nje ya nchi. Ripoti hiyo kuhusu mkata uliosainiwa mwaka 2015 baina ya serikali ya Kongo na kampuni ya kibelgiji iitwayo Semlex kutengeneza paspoti za kisasa, inaonyesha kuwa gharama ya paspoti moja ni dola 185 za kimarekani, na kwamba nyingi kati ya fedha hizo huenda katika kampuni ya Semlex na nyingine iliyosajiliwa katika Umoja wa Falme za Kiarabu ijulikanayo kama LRPS. Aidha, ripoti hiyo inamnukuu mtu mwenye ujuzi kuhusu kampuni la LRPS, akisema kampuni hiyo ni mali ya mtu mwenye uhusiano wa karibu na Rais Joseph Kabila, aitwaye Makie Makolo Wagoi. Serikali ya Kongo na Kampuni ya Semlex hawajatoa majibu yoyote kwa taarifa hizo.

KOREA KASKAZINI YALAANI MAREKANI KWA 'KUHUJUMU ' AMANI

Balozi wa Korea Kaskazini ameituhumu Marekani kuhujumu amani na utengamano katika Rasi ya Korea wakati mvutano ukishamiri katika eneo hilo. Akizungumza katika Umoja wa Mataifa Balozi Kim In-ryong alisisitiza kuwa Korea Kaskazini iko tayari kwa vita kamili na Marekani. Alisema mwenendo wa Marekani wa kutumia ubabe kuzivamia nchi huru na baadaye kudai inachangia katika kulinda amani ya dunia ni kukosa uwajibikaji. Korea Kaskazini ambayo hujulikana pia kama Jamhuri wa Kidemokrasia ya Watu wa Korea ilizidisha mvutano wa kikanda kwa kufanya jaribio jingine la kurusha kombora ambalo lilishindwa Jumapili. Wanadiplomasia kadhaa wa nchi hiyo wamesema nchi yao itaendelea kufanya majaribio mengine kila wiki, kila mwezi na kila mwaka.

UPINZANI WATAKA KUFUTWA KWA MATOKEO UTURUKI

Chama kikuu cha upizani Uturuki kimeitaka tume ya uchaguzi kufuta matokeo ya kura maoni ambayo yamempa madaraka mapya makubwa kabisa rais wa taifa hilo kutokana na ukiukaji mkubwa sana wa taratibu za kupiga kura.
Türkei Referendum | (picture alliance/AP Photo/L. Pitarakis)
Chama kikuu cha upizani nchini Uturuki kimeitaka tume ya uchaguzi kufuta matokeo ya kura maoni ya kihistoria nchini humo ambayo imempa madaraka mapya makubwa kabisa rais wa taifa hilo kutokana na ukiukaji mkubwa sana wa taratibu za kupiga kura.
Ujumbe wa kimataifa wa waangalizi ambao umeangalia kura hiyo ya maoni pia umegunduwa kuwepo kwa ukiukaji wa taratibu za kupiga kura kwa kusema upigaji kura huo hapo Jumapili ulikuwa haukukidhi viwango vya kimataifa.Hususan umekosowa uamuzi wa tume ya uchaguzi ya Uturuki kuzikubali kura ambazo zilikuwa hazina mihuri rasmi jambo mbalo imesema limedhoofisha usalama dhidi ya udanganyifu.
Tume hiyo ya uchaguzi ya Uturuki imethibitisha ushindi wa kura ya ndio katika kura hiyo ya maoni na kusema matokeo ya mwisho yataamuliwa katika kipindi cha siku 11 hadi siku 12 hivi.Shirika la habari la taifa Anadolu limesema kura za "ndio"  zilikuwa asilimia 51.4 wakati zile za "hapana" zilikuwa asilimia 48.6 .
Tafauti hiyo ya kura itaimarisha hatamu ya Erdogan madarakani nchini Uturuki kwa muongo mzima na inatazamiwa kuwa na athari kubwa kwa mustakabali wa kisiasa wa muda mrefu wa nchi hiyo na mahusiano yake ya kimataifa. Wapinzani wa mabadiliko hayo ya katiba hoja yao ilikuwa mageuzi hayo yanampa madaraka makubwa mno mtu ambaye amekuwa akizidi kuonyesha tabia za udikteta.
Alilazimika kupambana na mataifa yenye nguvu
Türkei Referendum Recep Tayyip Erdogan (picture alliance/AP Photo/L. Pitarakis) Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki.
Howard Eissenstat profesa mshiriki wa historia ya Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha St.Lawrence huko Canton,New York amesema "anatuhumu matokeo hayo ni finyu kuliko vile alivyokuwa ametegemea Erdogan".Ameongeza kusema " Erdogan aliwahi kutawala kwa ushindi wa kura chache hapo kabla na kwamba haoni ushindi wa kura chache kuwa ni kitu kengine ziada ya mamlaka.Msimamo wake emekuwa kutoujumuisha upinzani bali kuutokomeza".
Hapo Jumatatu Erdogan amewashambulia wakosoaji wake wa ndani na nje ya nchi kwa kusema "amelazimika kupambana na mataifa yenye nguvu duniani ambayo yalipinga kura ya ndio katika kura hiyo ya maoni ya kumuongezea madaraka."
Akihutubia wafuasi wake katika uwanja wa ndege wa Ankara hapo Jumatatu alipokuwa amewasili kutoka Istanbul amesema alikuwa "ameshambuliwa na mataifa yenye " mawazo "ya vita vya kidini dhidi ya Uislamu."
Haiko wazi iwapo alikukuwa akiyakusudia mataifa ya Ulaya yakiwemo Ujerumani na Uholanzi ambayo yaliwazuwiya mawaziri wake kufanya kampeni za mikutano ya hadhara kuwashawishi Waturuki wanaoishi katika nchi hizo kupiga kura ya ndio wakati wa kura hiyo ya maoni.
Merkel ataka serikali izungumze na upinzani
Merkel und Hollande Symbolbild (Getty Images/S. Gallup) Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa .
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameitolea wito serikali ya Uturuki kufanya mazungumzo ya kina na vyama vyote vya kisiasa pamoja na asasi za kiraia, kutokana na ushindi finyu wa kura hiyo ya maoni kuonesha namna taifa hilo lilivyogawika. Katika taarifa ya pamoja na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Sigmar Gabriel, Merkel amesema Ujerumani inaheshimu uamuzi wa watu wa Uturuki juu ya katiba yao, lakini wakati huo huo wamemtaka Rais Erdogan kutambua dhamana kubwa aliyonayo katika kuivuusha nchi yake kwenye hatua ya pili.
Ufaransa nayo imejiunga na Ujerumani kumtaka Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki kufanya mazungumzo na wapinzani wake wa kisiasa, kufuatia ushindi huo finyu sana kwenye kura ya maoni.  Rais Francoise Hollande wa Ufaransa amesema kwenye taarifa yake Jumatatu, kwamba ni juu ya Waturuki wenyewe kuamua utaratibu wa kisiasa, lakini matokeo ya kura hiyo ya maoni yanaakisi namna taifa hilo lilivyogawika.Lakini ikulu ya Urusi, Kremlin, imesema maamuzi ya kura hiyo ni jambo la ndani na Uturuki, na kwamba lazima yaheshimiwe.

Monday, April 17, 2017

ERDOGAN ASHINDA KURA YA MAONI WAPINZANI WADAI KULIKUWA NA UDANGANYIFU

Rais wa Uturuki Erdogan ameibuka mshindi katika kura ya maoni ya kihistoria Jumapili(16.04.2017) itakayoimarisha madarakani yake, na matokeo hayo yameiacha nchi hiyo ikigawanyika mno na upinzani unalalamikia udanganyifu.
Türkei Referendum Wahllokal in Istanbul Präsident Erdogan (Reuters/A. Konstantinidis) Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Mabadiliko  hayo  makubwa  ya  katiba  yaliyoidhinishwa  kupitia kura  hiyo  ya  maoni yanaunda  mfumo  wa  madaraka  ya  rais ambao  utampa  rais Erdogan  madaraka  zaidi  kuliko  kiongozi yeyote  tangu  muasisi  wa  Uturuki Mustafa Kemal Ataturk  na mrithi wake  Ismet Inonu.
Kambi  ya "ndio" imeshinda  kwa  asilimia  51.4 ya  kura  dhidi  ya asilimia  48.6 kwa  upande  wa  "hapana", tume  ya  uchaguzi imesema  katika  tarakimu  zilizonukuliwa  na  shirika  la  habari  la Anadolu, katika  zoezi  la  kuhesabu  kura  kwa  misingi  ya  asilimia 99.5 ya  masanduku  ya  kura. Watu waliojitokeza  kupiga  kura  ni asilimia  85.
Türkei Regierung erklärt Sieg bei Referendum (picture alliance/AA/H. Yaman ) Watu wakipunga bendera wakifurahia ushindi wa Erdogan
Matokeo  ya  kura  hiyo  pia  yanaathari  pana  kwa  Uturuki  ambayo imejiunga  na  jumuiya  ya  kujihami  ya  NATO mwaka  1952 na katika  kipindi  cha  mwisho  cha  nusu  karne  nchi  hiyo  imelenga katika  kujiunga  na  Umoja  wa  Ulaya.
Sherehe mitaani
Kundi  kubwa  la  watu  waliokuwa  wakipunga  bendera walisherehekea  ushindi  huo  mitaani, Erdogan  akiisifu  Uturuki kwa kuchukua "uamuzi  wa  kihistoria".
Türkei Referendum | Abstimmung (picture alliance/AA/E. Atalay) Mifuko ya kura kutoka katika vituo vya kupigia kura nchini Utruki
"Pamoja  na  umma, tumeweza  kufikia  mabadiliko  muhimu  katika historia  yetu," ameongeza.
Lakini  waungaji  mkono  wa upinzani  katika  wilaya  zinazompinga Erdogan  za  mjini  Istanbul  wameonesha  kutoridhishwa  kwa kupiga mabakuli  na  sufuria kwa  vijiko  na  umma  na  kufanya kelele  za  kupinga. Mamia  ya  watu  pia  waliingia  mitaani  katika maeneo  ya  Besiktas  na  Kadikoy.
Mkuu  wa  mamlaka  kuu  ya  uchaguzi  Sadi Guven  amethibitisha kwamba  kambi  ya  "ndio" imeibuka  mshindi, lakini  upinzani umeapa  kupinga  matokeo  hayo.
Kura  hiyo  ya  maoni  ilifanyika  chini  ya  amri  ya  hali  ya  hatari ambayo  imeshuhudia  watu  47,000 wakikamatwa  katika ukandamizaji  baada  ya  jaribio  lililoshindwa  la  mapinduzi  dhidi  ya Erdogan Julai  mwaka  jana.
Türkei Yildirim verkündet den Sieg der Ja-Sager (picture alliance/AA/A. Balikci) Waziri mkuu wa Uturuki na kiongozi wa chama tawala cha AKP Binali Yildirim
Mwishoni  mwa  kampeni iliyokuwa  na  hamasa  nyingi , kambi  ya "hapana" iliweza  kuongeza  idadi  ya  kura  wakati  kura  zaidi zikihesabiwa , baada  ya  kuwa  nyuma  kwa  muda  mrefu  katika matokeo  ya  awali, lakini  kambi  hiyo  ilishindwa  kuipita  kambi  ya kura  za  "ndio".
Wakati  huo  huo theluthi  mbili  ya  Waturuki  wanaoishi  nchini Ujerumani wamepiga  kura  zao  wakimuunga  mkono  rais Recep Tayyip Erdogan katika  kura  ya  maoni  inayotaka  kumpa  madaraka zaidi  rais. Asilimia  63.1  ya  wapigakura  Waturuki  nchini Ujerumani  wameunga  mkono  hatua  hiyo, limesema  shirika  la habari  la  Uturuki Anadolu  mapema  leo  Jumatatu.
Brexit-Hauptakteure - Jean-Claude Juncker (Getty Images/C. Court) Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker
Maoni ya viongozi mbali mbali
Taarifa ya  pamoja ya rais  wa  Halmashauri  ya  Umoja  wa  Ulaya Jean-Calude Juncker  na  waziri  mwenye  dhamana  ya  masuala ya  kigeni  katika  Umoja  huo  Federica Mogherini  imesema , mabadiliko  ya  katiba  na  hususan utekelezaji  wake utatathminiwa kwa  misingi  ya  jukumu  la  Uturuki  kama nchi  inayotaka  kujiunga na  Umoja  huo  na  mwanachama  wa  baraza  la  Ulaya.