Mwanamke raia wa Misri mwenye uzito wa kilo 500 amewasili Mumbai
nchini India, ambapo anatarajia kufanyiwa misururu ya upasuaji kupunguza
uzito wake. Inaripotiwa kuwa mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 36
huenda ndiye mwanamke mwenye uzito mkubwa kabisa duniani. Alisafirishwa
kwa ndege inayosafirisha mizigo. Eman Ahmed tayari anaugua kiharusi
ambacho kimesababisha mkono na mguu wake wa kulia kupooza, hali ambayo
imeathiri uwezo wake wa kuzungumza. Amelazwa katika hospitali ya Saifee
ambako wadi maalum yenye milango mikubwa na kitanda imara vimeundwa kwa
ajili yake. Atafanyiwa misururu ya majaribio kabla madaktari kumfanyia
upasuaji kupunguza uzito wake. Madaktari wanasema wanaweza kuchukua muda
wa miezi sita au zaidi. Kulingana na taarifa kwenye mtandao unaomfanyia
kampeni ya matibabu, Ahmed anaugua ugonjwa wa kisukari aina ya pili,
shinikizo la damu, ugonjwa wa mapafu na nyongo miongoni mwa mengine
makali. Ilibidi kreni kutumika kumpandisha kwenye ndege na pia kumshusha
kwenye ndege.
No comments:
Post a Comment