Friday, February 10, 2017

VELAYATI: VITISHO VYA TRUMP HAVITASITISHA MAENDELEO YA UWEZO WA KIULINZI WA IRAN

Mkuu wa kituo cha utafiti wa kistratejia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran amesisitiza kuwa vitisho vya rais mpya mwenye makelele wa Marekani haviwezi katu kusitisha maendeleo ya kiulinzi ya Iran.
Ali Akbar Velayati aliyasema hayo jana katika mahojiano na gazeti la Kifaransa la Le Monde na kanali ya televisheni ya France 24.
Dokta Velayati amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haivipi umuhimu wowote na wala haishughulishwi na vitisho na vikwazo vinavyotangazwa na serikali mpya ya Marekani dhidi yake na kuongeza kuwa Donald Trump anaendelea kufuata njia na sera zilezile za marais waliopita wa Marekani dhidi ya Iran.
Mkuu wa kituo cha utafiti wa kistratejia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran amefafanua kuwa tofauti pekee aliyonayo Trump na marais wengine waliotangulia wa Marekani ni katika mbinu ya utangazaji uadui wa Washington dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa wananchi wa Iran wana historia na ustaarabu mkubwa na wamejiweka tayari kukabiliana na mashinikizo.
Rais Donald Trump wa Marekani
Akijibu suali la mwandishi wa habari wa kanali ya televisheni ya France 24 kuhusu majaribio ya makombora ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Velayati amesema, lengo la Iran la kufanya majaribio ya makombora ni kwa ajili ya ulinzi tu na kwa msingi wa kuiramisha uwezo wake wa kujihami.
Kuhusiana na kadhia ya nyuklia, Mkuu wa kituo cha utafiti wa kistratejia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran amesema, kinyume na nchi nyingi ikiwemo Ufaransa ambayo haikusaini Mkataba wa Kuzuia Uundaji na Uenezaji Silaha za Nyuklia (NPT) mpaka ilipokuwa imeshamiliki silaha za nyuklia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina nia ya kumiliki silaha hizo, kwa sababu kwa mujibu wa fatua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, utumiaji wa silaha za aina hiyo ni haramu.
Huku akiashiria kuwa Iran ni mwanachama wa NPT na kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani ni haki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Dokta Veleyati amesisitiza kuwa sio tu Iran haina hatihati bali iko imara na thabiti katika azma yake ya kutumia na kunufaika na teknolojia ya nyuklia.../

No comments:

Post a Comment