Mawaziri wa kigeni wa nchi 20 zinazoongoza kiviwanda na
kiuchumi wanakutana mjini Bonn Ujerumani, kuijadili njia za kuepukana
na mizozo siku za mbele, huku kukiwa na wasiwasi juu ya muelekeo wa sera
ya nje ya Marekani.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, ambaye
ndiye mwenyeji wa mazungumzo hayo ya siku mbili, amesema kwamba
kuchaguliwa Rais Donald Trump kunapaswa kuwa sawa na king'ora cha
kuiamsha Ulaya, kukabiliana na changamoto zijazo. Waziri Gabriel
aliliambia gazeti la kila siku la Ujerumani, Frankfuerter Allgemeine
Zeitung, kwamba Umoja wa Ulaya unahitaji mageuzi, ikiwa unataka kweli
kuwa na umuhimu mbele ya madola yenye nguvu kama Marekani, Urusi na
China.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel
Alisema
tumekuwa tukiamini kwa muda mrefu, kwamba mwenendo wetu wa kuishi
unalindwa vilivyo na Wamarekani, akimaanisha ushawishi wa Marekani
kiutamaduni, diplomasia na kijeshi katika ulimwengu wa Magharibi baada
ya vita vya pili vya dunia. Gabriel alisema wakati umewadia kwa Waulaya
kusimamia maadili yao na ikihitajika hata kwa njia ya kijeshi, bila ya
kutegemea msaada wa Marekani. Kwa kufanya hivyo kutasaidia kuondokana na
shaka shaka zinazoongezeka kuhusu Ulaya, jambo ambalo limesababisha
kufufuka kwa siasa za kizalendo barani Ulaya katika miaka ya hivi
karibuni.
Mazungumzo miongoni mwa kundi hilo la G20 la mataifa
ya kiviwanda na yanayokuwa kiuchumi, yatatuwama katika kile kinachoitwa
malengo 17 ya maendeleo endelevu yaliokubaliwa na Jumuiya ya Kimataifa
yawe yamefikiwa ifikapo 2030. Lakini mazungumzo ya pembeni yalianza
mapema asubuhi kabla ya kufunguliwa mkutano huo leo mchana.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Rex Tillerson
Kwa
upande wa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Rex Tillerson,
ambaye ujumbe wake umepiga kambi nje ya jiji la Bonn itakuwa ni nafasi
yake ya kwanza kukutana na mawaziri kadhaa wa mambo ya nchi za nje,
akiwemo, Sergei Lavrov, wa Urusi ambaye alipangiwa kukutana naye baadae
leo. Tayari Tillerson alikutana kwa mara ya kwanza na mawaziri
wenzake wa Saudi Arabia, Uingereza, Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Mbali na mizozo duniani na njia ya kukabiliana nayo, masuala mengine
katika ajenda ni kuanzia jinsi ya kulisaidia bara la Afrika, changamoto
za mabadiliko ya tabianchi hadi vita nchini Syria wakati huu wa
misukosuko katika maeneo mbalimbali duniani.
Mkutano huu wa Bonn,
utakuwa sawa na maandalizi ya mkutano wa viongozi wakuu wa taifa na
serikali wa kundi hilo la G20, watakaokutana katika mji wa bandari wa
kaskazini mwa Ujerumani - Hamburg, mwezi Julai.
No comments:
Post a Comment