Friday, February 3, 2017

VELAYATI: MAREKANI INAFANYA ' MAKEKE HEWA' DHIDI YA IRAN

Mkuu wa kituo cha utafiti wa kistratijia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran amevielezea vitisho ilivyotoa Marekani kufuatia jaribio la kombora lililofanywa na Iran kuwa ni "makeke hewa".
Akizungumzia kauli za vitisho zilizotolewa na serikali ya Marekani, Ali Akbar Veleyati amesema, hii si mara ya kwanza kwa mtu asiye na tajiriba kutoka Marekani kutoa vitisho dhidi ya Iran. Amefafanua kuwa baada ya muda kupita, Trump ataelewa kwamba utoaji kauli hewa za majigambo na makeke dhidi ya Iran kutazidi kushusha hadhi na itibari yake tu mbele ya fikra za walimwengu.
Dakta Velayati, ambaye pia ni mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amesisitiza kwa kusema: "Ni vizuri huyu bwana (Trump) au watu wengine ambao ndio kwanza wamepata tajiriba ya kuongoza serikali, wakajifunza kutokana na uzoefu wa wale walioongoza serikali nchini Marekani huko nyuma ili kuelewa kwamba wasifanye makeke yasiyo na msukumo na kujifanya kinyago mbele ya nchi nyingine na fikra za walimwengu".
Rais Donald Trump wa Marekani
Mkuu wa kituo cha utafiti wa kistratijia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Iran ametoa jibu hilo, baada ya kama ilivyokuwa huko nyuma, viongozi wa serikali ya Marekani kutoa kauli za vitisho dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa sababu ya jaribio ililofanya hivi karibuni la kombora la balistiki.
Rais Donald Trump wa Marekani aliandika katika ukurasa wake wa kijamii wa Twitter hapo jana kuwa, Iran imepewa onyo kwa sababu ya jaribio ililofanya la kombora la balistiki.
Hii ni katika hali ambayo Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Hussein Dehqan alithibitisha siku ya Jumatano kuhusu kufanyiwa jaribio kombora hilo na kusisitiza kwamba Tehran haitoruhusu ajinabi yeyote kuingilia masuala yake ya kiulinzi…/

No comments:

Post a Comment