Sunday, February 5, 2017

SISITIZO LA WAPINZANI WA NETANYAHU LA KUJIUZULU WAZIRI MKUU HUYO WA ISRAEL

Upinzani dhidi ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel umeongezeka sana hivi sasa. Mamia ya wakazi wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu wanaendelea kuandamana wakimshikinikiza Netanyahu ajiuzulu.
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni hadi sasa ameshasailiwa mara kadhaa kutokana na kuhusika kwenye ubadhirifu wa fedha ndani ya utawala wa Kizayuni. Kushindwa siasa za Netanyahu katika miaka ya hivi karibu pamoja na vitendo vyake vya ufisadi kama walivyo viongozi wengine wa Israel, kumeshadidisha migogoro ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ndani ya utawala wa Kizayuni. Jambo hilo aidha limewafanya wakazi wa utawala wa Kizayuni wafanye maandamano ya mara kwa mara kuwalaani viongozi wa Israel. Waandamanaji hao wanamlalamikia vikali Netanyahu na kutaka kundolewa kinga yake ya kutoshtakiwa.
Waziri Mkuu wa Israel anashutumiwa kupokea hongo ya mamilioni ya dola za Kimarekani kupitia mkataba uliotiwa saini baina ya Israel na shirika moja la Ujerumani, wa kuuziwa nyambizi utawala huo dhalimu. Aidha Netanyahu anashutumiwa kwa kumpigia simu mmiliki wa gazeti la Kizayuni la Yediot Ahronot na kutaka kumpa rushwa ili gazeti hilo lilinde manufaa ya Netanyahu na limsaidie kubakia madarakani.
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel

Maandamano hayo makubwa ya Wazayuni yanafanyika katika hali ambayo, kwenye miezi ya hivi karibuni, kumezuka vita vikubwa vya kugombea madaraka na kutoa hongo za kisiasa na kiuchumi baina ya wanasiasa wa Israel. Jambo hilo linabainisha kwamba, utawala wa Kizayuni unakaribia kutumbukia kwenye wimbi jipya za mizozo ya kisiasa.
Baadhi ya wabunge wa utawala wa Kizayuni wamekuwa wakitoa matamshi mbalimbali ya kumlaumu vikali Netanyahu na wanamuona ni Waziri Mkuu asiye na uwezo wa kuongoza serikali. Hivi sasa wimbi la mizozo ndani ya utawala wa Kizayuni imezidi kuvidhoofisha vyama vikuu vya utawala huo pandikizi kikiwemo chama cha Likud kinachoongozwa na Benjamin Netanyahu. Sambamba na kupamba moto mashinikizo ya kumtaka Benjamin Netanyahu angóke madarakani, vita vya maneno na malumbano ya kisiasa yameongezeka pia kati ya viongozi wa Israel. Upinzani unaozidi kuongezeka dhidi ya Benjamin Netanyahu na masuala mengine mbalimbali ikiwemo kufuatiliwa kesi tofauti zikiwemo za ufisadi wa Benjamin Netanyahu, kunatilia nguvu mtazamo kwamba, Waziri Mkuu huyo wa Israel amekaribia kungólewa madarakani na kumalizika umri wake wa kisiasa. 
Maandamano ya kupinga ufisadi wa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni yakiendelea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Vile vile kuendelea utawala wa Kizayuni kukumbwa na migogoro tofauti kunazidi kuonesha kukaribia mwisho mbaya wa utawala huo pandikizi. Wakazi wa utawala wa Kizayuni wanaonesha wazi kuwa wamechoshwa na viongozi wa utawala huo ambao wananuka ufisadi wa kila namna. Kila leo wakazi hao wanazidi kuonesha hasira zao kwa njia tofauti ikiwa ni pamoja na hata kujichoma moto.
Wimbi la malalamiko ya wakazi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya siasa za viongozi wa Israel ni ushahidi mwingine unaoonesha wimbi kubwa la migogoro ndani ya utawala ghasibu wa Israel. Uhakika mwingine ni kuwa migogoro hiyo haitarajiwi kumalizika katika siku za karibuni bali inaongezeka sekunde baada ya sekunde nyingine. Ni kwa kuzingatia yote hayo ndio maana wachambuzi wa masuala ya kisiasa wakauita mwaka huu wa 2017 kuwa ni mwaka wa kupamba moto na kushadidi migogoro ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel. 

No comments:

Post a Comment