Serikali ya Ottawa imesema inachunguza madai yaliyotolewa na vyombo vya habari na mashirika ya kiraia kuwa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia unatumia silaha zilizotengenezwa Canada katika ukandamizaji na jinai dhidi ya raia wake.
Upinzani na mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Canada yameitaka serikali ya nchi hiyo isimamishe miamala na mauzo ya silaha kwa Saudia yakisisitiza kuwa Ottawa itajibebesha bure dhima ya ukatili unaofanywa na Riyadh dhidi ya raia wake wasio na ulinzi mashariki mwa nchi.
Vyombo vya habari nchini Canada vimesema kuwa, magari ya deraya na silaha zinazotumiwa na utawala wa Riyadh katika mashambulizi dhidi ya wakazi wa mashariki mwa nchi zina nembo za kuthibitisha kuwa zimetoka Canada.
Askari wa utawala wa kidikteta wa Aal-Saudi wameshadidisha mashambulizi kwa kutumia mizinga na silaha nyingine nzito katika makazi ya Waislamu wa Shia ya mji wa al-Awamiyah, mashariki mwa nchi hiyo.
Eneo la mashariki mwa Saudia limekuwa likishuhudia malalamiko ya wananchi wanaodai usawa tangu mwaka 2011. Hata hivyo badala ya utawala wa Aal-Saud kutekeleza matakwa ya wananchi, umekuwa ukitumia mkono wa chuma na ukatili kuwanyamazisha kwa nguvu wakazi wa mji wa al-Awamiyah.
No comments:
Post a Comment