Thursday, August 24, 2017

AMNESTY INTERNATIONAL: RAIA RAQQA SYRIA WAPO HATARINI

Shirika la Amnesty International, limesema kampeni ya kivita ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani ya kuwafurusha wanamgambo wa kundi la IS kutoka mji wa Raqqa, Syria, imesababisha vifo vya mamia ya raia.
Mapigano Raqqa (Reuters/Z. Bensemra)
Shirika hilo la kutetea Haki za Binaadamu - Amnesty International, pia imesema vikosi vya serikali ya Syria vinavyoungwa mkono na Urusi vimefanya mashambulizi ya kutochagua dhidi ya raia, yaliyoripotiwa kutumia mabomu ya kutawanyika na mabomu ya mapipa, katika kampeni nyingine tafauti dhidi ya wanamgambo wa IS kusini mwa mji wa Raqqa.
 "Raia wamekwama katika mji wa Raqqa na wanakabiliwa na mashabulizi kutoka kila upande," imesema ripoti ya Amnesty International.
Jeshi la Kidemokrasia la Syria (SDF) la muungano wa wapiganaji wa Kiarabu na Kikurdi liliingia katika mji huo mnamo mwezi Juni, na hadi kufikia sasa jeshi hilo limeweza kukamata asilimia 60 ya mji huo kutoka kwa wanajihadi wa IS.
Lakini mapigano hayo yamesababisha umwagaji damu mkubwa wa raia ambao bado wamekwama katika mji wa Raqqa, huku kukiwa na ripoti za kwamba zaidi ya raia 167 wameuawa katika mashambulizi hayo ndani na nje ya mji tokea Agosti 14.
Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba hadi raia 25,000 bado wamebaki ndani ya mji huo, lakini maelfu wengine wameukimbia mji, na wanaojaribu kukimbia wanahatarisha maisha yao njiani kutokana na uwezekano wa kulengwa kwa risasi na wapiganaji wa IS pamoja na kukanyaga mabomu yaliyofukiwa ardhini.
Raia wa Raqqa, Syria (DW/A. Alojayli )
Raia wa Raqqa, Syria
Raia watumika kama ngao za kivita
Aidha wanamgambo wa kundi la IS walioukamata mji wa Raqqa na maeneo yaliyouzunguka mnamo mwaka 2014, wanawatumia raia wa mji huo wa kaskazini mwa Syria kama ngao za kivita.
"Kwa vile vikosi vya SDF na vya Marekani vinajua kwamba kundi la IS linawatumia binaadamu kama ngao za kivita, vinalazimika kuongeza jitihada za kuwalinda raia hasa kwa kupunguza mashambulizi pamoja na kutengeneza njia salama," amesema Donatella Ronvera Mshauri Mkuu wa Masuala ya Migogoro wa Amnesty International.
Muungano unaoongozwa na Marekani hata hivyo unasema unachukua tahadhari zote za kuepusha mauaji ya raia.
Shirika la Amnesty International lilizungumza na watu 98 ambao ni miongoni mwa wale waliopoteza makaazi yao, na mmoja wao mkaazi wa zamani wa mji wa Raqqa alisema kwamba wanamgambo wa kundi la IS wanawazuia kuondoka mjini humo. Ameongeza kwamba hawana chakula, wala umeme.
Pamoja na mashambulizi ya anga, raia wa Raqqa wanakabiliana na kitisho cha mashabulizi makali ya  katika maeneo yaliyo na wakaazi wengi na ambayo yapo chini ya udhibiti wa kundi la IS.
Shirika la Amnesty International linahimiza kusitisha utumiaji wa silaha za kulipuka katika maeneo yenye wakaazi wengi, na kutoa wito wa kuunda mfumo wa uchunguzi ulio huru na usio na upendeleo kwa upande wowote ili kuchunguza mauaji ya raia katika vita vinavyoendelea nchini Syria.

No comments:

Post a Comment