Thursday, August 10, 2017

POLISI WANEE WAAUAWA MISRI KATIKA SHAMBULIZI LA DAESH ENEO LA SINAI

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daeh (ISIS) limekiri kutekeleza shambulizi dhidi ya gari la polisi ya Misri na kuua maafisa wanne wa usalama katika eneo la Sinai.
Shirika la habari la AMAQ limenukuu duru za usalama zikisema kuwa, genge hilo la kitakfiri ndilo lililohusika na hujuma ya jana Jumatano dhidi ya gari la kulinda doria la polisi ya Misri, katika mji wa al-Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini.
Shambulizi hilo la Daesh linaonekana kuwa la ulipizaji kisiasa, ikizingatiwa kuwa, mwishoni mwa mwezi uliopita wa Julai, wanachama wake 40 waliuawa baada ya vikosi vya usalama vya Misri kushambulia ngome zao katika Peninsula ya Sinai.
Gazeti la Al-Ahram la Misri limeripoti kuwa, magaidi hao waliliminia risasi gari hilo la doria na kuwaua maafisa wanne wa polisi waliukuwemo kwenye gari hilo na kwamba maafisa usalama tangu jana wamekuwa wakiwasaka kwa udi na uvumba wavamizi hao.
Wanachama wa Daesh katika eneo la Sinai nchini Misri
Eneo hilo la kaskazini mwa Misri limekuwa uwanja wa mashambulizi ya makundi yenye silaha kwa miaka kadhaa sasa. Kundi hatari zaidi ni lile linalojiita Ansar Bait al-Muqaddas ambalo limetangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS).
Eneo hilo halijawahi kushuhudia utulivu tangu magenge ya kigaidi yaanzishe harakati zao mwaka 2013, baada ya jeshi la Misri kumuondoa madarakani Mohamed Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri. 

No comments:

Post a Comment