Mrengo wa upinzani wa NASA nchini Kenya umeitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC imtangaze mgombea wa muungano huo Raila Odinga kuwa, mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika nchini humo siku ya Jumanne.
Akiongea na waandishi wa habari jijini Nairobi hii leo kwa niaba ya muungano huo, Musalia Mudavadi, Wakala Mkuu wa NASA katika uchaguzi huo amesema, vyanzo vyao vya siri ndani ya IEBC vimewapa ithibati kuwa Odinga amepata kura zaidi ya milioni nane huku Rais Uhuru Kenyatta aliyewania kiti hicho kwa muhula wa pili kupitia Chama cha Jubilee akipata kura milioni saba na laki saba.
Mudavadi ambaye amewahi kuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo amesema viongozi wa muungano huo wamefanya kikao na Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati mapema leo na kumkabidhi nyaraka za kuthibitisha madai yao.
Hapo jana viongozi wa NASA walidai kuwa mfumo wa kupeperusha matokeo wa IEBC umedukuliwa, madai ambayo yalikanushwa vikali na maafisa wa tume hiyo.
Matokeo ya awali yaliyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC yanaonesha kuwa, Kenyatta anaongoza kwa kura zaidi ya milioni 8, ambazo ni sawa na asilimia 53.89 ya kura zilizohesabiwa huku mpinzani wake mkuu, Raila Odinga akiwa na kura zaidi ya milioni sita na laki saba ambazo ni sawa na asilimia 44.47 ya kura.
Tume ya Uchaguzi nchini Kenya imetangaza kuwa itatoa matokeo rasmi na ya mwisho ya kura za urais hapo kesho.
No comments:
Post a Comment