Polisi katika jimbo la Haryana nchini India imetangaza kuwa, kwa akali watu 28 wameuawa na wengine 200 kujeruhiwa vibaya katika mapigano yaliyotokea Ijumaa ya jana katika majimbo mawili ya Haryana na Punjab kaskazini mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mapigano hayo makali yaliibuka baada ya Gurmeet Ram Rahim Singh, mmoja wa viongozi wakubwa wa Kihindu wa nchi hiyo kuhukumiwa na Mahakama ya Kati ya Uchunguzi katika mji wa Panchkula, jimbo la Haryana kwa tuhuma za kuhusika na ubakaji dhidi ya wanawake wawili.
Habari zaidi zinasema kuwa, Ram Rahim Singh, kiongozi wa dini ya 'Dera Sacha Sauda' alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela baada ya kubainika na tuhuma za ubakaji wa wanawake wawili. Mbali na Gurmeet Ram Rahim Singh kuwa na nafasi kubwa ya kidini miongoni mwa jamii ya Wahindu nchini India, anahusika pia na shughuli za kijamii kama vile uchezaji sinema, uimbaji na usimamiaji filamu, huku akiwa na ushawishi mkubwa katika majimbo ya Haryana na Punjab kaskazini mwa nchi hiyo. Kwa kuzingatia suala hilo, Ijumaa ya jana maelfu ya wafuasi wake walimiminika mabarabarani baada ya kuhukumiwa kiongozi huyo katika miji mbalimbali kuanzia, Haryana na Punjab na hata mji mkuu wa India New Delhi ambapo walianza kuchoma moto magari, maduka na mali nyingine za umma.
Katika kujaribu kudhibiti hali ya mambo, polisi walitumia helikopta katika anga ya mji wa Panchkula na kukabiliana na wafuasi wa Gurmeet Ram Rahim Singh. Inafaa kuashiria kuwa, kila mwaka maelfu ya wanawake wa India hukumbwa na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia hususan ubakaji, huku wengine wakipoteza maisha.
No comments:
Post a Comment