Sunday, July 30, 2017

KIONGOZI: HIJA NI FURSA YA KUTANGAZA MSIMAMO KUHUSU MSIKITI WA AL-AQSA NA UWEPO WENYE MALENGO MAOVU WA MAREKANI KATIKA ENEO

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Hija ni fursa bora ya mahali na wakati kwa Umma wa Kiislamu kutangaza misimamo kuhusu kadhia ya Palestina, msikiti wa Al-Aqsa na uwepo wenye malengo maovu wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo katika mkutano na viongozi na watendaji wa masuala ya Hija na kuongeza kuwa, Hija ni fursa ya kutangaza misimamo kuhusu maudhui zinazokubaliwa na Umma wa Kiislamu. Amefafanua kwa kusema: Moja ya maudhui hizo ni kadhia ya msikiti wa Al-Aqsa na Quds ambayo inazungumziwa na kupewa uzito zaidi wakati huu kutokana na jeuri, utovu wa haya na ukhabithi wa utawala ghasibu na bandia wa Kizayuni.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa haifai kwa namna yoyote ile kughafilika na suala la Palestina ambalo ni mhimili mkuu wa masuala ya Ulimwengu wa Kiislamu na akaongezea kwa kusema: Kuna mahali gani bora zaidi kuliko Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu, Makka, Madina, Arafat, Mash'ar na Mina kwa mataifa ya Waislamu kudhihirisha mitazamo yao na kubainisha misimamo yao kuhusu Palestina na msikiti wa Al-Aqsa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, uwepo wenye malengo maovu wa Marekani katika nchi za Kiislamu na eneo kwa ujumla na kuanzisha makundi ya kigaidi na kitakfiri, ni maudhui nyengine muhimu  ambayo mataifa ya Waislamu yanapaswa kutangaza msimamo wao juu yake katika Hija. Ameongeza kuwa: Utawala wenyewe wa Marekani ni shari kubwa zaidi na khabithi zaidi kuliko hata makundi ya kigaidi uliyoyaanzisha. 
Viongozi na wasimamizi wa ibada ya Hija wakisikiliza hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
Katika sehemu nyengine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei ameeleza kuwa maudhui ya umoja ni jambo jengine muhimu zaidi na la dharura kwa mataifa ya Waislamu, na akafafanua kwa kusema: Wakati mabilioni ya dola zinatumika kuzusha mifarakano, hitilafu na uadui baina ya Waislamu, Waislamu wenyewe wanapaswa wajihadhari na kufanya mambo yatakayosaidia uzushaji huo wa hitilafu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Takwa muhimu zaidi na la kila mara la Jamhuri ya Kiislamu ni kudhaminiwa usalama, izza na huduma bora kwa mahujaji wote hususan wa Kiirani; na kudhamini usalama wa Hija ni jukumu la nchi yenye mamlaka ya Haram Mbili Tukufu.../

No comments:

Post a Comment