Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, jamii ya kimataifa inalazimika kukomesha utamaduni wa kutouadhibu utawala wa Kizayuni wa Israel na kuulazimisha utawala huo usitishe kabisa uhalifu na jinai zake dhidi ya watu wa Palestina.
Muhammad Javad Zarif ambaye jana jioni alikuwa akihutubia mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) unaofanyika Istanbul nchini Uturuki kujadili kadhia ya Quds tukufu, amelaani mashambulizi yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina na kusema kuwa: Umma wa Kiislamu unapaswa kusimama imara na kutomruhusu yeyote kuindoa jumuiya ya OIC katika malengo yake makuu ambayo ni kuimarisha umoja na mshikamano wa Kiislamu, kukomesha uvamizi wa Israel na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina na kuunga mkono jitihada za kuundwa dola huru la Palestina, mji wake mkuu ukiwa Quds tukufu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amezungumzia mzingiro wa Israel dhidi ya watu wa eneo la Ukanda wa Gaza na kusema, mzingiro huo ni jinamizi kubwa kwa wakazi wa eneo hilo ambalo linapaswa kushughulikiwa. Zarif amesema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umepuuza matakwa yote ya jamii ya kimataifa kwa ajili ya kusitisha na kubadili siasa zake za kibaguzi dhidi ya watu wa Palestina.
Tarehe 14 mwezi uliomalizika wa Julai Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel aliliamuru jeshi la utawala huo haramu kufunga milango yote ya kuingia na kutoka katika Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa siku kadhaa, suala lililozusha machafuko makubwa na kupelekea kuuawa raia kadhaa wa Palestina.
No comments:
Post a Comment