Sunday, August 27, 2017

19 AKIWEMO MWANAHABARI WA US WAUAWA KATIKA MAPIGANO SUDANI KUSINI

Watu 19 akiwemo mwandishi wa habari raia wa Marekani wameuawa katika mapigano mapya baina ya vikosi vya serikali na waasi wanaobeba silaha katika jimbo la Yei, nchini Sudan Kusini.
Santo Domic Chol, msemaji wa jeshi la Sudan Kusini ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, mapigano hayo ya jana Jumamosi yalianza baada ya kundi hilo la wabeba silaha kujaribu kuvamia kituo cha kijeshi cha Kaya.
Ameongeza kuwa, waasi 15 wameuawa katika makabiliano hayo huku jeshi la nchi hiyo likipoteza askari wake watatu. 
Wanachama wa genge la waasi Sudan Kusini
Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini amesema mwandishi huyo wa habari wa Marekani aliyeuawa katika makabiliano hayo ya jana kati ya wanajeshi wa serikali na waasi ametambuliwa kwa jina Christopher Allen, ambaye alikuwa akifanyia kazi mashirika kadhaa ya habari.
Sudan Kusini ilitumbukia katika machafuko na mapigano kati ya askari watiifu kwa Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani Riek Machar tangu mwaka 2013.
Vita vya ndani katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika vimewalazimisha raia karibu milioni tatu kuwa wakimbizi katika nchi jirani na maelfu ya wengine kuuawa. 

No comments:

Post a Comment