Tuesday, August 1, 2017

SYRIA NAYO YAIKOSOA SAUDIA KWA KUINGIZA SIASA KATIKA SUALA LA HIJJA

Serikali ya Syria imelalamikia vikali uendeshaji wa kisiasa wa ibada tukufu ya Hijja unaofanywa na utawala wa Aal-Saud wa Saudi Arabia.
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne na Wizara ya Masuala ya Dini ya Syria imekosoa hatua ya Saudia ya kuwawekea vingiti raia wa Syria wanotaka kwenda kutekeleza nguzo hiyo ya Uislamu.
Taarifa hiyo iliyopeperushwa na shirika rasmi la habari la Syria SANA imeongeza kuwa, haki ya kwenda kuhijji inatumiwa kwa malengo ya kisiasa na utawala wa Riyadh.
Saudia ambayo haina uhusiano wa kidiplomasia na serikali ya Rais Bashar al-Assad, tangu mwaka 2012 imekuwa ikiwalazimisha raia wa Syria wanaotaka kwenda kufanya ibada ya Hijja kuomba viza katika nchi ya tatu, kupitia Kamati Kuu ya Hijja ya Syria, inayoongozwa na muungano wa kisiasa wa upinzani.
Mahujaji wakiwa wamefurika katika Mlima Arafa
Hii ni katika hali ambayo, awali Qatar pia ililalamika kuwa Riyadh imewawekea vikwazo na vizingiti chungu nzima Mahujaji wa Qatar wanaotaka kwenda kutekeleza ibada hiyo muhimu ya Uislamu mwak huu.
Kamisheni Taifa ya Haki za Binadamu ya Qatar imewasilisha malalamiko hayo kwa Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia masuala ya haki ya kuabudu ikisisitiza kuwa kitendo hicho cha utawala wa kifalme wa Aal-Saudi cha kuendesha ibada ya Hija kisiasa kinakiuka sheria na makubaliano ya kimataifa yanayomdhaminia kila mtu uhuru wa kuabudu.
Huko nyuma Saudi Arabia imewahi kutumia ibada hiyo kisiasa dhidi ya Mahujaji wa Kiirani na Yemen. 

No comments:

Post a Comment