Bunge la Misri Jumanne wiki hii limeidhinisha marekebisho ya sheria yanayowazuia askari polisi wa nchi hiyo kutoa taarifa kwa vyombo vya habari.
Marekebisho hayo ya sheria yanayohusiana na askari polisi ambayo yaliidhinishwa jana na bunge la Misri, yanawapiga marufuku polisi nchini humo kutoa taarifa kwa vyombo vya habari, kuchapisha nyaraka, ripoti au picha zinazohusiana na kazi zao bila ya kuwa na kibali cha maandishi.
Polisi yoyote atakayekiuka sheria hiyo mpya atakabiliwa na adhabu ya kifungo cha jela au kulipa fidia ya pauni za Misri elfu ishirini sawa na yuro 2026.
Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri mwezi Februari mwaka huu alimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo achukue hatua za kubana mamlaka ya polisi nchini humo na pia awasilishe mapendekezo bungeni kuhusu suala hilo. Hii ni katika hali ambayo jumuiya za kutetea haki za binadamu na za mawakili nchini Misri kwa muda mrefu zimekuwa zikikosoa kile zinachokitaja kuwa ni kuwepo utamaduni wa kutoadhibiwa katika ngazi mbalimbali za utawala wa Misri; na kueleza kuwa, utumiaji mabavu na ukandamizaji wa polisi nchini humo umekuwa jambo la kawaida.
Wakati huo huo wakosoaji wa serikali ya Rais al Sisi wanaamini kuwa kupasishwa sheria hiyo mpya bungeni ni katika juhudi za kuficha maovu zaidi na vitendo vya ufisadi vinavyofanyika katika ngazi ya juu.
No comments:
Post a Comment