Sunday, August 20, 2017

GRACE MUGABE APEWA KINGA YA KIDIPLOMASIA YA KUONDOKA AFRIKA KUSINI

Mke wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Grace Mugabe ambaye anakabiliwa na kesi ya kumpiga na kumjeruhi mwanamitindo wa Afrika Kusini amepewa kinga ya kidiplomasia.
Ripoti zinasema serikali ya Afrika Kusini jana Jumamosi ilimpa kinga ya kidiplomasia Grace Mugabe na kumruhusu kuondoka nchini humo na kurejea nchini kwake. 
Grace Mugabe anatuhumiwa kwamba wakati wa safari yake nchini Afrika Kusini alimpiga na kumjeruhi mwanamitindo, Gabriella Angels mwenye umri wa amiaka 20. Ripoti zinasema Grace Mugabe alimpiga mwanamitindo huyo baada ya kushuku kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na kijana wake anayesoma nchini Afrika Kusini.
Mwanamitindo, Gabriela Engels
Chama kikuu cha upinzani nchini Afrika Kusini kilikuwa kimetoa wito wa kutiwa mbaroni mke wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma ya kumpiga na kumjeruhi mwanamitindo huyo. Chama cha Democratic Alliance (DA) kimesema, Grace Mugabe anapaswa kutiwa mbaroni baada ya kumshambulia na kumpiga Gabriella Engels na kwamba, hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria. Hata hivyo serikali ya Zimbabwe iliomba mke wa Rais wa nchi hiyo ambaye alikuwa safarini nchini Afrika Kusini, apewe kinga ya kidiplomasia. 
Grace Mugabe ni miongoni mwa watu wanaotajwa kuwa na nafasi ya kumrithi mumewe, Rais Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 93.

No comments:

Post a Comment