Serikali ya Myanmar imeamua kuongeza idadi ya wanajeshi wake katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa nchi hiyo suala ambalo limetajwa kuwa na kwa lengo la kuzidi kuwakandamiza Waislamu wa kabila ya Rohingya. Maelefu ya Waislamu hao wamelazimika kukimbilia Bangladesh kuokoa maisha yao.
Viongozi wa Waislamu wa Rohingya walioko nchini Bangladesh wamesema kuwa mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Myanmar yameongezeka sana kiasi kwamba kambi za wakimbizi za Waislamu hao nchini Bangladesh zimefurika watu hivi sasa. Waislamu wapatao 75 elfu wa kabila la Rohingya wamekimbilia nchi jirani ya Bangladesh tangu lilipoanza wimbi jipya la ukandamizaji na unyanyasaji wa Waislamu hao huko Myanmar. Takwimu za serikali ya Bangladesh zinaonesha kuwa, hivi sasa kuna Waislamu wapatao laki nne katika kambi za wakimbizi za Bangladesh ambao wamelazimika kuacha kila kitu chao ili kuokoa maisha yao kutokana na ukatili mkubwa wanaofanyiwa na mabudha wenye chuki za kidini. Wimbi jipya la wakimbizi hao limekuja baada ya serikali ya Myanmar kutuma idadi kubwa ya wanajeshi katika jimbo la Rakhine lenye Waislamu wengi. Waislamu hao wa Rohingya wanaamini kuwa, kutumwa wanajeshi hao kwenye jimbo hilo ni ishara ya kukaribia kuzuka wimbi jipya la kuuliwa kikatili ya mabudha wenye misimamo. Serikali ya mabudha ya Myanmar inadai kuwa Waislamu hao eti wamenzisha kambi za kijeshi hivyo imeamua kutuma wanajeshi kukabiliana na Waislamu. Hata hivyo Waislamu wa jimbo hilo la Rakhine wanasema hiyo ni ishara ya kukaribia wimbi jipya la ukandamizaji wa serikali na mabudha wenye misimamo mikali dhidi yao. Serikali ya Myanmar inachuja mno habari zinazohusiana na hali ya Waislamu wa nchi hiyo, lakini hata hizo habari chache sana zinazovuja kutoka katika eneo hilo zinaonesha kuweko kiwango kikubwa cha ukatili na mauji ya kimbari dhidi ya Waislamu hao. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kuanza wimbi jipya la maelfu ya wakimbizi Waislamu wa kabila la Rohingya hakukutokezea vivi hivi, bali ni ushahidi wa wazi wa kuwa mbaya hali ya Waislamu hao nchini Myanmar.
Yanghee Lee, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar anasema: Jeshi la Myanmar linahusika katika ukatili na unyama wanaofanyiwa Waislamu wa Rohingya. Ukubwa wa ukatili na unyama huo ni shadidi sana kuliko watu wanavyodhani duniani. Wanajeshi wa serikali ya Myanmar wanawanajisi kimakundi wanawake wa Kiislamu na kuwachinja kama wanyama kwa kuwakata vichwa Waislamu wa Rohingya wa kike na wa kiume. Baada ya ukatili huo huwachukua watoto wadogo wa Waislamu hao na kuwavurumisha katikati ya moto unaoteketeza nyumba zao.
Waislamu wanaeendelea kukandamizwa na kunyanyaswa vibaya katika hali ambayoi hadi hivi sasa serikali ya Myanmar inaendelea kukaidi amri ya Umoja wa Mataifa ya kuandaa ripoti kuhusu hali ya Waislamu wa Rohingya huko Rakhine. Serikali ya Mynamar inawanyima Waislamu wa nchi hiyo hata haki zao za kimsingi kabisa kama vile uraia. Inadai kuwa eti Waislamu hao ni wageni kutoka nchi jirani ya Bangladesh, wakati wamekuwa wakiishi Myanmar kwa karne nyingi sana.
Alaakullihaal, Umoja wa Mataifa umetangaza rasmi kuwa Waislamu wa Rohingya ni jamii ya watu wachache inayodhulumiwa zaidi duniani. Kinachotarajiwa na walimwengu ni kuuona Umoja wa Mataifa hauishii kulaani kwa maneno tu jinai wanazofanyiwa Waislamu hao na mabudha wenye misimamo mikali pamoja na wanajeshi wenye chuki za kidini wa serikali ya Myanmar. Bali Umoja wa Mataifa ambacho ndicho chombo kikubwa zaidi cha kimataifa duniani, kina jukumu la kuchukua hatua za kivitendo za kuzuia haraka kutokea wimbi lolote jipya la mauaji na ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo ambao wenyewe Umoja wa Mataifa unakiri kuwa ni jamii ya wachache inyaonyanyaswa na kudhulumiwa zaidi duniani.
No comments:
Post a Comment