Sunday, August 27, 2017

USAFIRISHAJI BIDHAA ZA IRAN NCHINI KENYA KUONGEZEKA KWA ASILIMIA 100 KATIKA MWAKA 2017

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Kenya amesema usafirishaji bidhaa zisizo za mafuta za Iran kuelekea nchini Kenya katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu wa 2017 ulikuwa wa kiwango cha dola milioni 58 na inakadiriwa kuwa hadi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu kiwango hicho kitaongezeka kwa kasi kubwa na kufikia asilimia 100.
Hadi Farajvand ameyasema hayo leo kuhusiana na hatua zilizochukuliwa na ubalozi wa Iran mjini Nairobi kwa ajili ya kustawisha uhusiano wa kibiashara na Kenya na kuongeza kuwa: Mashirika ya Kiirani yanayoshughulika sekta za biashara, uchumi na utoaji huduma na kiufundi na kiuhandisi yamepata fursa nzuri za kutangaza bidhaa na huduma zao katika soko la Kenya na pia kwenye masoko ya nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Hadi Farajvand, Balozi wa Iran nchini Kenya
Farajvand amebainisha kuwa, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, mashirika ya Kiirani yamekamilisha miradi ya utoaji huduma za kiufundi na kiuhandisi yenye thamani ya zaidi ya dola milioni mia moja na hivi sasa yanaendelea na mazungumzo kwa ajili ya kufunga mikataba mingine ya miradi ya ujenzi wa mabwawa, vinu vya umeme wa nishati ya maji na mabomba ya usafirishaji fueli.
Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Kenya ameeleza kwamba kuandaa ratiba kwa ajili ya safari ya jumbe za kiuchumi za Kenya nchini Iran na kuandaa maonyesho ya kwanza maalumu ya Iran mjini Nairobi ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na ubalozi wa Iran mjini Nairobi kwa lengo la kuongeza kiwango cha usafirishaji bidhaa za Iran na utoaji huduma za kiufundi na kiuhandisi nchini Kenya.../

No comments:

Post a Comment