Saturday, August 19, 2017

MSAIDIZI MKUU WA DONALD TRUMP KATIK IKULU YA WHITE HOUSE STEVE BANNON AFUTWA KAZI

Steve Bannon

Mkuu wa mikakati wa Rais Donald Trump katika ikulu ya White House, Steve Bannon amefutwa kazi na kuwa msaidizi wa karibuni zaidi wa Trump kuondoka katika wadhifa wake.
Katibu wa mawasiliano na wanahabari katika ikulu hiyo Sarah Huckabee Sanders amethibitisha kwamba Ijumaa ilikuwa siku ya mwisho kwa Bannon kazini.

Kuondoka kwake kumejiri baada ya kutathminiwa kwa wadhifa wake na Mkuu wa Watumishi wa Rais John Kelly.
Bw Bannon ni mtetezi wa taifa mwenye kufuata siasa za mrengo wa kulia.

Alikuwa mkuu wa tovuti ya Breitbart.com na alisaidia pakubwa kueneza ujumbe wa "America First" (Marekani Kwanza) wa Trump wakati wa kampeni za urais mwaka jana.

Lakini wakosoaji wamemtuhumu Bannon, 63, kwa kuwa na chuki dhidi ya wayahudi na kuwa mtu anayeamini katika ubabe wa wazungu.

Bw Bannon anadaiwa kushindania udhibiti wa ikulu dhidi ya mirengo ya watumishi wenye misimamo ya wastani ikulu, wakiwemo baadhi ya jamaa wa Trump.

Bw Trump alianzisha uvumi kumhusu Bannon alipoulizwa kuhusu mustakabali wake wiki iliyopita lakini akajibu: "Tutasubiri tuone."

Mahojiano ya Bannon na jarida la msimamo huru la American Prospect wiki hii yanadaiwa kumkera Trump.

Bannon alinukuliwa akipuuzilia mbali wazo la kutumia jeshi kutatua mzozo kuhusu Korea Kaskazini, jambo lililotazamwa kama kwenda kinyume na msimamo wa Trump.

Aliambia jarida hilo kwamba Marekani ilikuwa katika "vita vya kiuchumi na China" na kwamba analenga kuwaondoa watu wenye msimamo wa wastani serikali ya Trump ambao anaamini wana msimamo usio mkali sana dhidi ya China.

Bannon baadaye aliambia washirika wake kwamba alidhani alikuwa anaongea akipiga gumzo tu na kwamba hakutarajia angenukuliwa.

Nani mwingine ameondoka White House?
Anthony Scaramucci, mkurugenzi wa mawasiliano - 31 Julai
Reince Priebus, mkuu wa watumishi wa rais ikulu - 28 Julai
Sean Spicer, mkuu wa mawasiliano na wanahabari - 21 Julai
Mike Dubke, mkurugenzi wa mawasiliano 30 Mei

Michael Flynn, mshauri mkuu wa usalama wa taifa - 14 Februari
Bannon alichukua hatamu kama kiongozi wa kampeni ya urais ya Trump Agosti 2016.

Aliwahi kuhudumu katika jeshi la wanamaji la Marekani, mwekezaji wa benki katika Goldman Sachs, produsa wa filami Hollywood na mkuu wa Breitbart News.

Anadaiwa kuwaambia marafiki zake kwamba huenda akarejea katika shirika hilo la Breibart lenye msimamo mkali ambalo limekuwa likimuunga mkono Trump.
Chanzo:BBC

No comments:

Post a Comment