Thursday, August 24, 2017

KOFFI ANNAN: HAKI ZA WAISLAMU WA ROHINGYA NCHINI MYANMAR ZIHESHIMIWE

Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali mauaji ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar na kusisitiza kuwa, utumiaji wa mabavu na nguvu kupita kiasi dhidi yao hakuwezi kusaidia kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo.
Koffi Annan ambaye alikuwa anaongoza kamisheni iliyotwikwa jukumu la kuchunguza na kuja na mapendekezo ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Rohingya, iliyoundwa na Aung San Suu Kyi, mshauri wa ngazi ya juu wa serikali na Waziri wa Mambo ya Nje wa Myanmar amesema kuna haja ya kuwafikisha mbele ya sheria wale wote waliohusika na uvunjaji wa haki za binadamu katika jimbo la Rakhine.
Kamisheni hiyo yenye watu tisa imependekeza katika ripoti yake ya mwisho iliyotolewa leo Alkhamisi kuwa, hatua yoyote inayotajwa kuwa ya kiusalama ya vyombo vya dola nchini Myanmar haifai kuwa na taathira hasi kwa raia na kwamba wahanga wa mgogoro huo wana kila haki ya kupewa misaada ya kibinadamu wanayohitaji.
Akiongea mjini Yangon, Annan amesema serikali ya Myanmar inastahili kuhakikisha kuwa Waislamu wa kabila la Rohingya wanapewa haki sawa na watu wa jamii nyingine za nchi hiyo, ikiwemo haki ya kiuchumi, kijamii na kiraia.
Mabaki ya nyumba za Waislamu wa Rakhine zilizoteketezwa moto
Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa hivi karibuni ilisema kuwa, tangu Oktoba 9 mwaka jana kulipoanza operesheni za jeshi la serikali dhidi ya Waislamu wa Rohingya hadi sasa, zaidi ya watu elfu 75 wamekimbilia nchini Bangladesh kutokana na mauaji na jinai wanazofanyiwa na wanajeshi wakishirikiana na mabudha wenye misimamo ya kuchupa mipaka.
Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada wamekuwa wakitenda jinai za kila aina dhidi ya Waislamu zaidi ya milioni moja wa kabila la Rohingya jimboni Rakhine, wakidai kuwa ni wahamiaji haramu na wala hawafai kupewa haki ya uraia.

No comments:

Post a Comment