Thursday, August 10, 2017

MAGAIDI WALIOHUSIKA NA MAUAJI YA WAKRISTO WA KICOPTI NCHINI MISRI, WAUAWA

Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Misri imetangaza habari ya kuuawa magaidi watatu wanaodhaniwa kuhusika na shambulizi lililowalenga Wakristo wa Kicopti kusini mwa nchi hiyo.
Duru za usalama nchini Misri zimetangaza kuwa, magaidi hao wameuawa katika operesheni zilizotekelezwa na jeshi la nchi hiyo katika mji wa Qena kusini mwa taifa hilo. Tangu mwezi Disemba mwaka jana jumla ya Wakristo 100 wameuawa katika mashambulizi ya kigaidi ambayo genge la ukufurishaji la Daesh lilitangaza kuhusika nayo.
Magaidi wanaofanya jinai nchini Misri
Katika shambulizi la mwisho dhidi ya Wakristo hao lililotokea tarehe 26 Mei mwaka huu, watu 29 wakiwamo watoto kadhaa waliuawa. Aidha mashambulizi mengine yalitokea mwezi Disemba mwaka jana dhidi ya kanisa la mjini Cairo, na mashambulizi mengine mawili katika makanisa ya miji ya Alexandria na Tanta, kaskazini mwa Misri hapo mwezi April ambapo makumi ya watu waliuawa.
Hujuma za kigaidi kuwalenga Wakristo nchini Misri
Maeneo ya katikati na kaskazini mwa Misri ukiwemo mkoa wa Sinai kaskazini, yamekuwa yakishuhudia mashambulizi ya kigaidi dhidi ya askari wa serikali, polisi na hata raia wa kawaida. Kundi la kigaidi la Wilaayat Sina na lililotangaza utiifu wake kwa genge la Daesh (ISIS) ndilo limekuwa likitangaza kuhusika na jinai hizo.

No comments:

Post a Comment