Friday, August 25, 2017

SENETA WA ZAMANI WA MAREKANI AKOSOA VIKALI SIASA NA HATUA ZA RAIS DONALD TRUMP

John Danforth, seneta wa zamani wa Marekani wa chama cha Republican amekosoa siasa za Rais wa nchi hiyo Donald Trump na kusema kuwa, hatua zake hizo zimepelekea kuibuka mifarakano na machafuko katika nchi hiyo.
John Danforth amemtaja Donald Trump kuwa, Rais wa Marekani aliyezusha mifarakano zaidi kuliko Rais yeyote wa nchi hiyo. Seneta huyo wa zamani wa jimbo la Missouri nchini Marekani amesema kama ninavyomnukuu: Donald Trump ndiye Rais aliyezusha mifarakano zaidi katika historia ya nchi yetu. 
John Danforth ambaye amewahi kuhudumu pia kama Mwanasheria Mkuu wa jimbo la Missouri amewataka Warepulican wasimruhusu Trump aharibu na kutia dosari haiba na heshima ya chama hicho.
Rais Donald Trump anatajwa kuwa Rais wa aina yake katika historia ya Marekani
Aidha mwanasiasa huyo mstaafu wa Marekani mwenye umri wa miaka 80 amelaani vikali misimamo ya Rais Donald Trump dhidi ya Waislamu na watu wenye asili ya Amerika ya Latini na kueleza kwamba, Trump daima amekuwa akiegemea upande wa tabaka linalochukiwa zaidi nchini Marekani yaani kundi la wabaguzi ambalo linajiona bora kuliko watu wengine.
Ikumbukwe kuwa, licha ya hatua na vitendo vilivyoshuhudiwa hivi karibuni vya utumiaji mabavu vya makundi ya kibaguzi na ya mrengo wa kulia yenye kufurutu ada nchini Marekani, lakini rais wa nchi hiyo hajawa tayari kujitokeza na kulaani vitendo hivyo vya kibaguzi ambavyo vimekemewa na kulaaniwa katika kila pembe ya dunia.

No comments:

Post a Comment