Sunday, August 20, 2017

MAMLAKA HURU YA USIMAMIZI WA POLISI YA KENYA KUCHUNGUZA VIFO VYA WATU 28 KATIKA GHASIA ZA UCHAGUZI

Mamlaka Huru ya Usimamizi wa Polisi ya Kenya (IPOA) imeanza kufanya uchunguzi kuhusu vifo 28 vilivyotokea katika ghasia za uchaguzi mkuu nchini humo wiki iliyopita huku wachunguzi wakiwa tayari wamechunguza mwili wa binti mmoja na mtoto wanaodaiwa kuuliwa na polisi.
Mkuu wa Mamlaka Huru ya Usimamizi wa Polisi kwa kifupi IPOA, Macharia Njeru amesema chombo hicho kimeanza kuchunguza madai kwamba, polisi waliuwa watu na kuwajeruhi wengine wakati wa uchaguzi mkuu nchini humo wiki iliyopita. Njeru ameongeza kuwa, timu za uchunguzi tayari zimeanza kazi na kwamba wanashiriki katika kila uchunguzi unaofanywa katika mwili wa watu waliouliwa.
Macharia Njeru, Mkuu wa Mamlaka Huru ya Usimamizi wa Polisi ya Kenya
Ghasia zilijitokeza baada ya Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi ya Kenya (IEBC) kumtangaza Rais Uhuru Kenyatta kuwa ameshinda uchaguzi wa rais kwa kupata kura milioni 1.4. Raila Odinga Kiongozi wa Muungano wa upinzani wa (NASA) Jumatano iliyopita alipinga matokeo hayo ya uchaguzi na kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Kilele ya nchi hiyo.
Wakati huo huo George Morara Monyoro Mwenyekiti wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kenya inayofadhiliwa na serikali Jumatano iliyopita ilitangaza kuwa, watu wasiopungua 28 waliuawa katika machafuko kote nchini humo tangu Agosti 8 siku ya uchaguzi. Amesema inaaminiwa kuwa vifo vyote hivyo vilitokana na kupigwa risasi, mauaji ambayo wanayahusisha na polisi.

No comments:

Post a Comment