Friday, August 25, 2017

MAFANIKIO MAKUBWA YA MUQAWAMA; KUONGEZEKA KASI YA KUANGAMIZWA KUNDI LA KIGAIDI LA DAESH (ISIS)

Mwenendo wa kuliangamiza na kulitokomeza kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh umezidi kushika kasi kutokana na azma thabiti na mkakati madhubuti unaotekelezwa na mhimili wa muqawama katika mapambano na kundi hilo.
Vikosi vya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh vilivyokuwa vikisindikizwa na magari kadhaa ya deraya na idadi kubwa ya wapiganaji, siku ya Alkhamisi ya tarehe 24 mwezi huu vilijaribu kushambulia kituo kimoja cha jeshi la Syria katika eneo la Saddul-Wa'ar kwenye mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Syria, lakini vilipata kipigo kikali na kurudi nyuma kutoka eneo hilo baada ya wapiganaji wake wengi kuuawa na kujeruhiwa.
Magaidi wa DAESH (ISIS) walipokuwa wamejizatiti Syria
Katika miezi ya karibuni, kundi hilo la kigaidi na kitakfiri limekuwa likishindwa kwa kupata vipigo mtawalia katika maeneo yote liliyokuwa likiyakalia kwa mabavu katika ardhi za Iraq na Syria. Baada ya kukombolewa mji wa Mosul mkoani Nainawa nchini Iraq, magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh wamekuwa wakiendelea kupata vipigo mfululizo katika mji wa Tal afar pia ulioko kwenye mkoa huohuo na hivyo kuzidi kukaribia kusambaratishwa kikamilifu na kutokomezwa katika ardhi ya nchi hiyo. Lakini si huko Iraq pekee; kwani hata nchini Syria pia kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh pamoja na washirika wake wanaendelea kudhoofika na kusambaratika; kiasi kwamba siku chache zilizopita Rais Bashar Al-Assad wa Syria aliashiria kupatikana ushindi kamili katika vita dhidi ya magaidi hao.
Rais Bashar Al-Assad wa Syria akihutubia wananchi
Moja ya sababu muhimu ya kushuhudiwa kasi kubwa ya kusambaratika Daesh na makundi washirika ya kigaidi ni uwezo wa kivita wa mhimili wa muqawama. Hivi sasa vikosi vya kujitolea vya wananchi vimegeuka kuwa nguzo muhimu na imara ya muqawama katika Mashariki ya Kati; mfano hai wa hilo ikiwa ni harakati ya Al-Hashdu-Sha'abi ya Iraq na makundi mengine kadhaa ya wananchi yanayopambana na magaidi wa kitakfiri huko nchini Syria pia. Kuvitumia vikosi vya kujitolea vya wananchi ni moja ya sababu kuu za kuongezeka uwezo wa kivita wa mhimili wa muqawama.
Wapiganaji wa vikosi vya Al-Hashdu-Sha'abi
Lakini kuna nukta nyengine muhimu pia, nayo ni kwamba stratijia ya kila mara ya kivita inayotumiwa na Daesh kwa ajili ya kukabiliana na mkakati wa kivita wa mhimili wa muqawama imeshakuwa butu. Kueneza hofu na vitisho na kutumia ngao ya binadamu katika medani za mapambano ndizo stratijia mbili kuu ambazo zimekuwa zikitumiwa na kundi hilo la kigaidi na kitakfiri. Lakini ujasiri wa vikosi vya mhimili wa muqawama na hamu kubwa ya kufa shahidi waliyonayo wapiganaji wa vikosi hivyo vimeweza kuzima na kuivunja kikamilifu mikakati ya kueneza hofu na vitisho na utumiaji ngao ya binadamu iliyokuwa ikitekelezwa na Daesh. Ni kama alivyosisitiza Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah katika hotuba aliyotoa siku ya Alkhamisi ya kwamba: "Mafanaikio ya operesheni zilizotekelezwa kwenye miinuko ya mpakani mwa Lebanon na Syria, yamepatikana licha ya mbinu na hila zilizotumiwa na Daesh za kuwafanya raia kama ngao ya kibinadamu". Sababu nyengine muhimu iliyowezesha kushindwa mbinu hiyo ya Daesh ni kutumia Hizbullah stratijia ya "mazungumzo sambamba na vita". Mkakati huo umewezesha kuhamishiwa maeneo mengine wapiganaji wa makundi ya kigaidi na kitakfiri. Ni kama lilivyoandika gazeti la Ash-Sharqul-Awsa't kuwa:"Duru za karibu na kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) zimetuma mwakilishi wake mmoja kwa viongozi wa Hizbullah ya Lebanon ili kuwafikishia pendekezo la kufikia mapatano. Kwa mujibu wa pendekezo hilo makumi ya wapiganaji wa makundi ya kigaidi wataweza kuhamishiwa eneo la Deir ez-Zor". Kuridhia kufanya mazungumzo kundi la kitakfiri la Daesh maana yake ni kushindwa na kutokuwa na taathira tena mikakati ya kundi hilo ya kueneza hofu na vitisho na kutumia ngao ya binadamu.
Wanamapambano wa Hizbullah, mhimili mkuu wa harakati za muqawama katika Mashariki ya Kati
Nukta ya kumalizia ni kwamba vipigo mtawalia na kushindwa mfululizo Daesh na vikosi vya mhimili wa muqawama kumeitia wasiwasi mkubwa Israel na tab'an baadhi ya nchi za Kiarabu ambazo ni waungaji mkono wa kundi hilo. Kuhusiana na nukta hiyo gazeti la Al-Akhbar limechapa makala iliyoandikwa na Ali Haidar, ambapo mwandishi huyo anasema: "Wasiwasi walionao wapangaji sera na viongozi wa Israel ambao umefichuliwa na kanali ya 10 ya televisheni ya Israel unaendana kikamilifu na msimamo rasmi wa Netanyahu kuhusiana na Daesh. Msimamo ambao Netanyahu ameutangaza rasmi na kuujadili katika mazungumzo na Washington na nchi nyingine za Ulaya na hata akarudia kuusisitizia mara kadhaa ni kwamba 'kuangamizwa Daesh kunamaanisha kushindwa Israel katika vita vinavyofuatia' ".
Kwa maelezo haya tunaweza kusema kuwa kushindwa na kuangamizwa Daesh kutakuwa na matokeo mabaya zaidi kwa Israel kuliko ya kushindwa katika vita vya siku 33 vya mwaka 2006 ilivyoanzisha dhidi ya Hizbullah ya Lebanon.../

No comments:

Post a Comment