Thursday, August 31, 2017

KUSHTADI MAUAJI YANAYOFANYWA NA SAUDIA DHIDI YA WATOTO WA YEMEN NA WASIWASI WA JAMII YA KIMATAIFA

Kanali ya televisheni ya Al Mayadeen ya Lebanon imetangaza kuwa watoto wa Yemen wamegeuzwa dango za kutungia shabaha makombora ya ndege za kivita za Saudi Arabia; na hadi sasa karibu watoto elfu tatu wamepoteza maisha katika mashambulio ya anga yaliyofanywa na ndege hizo.
Al- Mayadeen imeongeza kuwa mashambulizi hayo yamejeruhi pia watoto 2,400 na hii ni katika hali ambayo jamii ya kimataifa imeendelea kunyamazia kimya jinai zinazofanywa na Saudia nchini Yemen.
Utawala wa Aal Saud ulianzisha mashambulio ya kijeshi dhidi ya Yemen tangu mwezi Machi 2015 kwa uungaji mkono wa Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo hili. Mashambulio hayo hadi sasa yameshaua zaidi ya Wayemeni 12,000 na kuwajeruhi maelfu ya wengine, wengi wao wakiwa ni watoto wadogo. 
Kutokana na hali hiyo shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch pamoja na mashirika mengine 56 yasiyo ya kiserikali yamelitaka Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa liunde jopo huru la kuchunguza vitendo mbalimbali visivyo vya kiutu, ukiukaji wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na wa sheria za masuala ya kibinadamu uliofanywa nchini Yemen. Ulegevu unaoendelea kuonyeshwa na jamii ya kimataifa mbele ya utawala unaoua watoto wasio na hatia wa Yemen umeupa jeuri utawala huo wa Aal Saud ya kushadidisha jinai zake ikiwemo ya kuua raia zaidi wa Yemen. Kwa kufanya mauaji ya watoto wadogo, Saudi Arabia unataka kuzusha hali ya woga na hofu ili kuwafanya wananchi wa Yemen wasalimu amri mbele ya malengo yake ya kujipanua.
Kuhusiana na suala hilo, gazeti linalochapishwa Dublin, Ireland la Irish Timeslimeashiria taarifa ya pamoja ya wakurugenzi wa taasisi tatu zilizo chini ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali mbaya ya kibinadamu inayotawala nchini Yemen, na kuandika: 
"Vita vya Yemen-Vita dhidi ya watoto".
Wachambuzi wa siasa wameyaelezea mauaji ya halaiki kama ya wananchi wa Yemen yanayofanywa na Saudia kuwa ni moja ya aina mbaya zaidi za ugaidi.
Katika hali na mazingira kama hayo, misimamo ya Katibu Mkuu wa sasa na aliyetangulia wa Umoja wa Mataifa imekuwa ikikosolewa vikali kutokana na kutamka dhahiri shahiri au kwa namna isiyo ya wazi kwamba haiwezekani kulaani mauaji ya watoto wa Yemen kutokana na utegemezi ulionao umoja huo kwa Saudia. Misimamo hiyo inadhihirisha hali mbaya na ya kusikitisha ya kiakhlaqi na kiutu waliyonayo wanasiasa na shakhsia muhimu wa kimataifa. Hatua ya Ban Ki-Moon, Katibu Mkuu aliyetangulia wa Umoja wa Mataifa ya kuiondoa Saudi Arabia kwenye orodha nyeusi ya nchi zinazokiuka haki za watoto na uzembeaji uliofanywa na Katibu Mkuu wa sasa Antonio Guterres wa kushindwa kurekebisha utendaji mbovu wa mtangulizi wake katika kadhia hiyo na kuendelea kuonyesha ulegevu mbele ya jinai zinazofanywa na Saudia vimechangia sana kuufanya utawala huo wa kifalme uwe na jeuri ya kuendeleza jinai zake nchini Yemen.
Baada ya kushindwa kufikia malengo yake nchini Yemen, utawala wa Aal Saud umeshadidisha jinai zake nchini humo kwa kiwango cha kutisha zaidi ili kujaribu kufifilisha kushindwa kwake huko. Hali hiyo imewafanya walimwengu waendelee kushuhudia kila leo maafa yanayowasibu wananchi wa Yemen kutokana na jinai za utawala wa Saudi Arabia dhidi ya wananchi hao wasio na mlinzi.
Profesa Rodney Shakespeare, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Uingereza anaizungumzia nukta hiyo kwamba:
"Uvamizi uliofanywa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen na mauaji ya wanawake na watoto wa nchi hiyo ni jinai ya mauaji ya kimbari".
Kwa kuua hata watoto wadogo, Saudia ambayo ni nembo ya Uwahabi na muenezaji itikadi potofu za kitakfiri na kisalafi imeonyesha kuwa haina mpaka wowote iliojiwekea katika kufanya jinai; na ni kwa kushadidisha jinai hizo tu ndipo itaweza kutuliza kiu yake ya ukatili na umwagaji damu. Mwenendo wa aina hii unakumbusha jinai na ukatili wa Unazi, Ufashisti na Uzayuni katika uga wa uhusiano wa kimataifa.../

No comments:

Post a Comment