Sunday, August 27, 2017

NASAHA ZA KIONGIOZI MUADHAMAMU WA MAPINDUZI YA KIISLAMU KWA SERIKALI YA RAIS ROUHANI

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu jana Jumamosi alionana na Rais Hassan Rouhani na baraza lake la mawaziri kwa mnasaba wa Wiki ya Serikali nchini Iran na kwa mara nyingine amesema kuwa, suala la uchumi ndicho kipaumbele kikuu cha Iran hivi sasa.
Sisitizo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu udharura wa serikali ya Iran kuyapa umuhimu mkubwa masuala ya kiuchumi, ni jambo linalowezi kutathminiwa katika nyuga kadhaa. Moja ya nukta hizo ni uhakika kwamba uchumi dhaifu una madhara mengi sana na ya muda mrefu. Nchi huru duniani haipaswi kuruhusu bei za bidhaa kupanda ovyo, au kuzorota uchumi wake, au kuweko juu kiwango cha ukosefu wa kazi au jamii ya nchi hiyo kukumbwa na ugonjwa wa kupenda kutumia bidhaa za kigeni na kudharau bidhaa zao wenyewe. Moja ya sababu ya kuweko jambo hilo inaweza kuwa ni vikwazo na mashinikizo ya kigeni, lakini chanzo chake kikuu ni kutegemea pato la mafuta na wakati bei ya mafuta inapoporoka katika soko la dunia, uchumi wa nchi hupata pigo kubwa. Ni kwa kutilia mkazo suala hilo ndio maana Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akasema kuwa, kuna wajibu kwa uchumi wa Iran kuacha kabisa kutegemea pato linalotokana na kuuza nje mafuta ghafi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mazungumzo na Rais Rouhani na baraza lake la mawaziri

Jambo hilo linaweza kufanikishwa kwa kuzingatia suhula, uwezo wa kila namna na nguvu kazi mahiri iliyopo nchini Iran; lakini pia lina masharti yake. Kuliko wakati mwingine wowote, hivi sasa Serikali ya Iran ina jukumu kubwa zaidi la kuwa na mipangilio mizuri na kutumia ipoasavyo suhula na nguvu kazi iliyopo nchini katika jitihada za kukuza uchumi na kutoruhusu kabisa suala hilo kuathiriwa na masuala mengine. Takwimu mbalimbali zinaonesha kuweko mafanikio katika juhudi hizo lakini bado kuna safari ndefu ya kufikia kwenye ustawi wa kiuchumi unaokusudiwa na Jamhuri ya Kiislamu.
Kuchukuliwa hatua kama kuimarisha uzalishaji wa bidhaa za ndani, kuuza huduma za teknolojia na kutegemea elimu za kimsingi katika sehemu muhimu na nyeti za kiuchumi hususan kupambana vilivyo na ufisadi na magendo nchini ni katika mambo ambayo yamekuwa yakisisitiziwa mno na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Katika maadhimisho ya Wiki ya Serikali, Rais Rouhani na baraza lake la mawaziri wakisoma QurĂ¡n katika Haram ya Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kusini mwa Tehran

Kama alivyoashiria katika hotuba yake ya jana, maafisa wa Iran wanapaswa kufanya kazi kimapinduzi katika siasa za nje na kwenye upeo wa kidiplomasia. Amesema, kulindwa msimamo na muelekeo wa kimapinduzi na kidini katika siasa za kigeni za Iran ni jambo muhimu sana. Kama ambavyo amesema pia kuwa, inabidi katika uwanja wa udiplomasia kuwe na uharakishaji mambo, kwenda na wakati na watu kuwa macho na kusisitiza kuwa, watu walioko katika masuala ya kidiplomasia humu nchini wana wajibu wa kuona fakhari kuwa ni wanamapinduzi na wajivunie kusimama imara katika ufanikishaji wa malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu kama vile kusimama kidete kukabiliana na uistikbari, kupiga vita dhulma na kupinga mfumo wa kibeberu.
Kwa kweli ni jambo lisilo na shaka kwamba maadui wa taifa la Iran wataendelea kufanya njama za kila namna za kuikwamisha Jamhuri ya Kiislamu kufikia malengo yake hasa ya kiuchumi.
Miongozo iliyotolewa jana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mnasaba wa kuanza kazi serikali ya 12 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa hakika imebainisha nukta muhimu sana nayo ni kwamba, kwa kuzingatia changamoto nyingi zilizopo, na kuendelea kuweko vikwazao dhidi ya Iran, Serikali ina wajibu wa kuongeza miundombinu ya kiuchumi ili kuandaa mazingira mazuri ya kudumu ya kufanikisha uchumi wa kimuqawama wa kutegemea nguvu za ndani na ambao hautetereshwi na matukio ya nje ya nchi. 

No comments:

Post a Comment