Sunday, August 20, 2017

MATUKIO YA KIGAIDI YA UHISPANIA, KISINGIZIO CHA KUZIDISHWA ZAIDI HATUA ZA KIUSALAMA KUKABILIANA NA WAHAJIRI

Ripoti mpya ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji imesema kwamba, idadi ya wahajiri wanaoingia nchini Uhispania imeongezeka.
Msemaji wa shirika hilo Joel Mailman amesema kuwa, idadi ya wahajiri walioingia Uhispania tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2017 hadi sasa kupitia bahari ya Mediterranean ikijumuishwa na wahajiri wanaokaribia 600 ambao waliokolewa katika maji ya bahari ya Alboran karibu na lango la Jabal Tareq (Gibraltar) inafikia elfu tisa. Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya wahajiri hao mwaka huu ni kubwa zaidi  ikilinganishwa na ile ya mwaka jana.
Wahajiri wakijaribu kuokoa maisha yao baharini
Baada ya kufungwa njia za Bahari ya Mediterranean na vilevile njia ya Ugiriki na Italia kuingia barani Ulaya, Uhispania imegeuka na kuwa lango la wafanya magendo ya binadamu kwa ajili ya kutorosha wahajiri haramu kuelekea barani humo.
 Njia ya wakimbizi wanaoelekea Ulaya kupitia Ugiriki ilifungwa baada ya kutiwa saini makubaliano kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki yaliyokuwa na lengo la kuzuia safari za wahajiri wa nchi zilizokumbwa na mgogoro za eneo la Mashariki ya Kati hususan Syria kwenda barani humo.

Serikali ya Italia ikishirikiana na serikali ya Libya yenye makao yake mjini Tripoli katika wiki za hivi karibuni ilituma manoari za kivita kwa ajili ya kuzuia boti zinazobeba wahajiri wanaoeleka barani Ulaya. Kwa msingi huo hivi sasa wafanya magendo ya binadamu wanafanya juhudi za kuingia barani Ulaya kupitia pwani ya Uhispania.
Meli ya Italia ikifanya doria katika maji ya Libya kuzuia wahajiri haramu
Mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea hivi karibuni nchini Uhispania yamepelekea kupuuzwa masuala ya kibinadamu kuhusu wahajiri ambao wamekimbia machafuko, njaa na vita na kuingia kwenye safari yenye hatari kubwa kwenda barani Ulaya kwa ndoto za kupata maisha bora.
 Baadhi ya makundi ya nchi za Magharibi yamekuwa yakitafuta kisingizio cha kukabiliana vikali zaidi na wahajiri na wakimbizi, na inaonekana kuwa mashambulizi ya kigaidi ya hivi karibuni nchini Uhispania yanatumiwa kwa ajili ya kuimarisha hoja ya kukabiliana vikali na wakimbizi hao.

Kuhusiana na suala hilo, siku moja baada ya shambulizi la kigaidi katika jimbo la Catalonia, Uhispania, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Poland Mariusz Błaszczak sambamba na kueleza kwamba, mpambano wa tamaduni mbalimbali unapaswa kutambuliwa kuwa ni kengele ya hatari kwa nchi za Ulaya  alitoa wito wa kuangaliwa upya sera za uhajiri za Umoja wa Ulaya. 

Hayo yanajiri katika hali ambayo kundi la kibaguzi dhidi ya wahajiri limekuwa likitoa nara za kukabiliana na wahajiri na wakimbizi. Wafuasi wa kundi hilo wanaamini kuwa, Waarabu na Waislamu wanaotoka katika nchi zenye machafuko ndio sababu ya matatizo ya kiusalama, kijamii na hata kiuchumi kwa nchi hizo za Ulaya.
Doria zikiendelea baada ya shambulizi la kigaidi Uhispania
Kwa sababu hiyo wanasisitizia  udharura wa kuzuiliwa wahajiri hao kuingia barani Ulaya. Hata hivyo huko Ulaya lipo kundi jingine linalojua vyema chanzo cha ongezeko la wimbi la ugaidi na wala haliwabebeshi wahajiri lawama za kuhusika na matatizo ya watu wa bara hilo. 
André Abdalo Fernandez, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Uhispania hivi karibuni na katika mahojiano na shirika la habari la Sputnik alinukuliwa akisema kuwa, harakati za madola ya Magharibi za kutaka kuziondoa madarakani serikali halali za Libya, Iraq na Syria zimetayarisha mazingira yaliyowapa magaidi fursa ya kutumia ombwe la kisiasa na kiutawala lililojitokeza katika nchi hizo.

 Abdalo Fernandez aliongeza kwa kusema: "Tunajua kuwa baadhi ya waitifaki wetu kama vile Uturuki na Saudi Arabia wanaunga mkono ugaidi na hili ndilo suala ambalo wanatakiwa kulijua viongozi wa nchi za Ulaya. 
Kwa upande mmoja tunadai kupambana na ugaidi na katika upande mwingine tunafanya uhusiano wa kirafiki na nchi ambazo zinaendelea kuyaunga mkono makundi ya kigaidi." Mwisho wa kunukuu.

No comments:

Post a Comment