Thursday, August 10, 2017

MIITO YA UTULIVU YAZIDI KUTOLEWA NCHINI KENYA

Maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi yameenea katika mtaa mwengine wa mabanda mjini Nairobi. Wafuasi wa upande wa upinzani katika mtaa wa mabanda wa Kibera wamechoma moto mipira ya magari na kupaza sauti masaa kadhaa baada ya polisi kukabiliana na waandamanaji huko Kawangware-eneo jengine la mabanda katika mji mkuu huo wa Kenya. Waandamanaji katika baadhi ya ngome za upande wa upinzani waliteremka majiani baada ya kumsikia kiongozi wao Raila odinga akilalamika kumetokea udanganyifu na udukuzi.Tume ya uchaguzi inakiri kulikuwa na njama ya udukuzi lakini njama hiyo haikufanikiwa, tume inasema. Matokeo ya kura zilizohesabiwa hadi sasa yanaashiria ushindi wa rais Uhuru Kenyatta. Hata hivyo upande wa upinzani unasema kiongozi wao Raila Odinga ndie anaestahiki kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais. Itafaa kusema hapa kwamba wasimamizi wote wa kimataifa wamesifu zoezi la uchaguzi nchini Kenya na kusema lilikuwa huru na la uwazi. Wasimamizi hao ambao ni pamoja na wale wa umoja wa Afrika, Jumuia ya madola, Commonwealth , Umoja wa Ulaya na wakfu wa Jimmy Carter wanasema hawaakushuhudia visa vya udanganyifu. Matokeo rasmi hayatotangazwa kabla ya leo ijumaa.

No comments:

Post a Comment