Ujerumani na Ulaya zinataka kuhakikisha vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Urusi havisababishi kuzuka kwa enzi mpya ya uhusiano mbaya kati ya Urusi na nchi za Magharibi
Hayo yameelezwa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel baada ya mazungumzo na Waziri mwenzake wa Marekani Rex Tillerson mjini washington.
Waziri Gabriel alisema alizungumza na na Tillerson jana na kuongeza kwamba amefurahishwa kwamba Rais Donal Trump wa Marekani amekubali kuwa na ushirikiano na washirika wa Marekani kuhusu hatua zaidi za baadaye. Gabriel alisema , " sisi kama Waulaya tuna wasiwasi mkubwa kwamba hili litakuwa na athari isiyotarajiwa kwa Ulaya. Hatutaki kuharibu kabisa uhusiano wa kibiashara na Urusi hasa katika sekta ya nishati."
Mnamo mwezi huu Rais Trump aliidhinisha vikwazo vipya dhidi ya Urusi kutokana na hatua yake ya kulitwaa jimbo la ukraine la Crimea 2014, na kwa kile kilichoelezwa na duru za usalama za Marekani kuwa ni kujiingiza kwa Urusi katika mchakato wa uchaguzi wa Marekani, dai ambalo Urusi imelikanusha.
Gabriel ameikosoa Marekani kwa kuchukua hatua hiyo na kwamba itasababisha makampuni ya Ujerumani yanayohusika na miradi ya nishati nchini Urusi kutozwa faini kwa kukiuka sheria ya Marekani na kusababisha enzi ya mvutano mpya kati ya Urusi na Marekani na pia na nchi nyengine za magharibi.
Kwa upande mwengine waziri wa uchumi wa Ujerumani Brigitte Zypries ameutaka Umoja wa Ulaya ulipize kisasi dhidi ya Marekani ikiwa vikwazo vipya dhidi ya Urusi vitapelekea makampuni ya Ujerumani kuadhibiwa.
Mwakilishi mpya mteule wa Marekani nchini Ukraine Kurt Volker aliiambia Deutsche Welle kwamba Marekani haitokuwa na mkataba mwengine na Urusi bila ya kuzingatia ridhaa ya ukraine au kushauriana na Ulaya. Alisema Marekani imeeleza wazi inaunga mkono kikamilifu mchakato wa Normandy na haina nia ya kuwa sehemu ya utaratibu huo au kukiuka yaliofikiwa.
Mapema wiki hii, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa walitowa wito kuwataka wanajeshi wa Ukraine na wapiganaji wanaotaka kujitenga wakiungwa mkono na Urusi, kuzidisha juhudi ili kuyatekeleza makubaliano ya usimamishaji mapigano. Mzozo huo umeshasababisha kupotea kwa maisha ya zaidi ya watu 10,000. Merkel aliwaambia waandishi habari jana kwamba vikwazo dhidi ya Urusi vitaondolewa pale hali itakapoboreka, mashariki mwa Ukraine.
Gabriel leo yuko mjini Paris alikoelekea moja kwa moja baada ya ziara yake mjini Washington. Amekutana na Rais Emmanuel Macron na amepangiwa pia kuhudhurai kikao cha baraza la mawaziri baada ya mazungumzo yake katika ikulu ya Elysee.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, Reuters, dpa
Mhariri:Iddi Ssessanga