Tuesday, October 3, 2017

SHAMBULIO LA ANGA LA MAREKANI LAUA RAIA 45 NCHINI SYRIA

Shambulizi la anga la Marekani laua raia 45 nchini Syria
Kwa akali raia 45 wameuawa katika shambulizi la anga la hivi punde lililotekelezwa na ndege za kivita za Marekani nchini Syria.
Kwa mujibu wa kanali ya Press TV ya Iran, raia hao waliuawa hapo jana baada ya ndege za kivita za Marekani kushambulia mji wa Raqqah, wilayani al-Touse’eiyah.
Aidha watu wengine kadhaa wamejeruhiwa katika hujuma hiyo ya anga, ambayo pia imeharibu majumba na miundomsingi ya eneo hilo.
Haya yanajiri siku chache baada ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani kukiri kuwa mashambulizi yake ya anga yameua raia wasiopungua 50 katika nchi za Iraq na Syria mwezi uliopita pekee wa Agosti.
Ndege za kivita za US zikiruka katika anga ya Syria
Aidha shambulizi hili jipya linaripotiwa katika hali ambayo, hivi karibuni shirika linalojiita Syrian Observatory for Human Rights lilidai kuwa, watu zaidi ya elfu tatu, wakiwemo raia elfu moja wameuawa katika vita ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu mwezi uliopita wa Agosti.
Muungano wa kijeshi wa Marekani umekuwa ukifanya mashambulizi ya anga nchini Syria tangu Septemba 2014, pasina idhini ya serikali ya Damascus wala Umoja wa Mataifa.

No comments:

Post a Comment