Friday, October 13, 2017

MAREKANI YATAKIWA KUHESHIMU MAKUBALIANO YA NYUKILIA

Waziri wa mambo ya nchi za  nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel ameonya kuwa iwapo rais Donald Trump hataheshimu makubaliano ya nyukilia kati ya Iran na mataiafa sita yenye nguvu basi hatua hiyo itakuwa na athari kimataifa.
Washington, US-Präsident Donald Trump (Reuters/Y.Gripas)
Sigmar Gabriel ameonya kuwa iwapo Marekani itajiondoa au kuchukua hatua yoyote kinyume cha makubaliano hayo  basi  hatua hiyo  italeta athari kati ya Marekani na nchi za ulaya na kutoa mwito kwa mataifa ya ulaya  kuwa na msimamo wa pamoja katika suala hilo pamoja na kuchukua hatua muhimu  na za haraka.
Rais Trump anatarajia kutangaza hii leo mikakati mipya  kufuatilia uwezo wa Iran kuhusiana na nguvu za nyukilia ambapo anatarajiwa pia kutangaza kuwa Marekani haina masilahi na  makubaliano hayo ya kihistoria yaliyofikiwa mwaka 2015.
Hata hivyo maafisa wa Marekani wanasema Trump hatatangaza rasmi kutoyatambua makubaliano hayo bali ataelezea  jinsi asivyokubaliana na jinsi Iran inavyoyatekekeleza  na kuliachia bunge kuamua.
Makubaliano hayo yalisainiwa mwaka 2015 kati ya Iran na nchi sita zenye nguvu duniani ambazo ni pamoja na Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Urusi.
Waziri  wa mambo ya nje wa Ujerumani  Sigmar Gabriel amewaeleza wachapishaji magazeti wa kampuni ya RND kuwa wanapaswa kuwaeleza  wamarekani kuwa mwenendo wao kuhusiana na suala hilo utasababisha mataifa ya ulaya kuwa na msimamo wa pamoja na Urusi na China dhidi ya Marekani.
Trump mara kadhaa amekuwa akitahadharishwa na viongozi wa kidunia na  pia ndani ya uatawala wake juu ya umuhimu wa kuheshimu makubaliano hayo ya nyukilia.
Iran iliondolewa vikwazo vya kiuchumi
Makubaliano hayo  yalishuhudia Iran ikiondolewa  vikwazo vya kiuchumi vilivyokuwa vimewekwa dhidi yake ambapo Iran nayo kwa mujibu wa makubaliano hayo ilipaswa kuacha kuendeleza mipango yake ya kuwa na silaha za nyukilia.
Iran Hassan Rouhani (picture alliance/AP Photo/Iranian Presidency Office) Rais wa Iran Hassan Rouhani
Hata hivyo shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya nyukilia mara kadhaa limekuwa likisisitiza kuwa Iran imekuwa ikitekeleza makubaliano hayo licha ya rais Trump kudai kuwa Iran inakiuka makubaliano ya nyukilia kutokana na kumuunga moono rais wa Syria Bashar al-Assad pamoja na kufanya jaribio la kurusha kombora la masafa.
Marekani inaitaka Iran kuhakikisha kuwa inaacha kuchochea migogoro nchini Syria, Iraq au Yemen lakini Gabriel anasema hilo halipaswi kuwa sharti la kuibana Iran isijihusishe na mpango wa kuwa na silaha za nyukilia.
Rais wa  Iran Hassan Rouhani amemshutumu Trump kuwa anapingana na dunia kutokana na kujaribu kujitenaga na makubaliano hayo ya kihistoria.  Rouhani ameongeza kuwa  sasa itafahamika wazi kuwa  ni nchi gani inafuata sheria na nchi gani inaheshimika kimataifa.
Hadi Jumapili Trump alikuwa hajaliarifu bunge la nchi hiyo  iwapo anaamini kuwa Iran inatekeleza makubaliano ya nyukilia yaiyofikiwa kati yake na nchi sita zenye nguvu duniani.
Iwapo Trump atakataa kukubali kuwa Iran inatekeleza makubaliano hayo basi bunge litapaswa kuamua katika muda wa  siku 60 ni vikwazo gani vipya viwekwe dhidi ya Iran.

No comments:

Post a Comment